Vodacom Tanzania yaripoti faida ya Sh90.5 bilioni
- Sehemu kubwa ya faida hiyo imechochea na kuongezeka kwa mapato yatokanayo na huduma na mikakati ya kubana matumizi.
Dar es Salaam. Kampuni ya huduma za simu Vodacom Tanzania imetangaza ongezeko la faida baada ya kodi la zaidi ya Sh37 bilioni ndani ya mwaka mmoja na kufikia Sh90.5 bilioni katika mwaka wa fedha ulioishia Machi, 2025 ikichochewa zaidi na kuongezeka kwa mapato ya huduma na mkakati wa kuminya matumizi.
Ongezeko hilo la faida ni habari njema kwa wawekezaji wa kampuni hiyo ambao wamekuwa wakisubiri kwa hamu kuongezeka kwa gawio ili kutunisha zaidi mifuko yao.
Mkurugenzi Mtendaji wa Vodacom Tanzania Philip Besiimire ameeleza katika ripoti ya awali ya mwaka wa fedha unaoishia Machi 2025 kuwa kampuni hiyo ilirekodi utendaji imara baada ya mapato yatokanayo na huduma kukua kwa asilimia 20.5 ndani ya mwaka mmoja.
Sehemu kubwa ya ukuaji wa mapato yatokanayo na huduma yaliyochochewa na ukuaji imara wa huduma za kifedha za M-Pesa zilizokua kwa asilimia 29.3 na intaneti kwa asilimia 21.6.
Vodacom yafikia Sh1.5 trilioni mapato ya jumla
Utendaji huo umefanya mapato ya jumla ya Vodacom Tanzania kuongezeka hadi takriban Sh1.515 trilioni kwa mwaka ulioishia Machi 2025 kutoka Sh1.258 trilioni mwaka uliopita na kuifanya kuwa moja ya kampuni kubwa nchini zenye kiwango kikubwa cha mapato.
Uchambuzi wa taarifa hizo za awali za kifedha umebainisha kuwa mapato yatokanayo na huduma za sauti ya Vodacom Tanzania yameendelea kuimarika ndani ya miaka mitatu baada ya kurekodi ya ukuaji wake kusinyaa miaka ya nyuma.
Ripoti hiyo inaonyesha mapato ya huduma za sauti (mobile voice) yalikuwa takriban Sh310.6 bilioni mwaka ulioishia Machi 2025 kutoka Sh285.77 bilioni zilizorekodiwa kipindi kama hicho mwaka jana.
“Mikakati yetu ya kupunguza matumizi yalisaidia kuokoa Sh59.2 bilioni jambo lililochochea ukuaji wa faida ya kiundeshaji kwa asilimia 55 na ongezeko la faida baada ya kodi kwa asilimia 69.4 na kufikia Sh90.5 bilioni,” amesema Besiimire katika ripoti hiyo.
Matumizi ya matangazo yapigwa panga
Katika mwaka ulioishia Machi 2024, kampuni hiyo iliyoorodheshwa katika Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE) ilipata faida ya takriban Sh53.43 bilioni baada ya utendaji wake kuendelea kuimarika kutoka katika hasara ya Sh 20.23 iliyorekodiwa mwaka 2022.
Miongoni mwa maeneo yaliyopigwa zaidi panga katika matumizi ndani ya kampuni hiyo kubwa ya mawasiliano na gharama zinazohusiana na matangazo na habari ambazo zilipunguzwa kwa zaidi ya Sh5 bilioni sawa na asilimia 15.
Matumizi hayo ya matangazo (publicity) yamekuwa yakipungua mwaka hadi mwaka na sasa yamepunguzwa kutoka takriban Sh30.36 bilioni katika mwaka wa fedha ulioishia Machi 2024 hadi Sh25.81 bilioni mwaka ulioishia Machi mwaka huu.
Latest



