Hisham Hendi kuipaisha zaidi Vodacom Tanzania?

March 27, 2019 12:57 pm · Rodgers Raphael
Share
Tweet
Copy Link

Hisham Hendi (kushoto) Mkurugenzi Mtendaji mpya atakayeongoza kampuni ya Vodacom Tanzania akiwa na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Vodacom, Ali Mafuruki. Picha|Mtandao.


  • Ni Mkurugenzi Mtendaji mpya aliyeteuliwa na Bodi ya Wakurugenzi kuiongoza kampuni hiyo baada ya kukaimu nafasi hiyo tangu Septemba 2018. 
  • Anachukua nafasi iliyopaswa kushikiriwa na Sylvia Mulinge, raia wa Kenya ambaye hakupata vibali vya kufanya kazi hapa Tanzania. 

Dar es Salaam. Hatimaye kitendawili cha uongozi katika kampuni ya mawasiliano ya simu ya Vodacom Tanzania kimeteguliwa, baada ya Bodi ya Wakurugenzi kumteua Hisham Hendi kuwa Mkurugenzi Mtendaji mpya atakayeongoza kampuni hiyo. 

Uteuzi huo umekuja baada ya Mkurugenzi Mtendaji aliyeteuliwa awali, Sylvia Mulinge, raia wa Kenya kutopata kibali cha kufanya kazi nchini alichoomba tangu Mei 23, 2018 ambapo Hendi alikuwa anakaimu nafasi hiyo tangu Septemba 2018 mpaka leo. 

Mulinge alitakiwa kuchukua nafasi iliyoachwa na Ian Ferrao aliyemaliza muda wake. 

Taarifa ya uteuzi wa kigogo huyo mpya wa Vodacom zimetolewa leo (Machi 27, 2019) na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Vodacom, Ali Mafuruki ambapo imeeleza kuwa Hendi ana uzoefu na uwezo wa kuipeleka mbali kampuni hiyo.

“Chini ya uongozi wake, kampuni imekua kiutendaji kwenye ushindani mkubwa wa kimasoko” inasomeka sehemu ya taarifa hiyo.

Hendi ambaye ana shahada ya kwanza ya Biashara kutoka Chuo Kikuu cha Cairo, Misri ambapo mwaka 2016 alikabidhiwa kuongoza kitengo cha Masoko na Mauzo cha Vodacom Tanzania na alifanya vizuri katika utendaji wake.

Kigogo huyo atakuwa na kibarua kigumu kuendeleza mafanikio ya watangulizi wake ambapo mpaka sasa Vodacom Tanzania iko katika orodha ya makampuni ya Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE) na inafanya vizuri. 

Ana uzoefu wa zaidi ya miaka 15 kwenye masuala ya mawasiliano pepe (Telecommunication) akiwa amefanya kazi na makampuni mbalimbali katika nchi za Uingereza, Misri na Afrika Kusini. 

Pia amefuzu mafunzo ya uongozi ya “Vodafone’s Global Leadership Program” huko London na kupata cheti cha biashara kutoka Chuo Cha IMD nchini Switzerland.

Kwa mujibu taarifa ya Mafuruki, wana imani na Hendi kuwa ataisaidia Vodacom kupata mafanikio makubwa kwa sababu una uzoefu wa kimataifa katika shughuli za mawasiliano. 

“Tunauhakika kuwa chini ya uongozi wake, Vodacom Tanzania itaendela kuleta mchango sawia kwenye jamii inazozihudumia na kusaidia Tanzania kufikia malengo yake kimaendeleo,” imesomeka taarifa hiyo iliyosainiwa na Mafuruki. 

Enable Notifications OK No thanks