Mambo muhimu ya kuzingatia ili kuzuia vifo vya wajawazito
- Ni pamoja na kuwatambua mapema wajawazito wenye vihatarishi na kuhudhuria kliniki mara kwa mara.
Dar es Salaam. Baada ya kuona mikoa inayoongoza kwa vifo vya wajawazito pamoja na sababu zinazochangia tatizo hilo, ni muhimu kuangalia hatua zinazoweza kusaidia kuokoa maisha ya mama na mtoto wakati wa ujauzito, kujifungua na baada ya kujifungua.
Wataalamu wa afya wanaeleza kuwa sehemu kubwa ya vifo hivi vinaweza kuzuilika kupitia ufuatiliaji wa karibu wa ujauzito na upatikanaji wa huduma bora za afya.
Kulingana na wataalamu hao Nukta Habari tunakuleta mambo ya kuzingatia ili kuzuia vifo vya wajawazito.
Kuwatambua mapema wajawazito wenye vihatarishi
Hatua ya kwanza ya kuzuia vifo vya wajawazito ni kutambua mapema wanawake wenye hatari kubwa ya kupata matatizo wakati wa ujauzito au kujifungua.
Hawa ni pamoja na wenye kisukari, presha ya ujauzito, upungufu wa damu wa muda mrefu, ugonjwa wa selimundu au historia ya upasuaji wa kizazi.
“Mama anapoanza kliniki ni lazima aelezwe dalili zote za hatari na viashiria vyote vya hatari kuhusiana na ujauzito wake,” anasema Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Wanawake Emmanuel Masali, kutoka Hospitali ya Kitonka jijini Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa daktari huyo, wanawake wenye changamoto hizo wanapaswa kufuatiliwa kwa karibu zaidi ili matatizo yaweze kubainika mapema na kushughulikiwa kabla hayajaleta madhara kwa mama au mtoto.
Kuhudhuria kliniki mara kwa mara na kufanya vipimo muhimu
Huduma za kliniki ni msingi muhimu katika kuhakikisha ujauzito unafuatiliwa kwa karibu. Vipimo vya damu, mkojo, sukari na “ultrasound’ husaidia kubaini changamoto mapema na kutoa matibabu kabla hali haijawa mbaya.
Kadiri ujauzito unavyokaribia mwisho, Dk Masali anabainisha kuwa ufuatiliaji huongezwa ili kufuatilia ukuaji wa mtoto na hali ya mama.
Hatua hii husaidia kugundua mapema matatizo yanayoweza kuhatarisha maisha ya mama na mtoto.
Kuweka ufuatiliaji wa karibu wakati wa uchungu
Wakati wa uchungu, wataalamu hutumia vifaa maalum kufuatilia maendeleo ya kujifungua na kubaini mapema matatizo yanayoweza kuhatarisha maisha ya mama au mtoto.
Ufuatiliaji huu wa karibu husaidia wataalamu kufanya maamuzi ya haraka pale uchungu unaposhindwa kuendelea kawaida au mtoto anapoonyesha dalili za kuwa katika hatari.
Kujifungulia hospitali zenye huduma kamili za dharura
Moja ya mapendekezo makubwa ya wataalamu ni kuhakikisha wajawazito wanajifungulia katika hospitali zenye uwezo wa kufanya upasuaji wa dharura na kutoa huduma za haraka pale matatizo yanapotokea.
“Tunashauri sana kina mama wajifungulie katika hospitali ambayo ina uwezo wa kufanya upasuaji wa dharura pale inapohitajika,” anasisitiza Dk Masali.
Anasema baadhi ya vifo hutokana na kuchelewa kupata huduma wakati wa kujifungua, hususan pale mtoto anapokwama tumboni au uchungu kushindwa kuendelea kawaida.
Kudhibiti kutokwa damu na upatikanaji wake baada ya kujifungua
Kwa mujibu wa Shirika la Afya Dunia (WHO), kutokwa na damu nyingi baada ya kujifungua ni moja ya sababu kuu za vifo vya wajawazito.
Mwanamke mwenye afya njema anaweza kupoteza maisha ndani ya saa chache ikiwa hatapatiwa msaada wa haraka.
WHO inaeleza kuwa matumizi ya dawa za kuongeza mkazo wa mfuko wa uzazi mara baada ya kujifungua husaidia kupunguza hatari hiyo.
Hatua hii ni muhimu katika kuzuia vifo vinavyotokana na upotevu mkubwa wa damu.
Dk Masali anaeleza kuwa hospitali zinapaswa kuwa na akiba ya damu ya kutosha kwa ajili ya kuwahudumia kina mama wanaopoteza damu nyingi wakati au baada ya kujifungua.
Anasisitiza kuwa upatikanaji wa damu kwa wakati ni muhimu katika kuokoa maisha na kuzuia madhara yanayoweza kusababishwa na upungufu mkubwa wa damu mwilini.
Kuzuia maambukizi na kudhibiti shinikizo la damu la ujauzito
WHO inaeleza kuwa maambukizi baada ya kujifungua yanaweza kuzuilika kwa kuzingatia usafi wakati wa kujifungua na kutambua mapema dalili za maambukizi ili kupata matibabu kwa wakati.
Vilevile, shinikizo la damu la ujauzito (pre-eclampsia) linapaswa kugunduliwa na kudhibitiwa mapema kabla halijasababisha degedege na matatizo mengine yanayohatarisha maisha. Utambuzi na matibabu ya mapema husaidia kulinda afya ya mama na mtoto.
Kupunguza vifo vya wajawazito kunahitaji elimu ya kutosha kwa watalamu wa afya, na mjamzito ili kuokoa maisha ya kiumbe kilichopo tumboni.