Mfahamu William Lukuvi: Mbunge wa Tanzania kwa zaidi ya miaka 30
- Amegombea na kushinda mara saba mfululizo tangu Uchaguzi Mkuu wa mwaka 1995 katika Jimbo la Isimani lilipo mkoani Iringa.
- Amehudumu katika nyadhifa mbalimbali za uongozi ikiwemo uwaziri.
Dar es Salaam. Katika kurasa za kitabu cha historia za wanasiasa nchini Tanzania huenda jina la William Lukuvi likawekewa nukta yenye wino mzito mara baada ya kutangazwa kwa kifo chake kilichotokana na maradhi ya mshtuko wa moyo.
Rais Samia Suluhu Hassan amethibitisha kifo cha mwanasiasa huyo Machi 25 2026 ikiashiria kufungwa rasmi kwa ukurasa wa maisha yake hapa duniani.
Kwa miongo 7 tangu kuzaliwa kwake Lukuvi ametengeza historia pana isiyofutika kuanzia kwa wanawafamilia hadi kwa Watanzania waliopata fursa ya kufanya nae kazi au kuguswa na maisha yake kwa namna moja au nyingine.
Karibu katika makala inayoelezea maisha yake alipozaliwa, elimu, kazi na siasa mpaka umauti ulipomkuta. Fuatana nami mpaka mwisho wa makala hii.
Undani wa maisha ya Lukuvi
William Vangimembe Lukuvi alizaliwa Agosti 15, 1955 katika kijiji cha Mapogoro, Wilaya ya Iringa Vijijini, wakati huo Tanzania ikiitwa Tanganyika.
Kwa mujibu wa taarifa za Bunge la Tanzania, Lukuvi ni msomi aliyeianza safari yake ya elimu mwaka 1962 katika shule ya Msingi Kitanewa na kuhitimu mwaka 1970.
Mwaka 1974 mpaka 1975 alipata mafunzo ya awali Chuo cha Ualimu Tabora (TTC) ngazi ya cheti.
Mwaka 1982 hadi 1983 alisoma Diploma ya Sayansi ya Siasa katika shule ya Komsomol huko Moscow nchini Urusi.
Safari yake ya elimu iliendelea katika ngazi ya shahada ambayo aliisoma kati ya mwaka 1999 hadi 2001 katika Chuo Kikuu cha Washington, na baadaye akasoma Shahada ya Uzamili ya Sayansi ya Siasa kutoka Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT)
Safari ya ubunge kwa miongo mitatu na uwaziri
Lukuvi, anaingia katika orodha ya wabunge wakongwe zaidi nchini Tanzania akiwa na miaka 30 na miezi kadhaa bungeni iliyotaraiia kuongezeka endapo angemaliza muda wake wa uongozi katika Bunge la 13.
Safari yake bungeni ilianza rasmi 1990 hadi 1995 kisha kuchaguliwa tena katika mabunge yote yaliyofuata hadi Bunge la 13 kabla ya kupatwa na umauti.
Katika miaka ya mwanzo ya uongozi wake, Lukuvi aliteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Wanawake na Watoto, nafasi aliyoitumikia kuanzia mwaka 1994 hadi Novemba 1995.
Baada ya uchaguzi wa mwaka 1995, aliteuliwa tena kuwa Naibu Waziri katika Ofisi ya Waziri Mkuu, akihudumu kuanzia mwaka 1995 hadi 1998.
Jukumu hili lilimpa uzoefu mkubwa katika uratibu wa shughuli za Serikali na usimamizi wa kero za wananchi kupitia ofisi hiyo kuu ya utendaji.
Mwaka 2000 na 2005 alishika wadhifa wa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Siasa na Mahusiano ya Jamii) kisha kuongezewa majumu mengine ya kuongoza mikoa ya Dar es Salaam na Dodoma kati ya mwaka 2005 na Machi 2008.
Vyeo hivyo vinamfanya Lukuvi kuwa miongoni mwa viongozi wachache waliowahi kutumikia vyeo viwili kwa wakati mmoja vikiimwongezea sifa ya kuwa kiongozi mwenye uwezo wa kusimamia watendaji wa Serikali katika ngazi ya mkoa, wilaya hata katika ngazi ya kitaifa.
Baadae mwaka 2008 hadi 2015 Lukuvi aliteuliwa kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Uratibu na Bunge.
Mguu nje mguu ndani Baraza la Mawaziri
Rais wa awamu ya nne Jakaya Kikwete hakumjumuisha Lukuvi kwenye Baraza la Mawaziri katika awamu yake ya kwanza ya uongozi, ambapo katika kipindi hicho ndipo alihudumu kama Mkuu wa mikoa ya Dar es Salaam na Dodoma.
Mwaka 2010 Rais Kikwete alimteua tena Lukuvi kuwa Waziri katika Ofisi ya Waziri Mkuu, anayesimamia masuala ya Sera, Bunge na Uratibu nafasi aliyohudumu mpaka mwaka 2015.
Mara baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, Lukuvi aliendelea kusalia katika Baraza la Mawaziri, Rais wa Awamu ya tano, Hayati John Magufuli alimteua kuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi nafasi aliyohudumu mpaka mwaka 2022.
Lukuvi ni miongoni mwa mawaziri wachache ambao hawakuondolewa katika wizara zao na Hayati Magufuli ambaye alikuwa anasifika kwa ufuatiliaji wa mambo, kusimamia nidhamu na hakusita kuwachukulia hatua watendaji wa Serikali waliobainika kuwa wazembe na kujihusisha na vitendo viovu.
Mara baada ya kifo cha Magufuli na nchi kuongozwa na aliyekuwa Makamu wake Samia Suluhu Hassan, Lukuvi aliwekwa nje ya Baraza la Mawaziri.
Rais Samia alipofanya mabadiliko ya baraza hilo mapema Januari 2022, ambapo alisema atampangia majukumu mengine.
Juni 13, 2023 Rais Samia alimteua Lukuvi kuwa mshauri wake wa masuala ya siasa na uhusiano wa jamii nafasi aliyohudumu kwa mwaka mmoja na miezi miwili.
Agosti 14, 2024, Rais Samia alimrejesha tena Lukuvi kwenye Baraza la Mawaziri akimteua kuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu) nafasi anayohudumu hadi sasa.
Baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2025 Lukuvi ambaye aligombea kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) alipata kura 5,797 akimshinda mpinzani Festo Kiswaga aliyepata kura 1,159.
Lukuvi alikuwa zaidi ya waziri. Alivunja rekodi ya kuwa mbunge aliyedumu kwa muda mrefu tangu mfumo wa vyama vingi urejeshwe Tanzania mwaka 1995.
Kifo chake kinaacha pengo kubwa katika uongozi wa taifa na mioyo ya Watanzania wengi walioguswa na mchango wake.
Latest