Vodacom Tanzania yaripoti faida ya zaidi ya Sh42 bilioni
- Kiwango hicho cha faida baada ya kodi kimerekodiwa katika nusu ya kwanza ya mwaka wa fedha wa kampuni hiyo inayoishia Septemba 30, 2024.
- Faida hiyo ni sawa na ongezeko la asilimia 42.4 kutoka Sh29.6 bilioni zilizorekodiwa kipindi kama hicho mwaka jana.
Dar es Salaam. Kampuni ya mawasiliano ya Vodacom Tanzania imeripoti ongezeko la faida baada ya kodi hadi kufikia Sh42.17 bilioni katika nusu ya kwanza ya mwaka wa fedha ulioishia Septemba 30 mwaka huu, ikichagizwa zaidi na kupaa kwa mapato ya huduma na hatua za kubana matumizi.
Ripoti ya awali ya kifedha ya Vodacom iliyotolewa leo Novemba 7, 2024 inabainisha kuwa faida hiyo imeongezeka kwa asilimia 42.4 ndani ya mwaka mmoja kutoka Sh29.6 bilioni iliyorekodiwa kipindi kama hicho mwaka 2023.
Kuongezeka kwa faida kwa kampuni hiyo kubwa zaidi kwa idadi ya watumiaji wa simu za mkononi, ni miongoni mwa dalili za kuimarika kwa sekta ya mawasiliano nchini baada ya kuyumba kidogo miaka miwili iliyopita kufuatia uamuzi wa Serikali wa kuongeza tozo kwenye miamala ya kifedha kupitia simu ya mkononi.
Shirika la umoja wa watoa huduma za simu duniani GSMA lilieleza katika mfululizo wa ripoti zake kuhusu athari za tozo hizo kuanzia mwaka 2022 kuwa uamuzi huo wa Serikali uliathiri mapato ya kampuni za simu na kuwatosa baadhi ya watumiaji wa huduma za kifedha baada ya kushindwa kumudu gharama za miamala.
Hata hivyo, Serikali iliondoa kabisa baadhi ya tozo na kushusha nyingine jambo lilolotoa ahueni kwa watumiaji na kampuni za huduma za simu nchini.
“Mapato yatokanayo na utoaji huduma yaliongezeka kwa asilimia 19.1 hadi Sh718.2 bilioni yakichagizwa na mwenendo imara wa ukuaji kibiashara,” imesema ripoti hiyo.
Vodacom imeeleza kuwa idadi ya wateja iliongezeka kwa asilimia 13.2 hadi kufikia wateja milioni 20.9 huku wastani wa mapato kwa mteja (ARPU) ukiongezeka kwa asilimia 1.9 kutokana na kuongezeka kwa matumizi ya intaneti na mwitikio chanya wa ununuzi wa bidhaa za kampuni hiyo.
M-Pesa yachangia pakubwa
Huduma za kifedha za M-Pesa, kwa mujibu wa ripoti hiyo, zimeendelea kuchangia sehemu kubwa ya mapato ya kampuni hiyo iliyoorodheshwa katika Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE) baada ya kuchangia zaidi ya theluthi ya mapato yote katika nusu ya kwanza iliyoishia Septemba 30, 2024.
Uchambuzi wa takwimu za kifedha wa kampuni hiyo uliofanywa na Nukta Habari unaonyesha kuwa Vodacom ilirekodi mapato ya M-Pesa kiasi cha Sh274. 24 bilioni katika nusu ya kwanza ikiwa ni ongezeko la asilimia 27.9 kutoka kutoka Sh214.4 bilioni zilizoripotiwa kipindi kama hicho mwaka jana.
Kwa kiwango hicho, M-Pesa ilichangia zaidi ya theluthi au takriban asilimia 38 ya mapato yote ya kampuni hiyo ya Sh730.2 bilioni yaliyorekodiwa katika robo mbili za awali za mwaka wa fedha ulioishia Septemba 30, 2024.
Bana matumizi yaokoa Sh28 bilioni
Mkurugenzi Mtendaji wa Vodacom, Philip Besiimire amesema utendaji wa kifedha wa kampuni hiyo unaridhisha na kwamba hatua za kubana matumizi zimesaidia kuokoa Sh28 bilioni ukiachilia mbali athari za mabadiliko ya sarafu za fedha za kigeni.
“Nina matumaini kuwa mazingira ya biashara yataendelea kuwa imara hapo mbeleni. Sera za chanya za Serikali na mikakati yake vinaendelea kukuza na kuimarisha mazingira ya biashara yanayotusaidia kutekeleza malengo yetu ya kuwaunganisha Watanzania ili kufikia mustakabali bora,” amesema Besiimire.