Vodacom, TPB wazindua huduma mpya ya kidijitali
- Inamwezesha mtumiaji wa M-Pesa kutumia pesa zaidi ya kiwango ulichonacho katika akaunti yake.
- Mteja atatakiwa kurudisha kiwango alichotumia kwa riba ya asilimia 1 kwa siku 18.
- Huduma hiyo ya inajulikana kama M-Pesa Songesha inalenga kuongeza huduma za fedha jumuishi.
Dar es Salaam. Huenda watumiaji wa huduma za fedha kwa njia ya simu za mkononi wakaendelea kufaidika na kuongeza tija katika shughuli zao, baada ya kampuni zinatoa huduma hiyo kuendelea kubuni mifumo rahisi ya upatikanaji wa fedha mtandaoni.
Kampuni ya simu ya Vodacom Tanzania kwa kushirikiana na Benki ya Posta Tanzania (TPB) wamezindua huduma mpya ya M-Pesa Songesha inayowezesha mtumiaji wa M-Pesa kutumia pesa zaidi ya kiwango ulichonacho katika akaunti yake.
Huduma hiyo inaruhusu wateja wa M-Pesa kukamilisha miamala ikiwemo kulipia bili, kutuma pesa kwa ndugu, jamaa na kununua bidhaa mtandaoni pasipo kuwa na fedha za kutosha katika akaunti yake.
Akizungumza na Wanahabari wakati wa uzinduzi wa huduma hiyo, Mkurugenzi wa M-Commerce, Epimack Mbeteni ameleza kuwa wana nia ya kubadili Tanzania kuwa jamii ya kidijitali na wataendelea kuwekeza zaidi katika mifumo ya kifedha inayorahisisha maisha.
“Dhamira yetu ya kuleta mifumo bunifu ya kifedha kwa kutumia simu za mkononi ilitupelekea kutazama kwa makini vikwazo vya mara kwa mara vinavyowazuia wateja wetu kukamilisha miamala yao kwa sababu ya upungufu wa fedha katika akaunti zao.
“Uchunguzi huo umepelekea kuja na ufumbuzi wa kibunifu wa wateja wetu kuweza kukamilisha miamala ya M-Pesa ambayo ingeshindikana kukamilika kwa sababu ya upungufu wa fedha,” amesema Mbeteni .
Amesema mtumiaji wa M-Pesa ataweza kupata huduma hiyo kwa kupiga *150*00# na kuchagua huduma za kifedha na kujiunga na huduma hiyo ya M-Pesa Songesha na atapata kiwango anachostahili au atachoweza kutumia kukamilisha miamala yake.
Lakini kiasi hicho kitarejeshwa pale ambapo mteja atakapokea fedha katika akaunti yake ya M-Pesa.
“Kiwango hicho kina riba ya asilimia moja kwa siku 18 na wateja wetu wanaweza kufanya miamala kwa kutumia huduma hii kadri watakavyo ikiwa ni ndani ya kikomo cha kiwango chao.
- NMB yaingiza sokoni huduma tatu za kidijitali kwa mpigo
- Hisham Hendi kuipaisha Vodacom Tanzania?
- Kigogo wa Safaricom kuiongoza Vodacom Tanzania
Tumeungana na benki ya TPB kuwezesha huduma hii na ili kuamua kiwango mteja anachostahili, benki itatumia taratibu zilizowekwa kulingana na miamala ya mteja husika katika matumizi yake ya M-Pesa,” alisema Mbeteni.
Huduma hiyo inazinduliwa wakati Vodacom Tanzania kiendelea kuongoza katika utoaji wa huduma za fedha kwa njia ya simu za mkononi na umiliki wa soko la mawasiliano ya simu nchini.
Ripoti mpya ya Takwimu za Mawasiliano ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), inaonyesha kuwa M-Pesa inaongoza kuwa na wateja wengi wanaofikia milioni 9 na kumiliki soko la huduma za fedha kwa njia ya simu za mkononi kwa asilimia 40 kati ya makampuni sita yanayotoa huduma hiyo.
Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa TPB, Moses Manyatta amesema lengo la huduma hiyo ni kufanya huduma jumuishi kwenye masuala ya fedha ili kuhamasisha Watanzania kujiwekea akiba na kupata mikopo kwa urahisi kuendesha shughuli zao.
“Songesha ni kila kitu na inapatikana masaa 24 kwa siku saba kupitia simu yako ya mkononi. Tunajivunia kuwa na uhusiano huu na tuna imani kwamba mapinduzi haya yatasaidia katika huduma jumuishi za kifedha,” amesema Manyatta.
Latest