Bajeti Wizara ya Habari, Mawasiliano, Teknolojia ya Habari yapungua kwa asilimia 14

May 16, 2024 2:34 pm · admin
Share
Tweet
Copy Link
  • Yafikia Sh180 bilioni kutoka Sh212.4 bilioni.
  • Fedha za matumizi ya kawaida zaongezeka wakati matumizi miradi ya maendeleo yapungua.
  • Kamati yaishauri Serikali kutoa fedha zinazoidhinishwa kwa wakati.

Dar es salaam. Serikali imepunguza zaidi ya Sh31 bilioni kwenye bajeti ya Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari mwaka ujao wa fedha yaani 2024/25 licha ya zaidi ya nusu ya fedha hizo kutumika kwenye miradi ya maendeleo.

Fedha hizo zimepungua kwa kwa asilimia 14.8 sawa na Sh31.6 bilioni kutoka Sh212.5 bilioni iliyoidhinishwa na Bunge kwa mwaka wa fedha 2023/24.

Waziri wa Habari na Mawasiliano Nape Nnauye, aliyekuwa akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi kwa wizara yake katika mwaka wa fedha 2024/25 leo Mei 16, 2024 Bungeni jijini Dodoma aliwaambia wabunge kuwa, kati ya fedha zinazoombwa Sh38.9 bilioni ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida ikiwemo mishahara na matumizi mengineyo.

“Mheshimiwa Spika kati ya fedha hizo Sh28.9 ni kwa ajili ya mishahara na Sh13.9 bilioni ni kwa ajili ya matumizi mengineyo na Sh142.2 bilioni ni kwa ajili ya miradi ya maendeleo ambapo Sh116.5 bilioni ni fedha za ndani na Sh25.6 bilioni ni fedha za nje,” amesema Waziri Nape.

Hata hivyo, bajeti ya matumizi ya kawaida imeongezeka kwa asilimia 19.35 sawa na Sh8.4 bilioni ikilinganishwa na Sh30.5 bilioni ya mwaka wa fedha 2023/24 unaomalizika mwezi Juni 2024.

Ongezeko hilo linatokana na kuongezeka kwa bajeti ya mishahara kwa Sh10.4 bilioni kutoka Sh18.5 bilioni na fedha ya matumizi mengineyo Sh2 bilioni kutoka Sh11.9 bilioni zilizoidhinishwa kwa mwaka wa fedha 2023/24.

Seleman Kakoso ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu aliyekuwa akisoma uchambuzi wa bajeti hiyo amewaambia wabunge kuwa kuongezeka kwa fedha hizo kutaleta manufaa kwa watumishi katika sekta hiyo.

“Mheshimiwa Naibu Spika, kamati inaipongeza Serikali kwa kuongeza fedha za matumizi ya kawaida kwa kuwa, hatua hii itaongeza motisha kwa watumishi kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi zaidi,” amesema Kakoso.

Wakati bajeti ya matumizi ya kawaida ikipaa kwa asilimia 19 bajeti ya maendeleo imepungua kwa asilimia 21.95 sawa na Sh39.8 bilioni ambapo Kakoso amekiri kwamba kamati haijaridhishwa na kupungua kwa fedha za utekelezaji wa fedha za miradi ya maendeleo kwa sababu itaathiri utekelezaji wa miradi.

Kutokana na hilo, kamati imeishauri Serikali iwekeze fedha za kutosha katika miradi na kuhakikisha fedha zilizotengwa na Bunge zinafika kwa wakati na kuwezesha wizara na taasisi zake kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi.

Miongoni mwa miradi ya maendeleo inayotarajiwa kutekelezwa mwaka 2024/25 ni pamoja na  kukamilisha ujenzi wa minara ya mawasiliano ya simu 616 ili kuweza kufikia minara 758 katika kata 713 pamoja na kuanza ujenzi wa minara mingine mipya 636 ili kuhakikisha maeneo yaliyobaki yanapata mawasiliano.

Follow us on TikTok

Nukta Habari

FOLLOW NOW
Subscribe to our channel

Nukta TV

SUBSCRIBE NOW
Rais Samia azindua minara 758, aacha maagizo mazito juu ya mkongo wa taifa

Rais Samia azindua minara 758, aacha maagizo mazito juu ya mkongo wa taifa

Nukta TV

JAJI MKUU: Njia za asili ni mojawapo ya njia halali za utatuzi wa migogoro

JAJI MKUU: Njia za asili ni mojawapo ya njia halali za utatuzi wa migogoro

Nukta TV

Hesabu ya bosi, bei ya mafuta pasua kichwa madereva wa daladala

Hesabu ya bosi, bei ya mafuta pasua kichwa madereva wa daladala

Nukta TV