Waziri Lugola ang’olewa, Simbachawene kumrithi mambo ya ndani Tanzania

January 24, 2020 5:38 am · Mwandishi
Share
Tweet
Copy Link
  • Anakuwa waziri wa tatu kufurushwa na Rais Magufuli ndani ya miaka minne ya utawala wake katika wizara hiyo. 
  • Rais Magufuli amefuta pia kazi Mkuu wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji. 

Dar es Salaam. Baada ya kutumikia Serikali kwenye baraza la mawaziri kwa mwaka mmoja na nusu, Kangi Lugola, Waziri wa Mambo ya Ndani ameng’oka na nafasi yake imechukuliwa na George Simbachawene.

Kabla ya uteuzi huo, Simbachawene alikuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira).

Nafasi ya Simbachawene aliyedumu katika nafasi hiyo kwa miezi sita sasa itachukuliwa na Mbunge wa Ilala, Mussa Zungu aliyeteuliwa leo (Januari 23, 2020) kuwa waziri katika wadhifa huo. 

Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi John Kijazi amesema katika matangazo mubashara kuwa uteuzi wa Lugola, umetenguliwa leo na Rais John Magufuli.

Taarifa ya Balozi Kijazi ni kama imepigia sakafu kufurushwa kwa Lugola katika nafasi yake ambaye mapema asubuhi alishambuliwa vikali na Rais Magufuli kwa kushindwa kusimamia wizara yake vizuri kiasi cha kuliacha Jeshi la Zimamoto na Uokoaji kuingia mkataba wa “mradi wa hovyo” wenye thamani ya zaidi ya Sh1 trilioni. 

 “Hivi karibuni kulikuwa na mkataba wa ajabu unatengenezwa ndani ya Wizara ya Mambo ya Ndani wenye thamani ya Euro milioni 408. Ni trilioni moja point something. Mradi huo umetayarishwa na kusainiwa na Kamishna Jenerali wa fire (Zimamoto),” amesema Rais Magufuli akionekana kukasirishwa.

“Haujapangwa kwenye bajeti, haujapitishwa na Bunge…wakati wa vikao na kampuni moja nafikiri kutoka Romania, wahusika wote wa Tanzania walipokuwa wanaenda kwenye majadiliano pale wanalipwa seating allowance (posho ya kikao) ya $800 (Sh1.8 milioni) bado ya kulipiwa tiketi ya ndege,” ameongeza Rais Magufuli. 


Zinazohusiana:


Rais Magufuli amesema maofisa hao wa Serikali wakiwemo kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali wameingia makubaliano ambayo ndani yake yanasema iwapo watataka kuvunja mkataba itabidi masuala yote yaliyokuwa yameanza kutekelezwa yaendelee kutekelezwa.

“Sasa mimi Lugola nampenda sana ni mwanafunzi wangu nimemfundisha Sengerema Sekondari, pamoja na mwili wake na ukubwa wake, ni mwanafunzi…lakini kwa hili hapana nilitegemea hata nitamkuta hayupo,” amesema Rais Magufuli.

Wengi watamkumbuka Lugola aliyeingia kwenye baraza hilo mwanzoni mwa Julai 2018 kama moja ya mawaziri walionekana kuwa wazalendo na watiifu katika Serikali ya Rais Magufuli kiasi cha kushona mashati yenye nakshi za bendera ya Taifa.

Lugola, aliyekuwa maarufu kwa kutembea na ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM), alichukua nafasi ya Mwigulu aliyefutwa kazi wakati huo. 

Wakati Lugola aking’ooka, Katibu Mkuu wa wizara hiyo Meja Jenerali Jacob Kingu alijiuzuru jana ikiwa ni sehemu ya kuwajibika kutokana na suala hilo. Meja Jenerali Kingu ameteuliwa kuwa balozi.

Ndani ya miaka minne ya awali ya Rais Magufuli, Wizara ya Mambo ya Ndani inaingia kwenye orodha ya wizara zilizoongozwa na mawaziri wengi ndani ya muda mfupi nchini, Simbachawene akiwa ni waziri wa nne. 

Wakati akiingia madarakani mwishoni mwa mwaka 2015, Dk Magufuli alimteua Charles Kitwanga kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani kabla ya kumfurusha Mei 2016. Nafasi ya Kitwanga ilichukuliwa na Mwigulu ambaye naye hakudumu sana.

Katika taarifa yake ya jioni hii, Dk Kijazi amesema Mkuu wa Jeshi la Zimamoto Kamishna Jenerali, Thobias Andengenye naye amefutwa kazi baada ya uteuzi wake kutenguliwa.

“Nafasi ya Kamishna Jenerali wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji itatangazwa hapo baadaye,” amesema Dk Kijazi.

Mapema mchana leo taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, Gerson Msigwa imesema mradi huo ulihusu ununuzi wa vifaa vya zimamoto na uokoaji.

Hatua ya Meja Jenerali Kingu imesifiwa na Rais Magufuli kama ni hatua nzuri ya kuwajibika.

“Nampongeza sana Maor General (Meja Jenerali) Kingu aliyekuwa Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Ndani kwa kuwajibika. Hii imempa heshima kwamba angalau ametambua kwamba inawezekana hakuyafanya yeye provided (ikizingatiwa) yeye ni Katibu Mkuu amewajibika kwa hilo. Nampongeza sana na nitaendelea kumheshimu,” amesema Rais Magufuli.

Rais ameagiza Takukuru kufanya uchunguzi haraka wa mkataba huo ulioingiwa na Jeshi la Zimamoto na kampuni ya nje kwa kuwa hauna tija kwa nchi.

Masoko & Zaidi
Loading…
No recent matches
No upcoming matches
/
No matches found for this filter
26 Aug, 2026 · TZS
No forex gainers today
No forex losers today
Forex rates unavailable
26 Aug, 2026 · TZS
No gainers today
No losers today
26 Aug, 2026
No active movers today

Inaendeshwa na Nukta AI

Follow us on TikTok

Nukta Habari

FOLLOW NOW
Subscribe to our channel

Nukta TV

SUBSCRIBE NOW
Elimu ya kodi mwarobaini wa wafanyabiashara kuikwepa TRA, ianzie shuleni

Elimu ya kodi mwarobaini wa wafanyabiashara kuikwepa TRA, ianzie shuleni

Nukta TV

Rais Samia: Serikali chini ya Magufuli haikutaka kuyumbishwa kukamili kwa JNHPP

Rais Samia: Serikali chini ya Magufuli haikutaka kuyumbishwa kukamili kwa JNHPP

Nukta TV

Rais Samia: Umeme wa SGR hautoingiliwa, Dodoma umeme uhakika 24/7

Rais Samia: Umeme wa SGR hautoingiliwa, Dodoma umeme uhakika 24/7

Nukta TV