Rais Magufuli awafuta kazi Tizeba, Mwijage joto la korosho likipanda

Nuzulack Dausen 1117Hrs   Novemba 10, 2018 Habari
  • Mabadiliko hayo pia yamejumuisha uteuzi wa manaibu mawaziri wanne akiwemo Mbunge wa Ukonga, Mwita Waitara aliyehamia CCM hivi karibuni.
  • Pia ameivunja Bodi ya Korosho Tanzania (CBT) na kutengua uteuzi wa Mwenyekiti wa bodi hiyo, Anna Abdallah.
  • Mabadiliko hayo yanakuja wakati kukiwa na msuguano wa chini kwa chini baina ya Serikali na wafanyabiashara wa korosho kutokana na kudorora kwa ununuzi wa zao hilo.

Dar es Salaam. Rais John Magufuli amefanya mabadiliko madogo ya baraza la mawaziri kwa kuwafuta kazi mawaziri Dk Charles Tizeba wa Wizara ya Kilimo na Dk Charles Mwijage wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji.

Taarifa kwa umma iliyotolewa na Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu, Gerson Msigwa imeeleza kuwa mabadiliko hayo pia yamejumuisha uteuzi wa manaibu mawaziri wanne akiwemo Mbunge wa Ukonga, Mwita Waitara aliyehamia CCM hivi karibuni.

Katika mabadiliko hayo, Rais Magufuli amemteua Japhet Hasunga kuwa Waziri wa Kilimo akiziba nafasi ya Dk Tizeba huku nafasi ya Dk Mwijage ikichukuliwa na Joseph Kakunda.

Kabla ya uteuzi huu wa leo jioni (Novemba 10, 2018) Hasunga alikuwa Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii wakati Kakunda alikuwa Naibu Waziri wa Ofisi ya Rais-Tamisemi.

“Rais Magufuli amemteua mheshimiwa Constantine Kanyasu kuwa Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii. Mheshimiwa Kanyasu anachukua nafasi ya Mheshimiwa Hasunga ambaye ameteuliwa kuwa Waziri wa Kilimo,” inasomeka sehemu ya taarifa hiyo ya Ikulu.

Dk Mary Mwanjelwa aliyekuwa naibu wa Dk Tizeba kateuliwa kuwa Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora huku Waitara akichukua nafasi ya Kakunda anayeenda kuongoza wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji.

Mbunge wa Karagwe (CCM) Innocent Bashungwa anaenda kuziba nafasi ya Dk Mwanjelwa Wizara ya Kilimo.

“Uteuzi wa viongozi hawa umeanza leo 10 Novemba 2018 na wateule wote wataapishwa Jumatatu 12 Novemba 2018 Saa 3 asubuhi Ikulu jijini Dar es Salaam,” inasomeka taarifa hiyo.

Katika taarifa hiyo, Dk Magufuli pia ameivunja Bodi ya Korosho Tanzania (CBT) na kutengua uteuzi wa Mwenyekiti wa bodi hiyo, Anna Abdallah kuanzia leo ikiwa ni takriban majuma mawili tu tangu atishie kufanya hivyo kutokana na kutoridhishwa na utendaji wa taasisi hiyo.

Mabadiliko hayo madogo ya baraza la mawaziri yanakuja wakati kukiwa na msuguano wa chini kwa chini baina ya Serikali na wafanyabiashara wa korosho kutokana na kudorora kwa ununuzi wa zao hilo ambalo mwaka jana ilichangia kwa kiasi kikubwa cha fedha za kigeni.


Zinazohusiana:   


Kwa mujibu wa Kitabu cha Hali ya Uchumi mwaka 2017, korosho ndiyo zao la biashara lililoongoza kwa kuingiza fedha nyingi za kigeni zikifikia Sh1.2 trilioni ikiwa ni zaidi ya mara nne ya thamani ya mauzo ya nje ya Kahawa.

Kuna kila dalili kuwa mabadiliko hayo ya madogo ya baraza la mawaziri yamechochewa na kusuasua kwa ununuzi wa korosho ambazo mwaka jana wakulima wake walijikuta wakipata faida maradufu kutokana na kuwepo kwa bei nono ya hadi takriban Sh4,000 kwa kilo.  

Mawaziri Dk Charles Tizeba wa Wizara ya Kilimo (kulia) na Dk Charles Mwijage wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji kabla ya kuondolewa katika nyadhifa zao. Picha] Wazo huru.

Kushuka kwa bei ya zao hilo katika minada ya awali mwaka huu kulishababisha uwepo wa vikao vingi baina ya wafanyabiashara na Serikali kikiwemo kilichoongozwa na Rais Magufuli hivi karibuni katika kufikia muafaka wa bei rafiki itakayowaokoa wakulima dhidi ya hasara.

Jana Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa aliwapa siku nne wafanyabiashara wa korosho waliosajiliwa na Serikali kuwasilisha mpango wao wa kiwango cha manunuzi na tarehe walizopanga kununua na iwapo watashindwa kufanya hivyo hataruhusiwa mtu mwingine kununua zao hilo.

Saa 24 baada ya notisi hiyo, Rais Magufuli leo alitembelea kikosi cha Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) cha 95KJ na kukagua magari ambayo yanaweza kutumika kubebea korosho zitakazonunuliwa na Serikali iwapo wanunuzi hao binafsi hawatatii maagizo hayo.

“Nataka kuwahakikishia wakulima wa korosho Serikali ipo na itaendelea kuwapigania, ikifika Jumatatu Saa 10:00 jioni hawa wanunuzi binafsi hawajajitokeza na kueleza watanunua tani ngapi, Serikali itanunua korosho zote na fedha za kununulia fedha tunazo,” amesema Rais Magufuli.

Oktoba 28 mwaka huu Rais Magufuli alitoa agizo kuwa hakuna mtu atakayeruhusiwa kununua korosho chini ya Sh3,000 kwa kilo baada ya kukutana na wafanyabiashara wa zao hilo linalolimwa zaidi mikoa ya Lindi, Mtwara, Ruvuma, Pwani na Tanga.

Hata hivyo, baada ya minada kuanza upya hivi karibuni mwitikio umekuwa hafifu huku sehemu kubwa ya shehena zikikosa wanunuzi.

Leo Rais Magufuli amesema kati ya kampuni 37 zilizoomba kununua korosho, ni 14 tu ndiyo zimejitokeza kununua zao ambalo wakulima wake waligomea bei ya awali ya kati ya Sh1,900 na Sh2,700 kutokana na kutoendana na hata gharama za uzalishaji.

Iwapo Serikali itanunua korosho zote zinazokadiriwa kuwa tani 200,000 mwaka huu, kwa bei ya wastani wa Sh3,000 kwa kilo itatakiwa kutoa kibindoni si chini ya Sh600 bilioni kufanikisha ununuzi huo. Gharama hizo zitakuwa nje ya usafirishaji na kuwezesha mchakato wa ununuzi.

Hasunga na Kakunda sasa watatakiwa kukabiliana na 'mfupa' huo wa bei ya korosho kuhakikisha kuwa wakulima wanaziuza kwa bei itakayokuwa na manufaa.

Related Post