NMB yaingiza sokoni huduma tatu za kidijitali kwa mpigo

August 15, 2018 11:53 am · Daniel
Share
Tweet
Copy Link
  • Huduma hizo zitakuwa zikipatikana katika app mpya ya NMB Klik na ujumbe mfupi wa maneno (Short codes). 
  • BoT yazitaka benki kuongeza ubunifu kuhakikisha sekta ya benki inakuwa jumuishi na Watanzania wanaachana na matumizi ya fedha za mifukoni.

Dar es salaam. Katika kukabiliana na ushindani na kasi ya mabadiliko ya teknolojia nchini, Benki ya NMB Plc imeingiza sokoni huduma tatu kwa mpigo za kibenki kidijitali ikiwemo ya kufungua akaunti ya benki ndani ya dakika tatu kwa kutumia simu ya mkononi. 

Safari hiyo ya kijiditali ya NMB ambayo ni moja ya mapinduzi makubwa katika sekta hiyo ya benki nchini ina lengo la kukuza sekta ya fedha jumuishi na kupunguza matumizi ya pesa za mifukoni (cash) katika ufanyaji wa miamala ya kifedha.

Mkuu wa Idara ya Ubunifu wa benki hiyo, Josina Njambi amesema huduma tatu zilizozinduliwa leo (Agosti 14, 2018) zinajumuisha namna mpya ya kujiunga na benki (accessebility), namna mpya inayomwezesha mteja kutumia benki yake kikamilifu kidijitali na huduma ya tatu inalenga zaidi kujenga jamii isiyotegemea pesa za mifukoni (Cashless society).

Njambi amesema huduma hizo zitakuwa zinafuata nguzo tano ambazo ni kufikiwa kwa urahisi popote ulipo Tanzania, kurahisisha huduma za benki hiyo kwa wateja wake, huduma za haraka, iliyosalama na huduma kutokana na mahitaji ya wateja.

Kwa wanaotumia simu janja maarufu kama smartphone, huduma hizo zinapatikana katika programu ya simu iitwayo NMB Klik wakati wale wenye simu za kawaida zilizopewa jina la utani za “Vitochi” watatumia ujumbe mfupi wa maneno (Shortcode Sms).

Katika mabadiliko hayo, Njambi amesema wateja wa benki hiyo wanapofungua akaunti hawatalazimika kutumia “fomu za makaratasi, kulipia gharama za kufungulia, masharti ya kuchosha na wala hawatahitajika kufika katika tawi la benki”.

“Mtu anayetaka kufungua akaunti atahitajika kuwa na moja ya vitambulisho vya aina tano ambavyo ni leseni ya gari, kitambulisho cha taifa, kitambulisho cha kupigia kura, pasi ya kusafiri na kitambulisho cha Mzanzibari mkazi mteja wa benki ya NMB ataweza kutumia kitambulisho kimoja wapo kufungulia akaunti kupitia simu kwa kuboonyeza *150*66# kujiunga.

“Huduma hiyo ambayo iko katika lugha mbili za Kiswahili na Kiingereza itatumika katika simu za aina zote za kawaida na smartphone ambapo sasa kufungua akaunti ni chini ya dakika tatu huku namba ya simu ikiwa ndio namba ya akaunti yako  unaweza kutumia hapo hapo na katika huduma zetu zote,” amesema Njambi.

Safari hiyo ya NMB kijiditali imekuja wakati Tanzania ikivunja rekodi katika ukuaji wa sekta ya mawasiliano baada ya kufikisha watumiaji wa intaneti takriban milioni 23 mwaka 2017, kiwango ambacho ni zaidi ya mara tatu ya kile kilichorekodiwa miaka mitano iliyopita.

Takwimu mpya za robo ya mwisho wa mwaka 2017 za Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) zinaonyesha kuwa idadi ya watumiaji wa intaneti ilipaa kwa asilimia 15 hadi watumiaji milioni 22.99 mwaka 2017 kutoka milioni 19.86 mwaka 2016

Katika app yao ya  NMB Klik, benki hiyo imeeleza kuwa itawawezesha wateja wao kupata huduma zote ikiwemo kuhamisha hela, kulipia huduma mbalimbali hata kuomba mshahara (Salary advance) na kujua mahitaji ya mkopo wake ikiwa ni kiasi gani anatakiwa kukopa kulingana na mshahara wake bila kwenda kwenye tawi la benki.

Vilevile Njambi amesema huduma hiyo itamwezesha mteja kubadilisha  fedha za kigeni na kuweza kutuma kulingana na mahitaji yake kwa kulingana na viwango vya siku hiyo pamoja na huduma zingine kwenye akaunti yake.

Huduma ya tatu iliyoingizwa sokoni leo na NMB Plc ni huduma ya mpya ya malipo kutumia QR Codes pamoja na wale wa simu za kawaida pia wataweza kufanya miamala ya malipo kwa kupiga *150*66#  ambapo huduma hiyo pia inatumika kupitia Visa na MasterCard kwa wateja wao. 

Ushindani katika sekta ya fedha nchini unazidi kukua hasa kutokana na matumizi makubwa ya teknolojia katika kufanikisha miamala ambayo imechagizwa na ubunifu wa kampuni za huduma za simu katika biashara hiyo. Tayari baadhi ya kampuni zinazotoa huduma za kifedha nchini kidijitali zimeanza kutumia teknolojia ya QR Codes kulipia huduma ikiwemo Tigo Pesa na Masterpass ya Mastercard.

Mkuu wa Idara ya Ubunifu wa benki hiyo, Josina Njambi akiwasilisha namna huduma tatu mpya za kibenki kidijitali zitakavyokuwa zinafanya kazi. Picha|NMB.

Ili kutumia vyema kasi ya mabadiliko ya teknolojia, Naibu Gavana Mkuu wa Benki Kuu ya Tanzania (BOT), Dk Bernard Kibesse imezishauri benki nchini kuimarisha mfumo wa benki jumuishi ili kuongeza usalama wa pesa za wateja na kuachana na mfumo wa zamani wa kubeba fedha mkononi.

“NMB wanatimiza ndoto ambayo watanzania tumeiota ya kuacha kutumia pesa za mfukoni na sasa kutumia simu kufanya miamala na tunataka matumizi ya vifaa yaongezeke,” amesema Dk Kibesse. 

Amesema ili mifumo hiyo ifanye kazi na kuwafikia watu wengi ambao wanatumia huduma za benki nchini, benki zinapaswa kuongeza ubunifu ili kuongeza usalama wa fedha za wateja.

“Benki Kuu kama msimamizi na mwangalizi wa mabenki haya tuna wajibu wa kuangalia usalama wa pesa za wateja lakini pia tuna wajibu wa kuhakikisha kwamba ubunifu katika nchi hii unakua,” amesema Dk Kibesse. 

Ikiwa benki zitakuwa na mifumo na usimamizi mzuri wa mwenendo wa miamala ya fedha zinazoingia na kutoka utasaidia nchi kuimarisha sarafu yake duniani. 

Enable Notifications OK No thanks