Haya hapa mafao ya Dk Nchimbi aking’atuka madarakani

August 26, 2026 7:39 pm · Lucy Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Atalipwa asilimia 80 ya mshahara wa Makamu wa Rais aliye madarakani.
  • Stahiki hizo ni kwa mujibu wa Sheria ya Mafao ya Kustaafu Katika Utumishi wa Kisiasa, (Sura ya 225).

Dar es Salaam. Uamuzi wa Dk Emmanuel Nchimbi wa kung’atuka katika nafasi ya Makamu wa Rais ndani ya siku 10 zijazo umeendelea kuwa gumzo nchini, hususan baada ya kutangaza pia kustaafu siasa na utumishi wa umma.

Dk Nchimbi aliyetangaza uamuzi huo rasmi jana Agosti 25, 2026 anaondoka katika nafasi hiyo baada ya zaidi ya miongo miwili ya utumishi wake katika Chama cha Mapinduzi  (CCM) na uongozi suala lililoacha mijadala mikubwa nchini.

Mbali na kujiuzulu, macho ya Watanzania sasa yanaelekezwa katika mafao anayostahili kiongozi huyo baada ya kuondoka katika nafasi ya Makamu wa Rais.

Kwa mujibu wa Sheria ya Mafao ya Kustaafu Katika Utumishi wa Kisiasa, (Sura ya 225) iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2023, Rais na Makamu wake wanahaki ya kupewa mafao na stahiki nyingine mara baada ya kumaliza utumishi wao.

Kwa upande wa Makamu wa Rais, jedwali namba 1 (A) la sheria hiyo linafafanua kuwa atalipwa posho ya kukamilisha shughuli baada ya kuacha madaraka (winding-up allowance), itakayokokotolewa kwa kuzingatia mshahara wa juu zaidi aliowahi kupokea kwa idadi fulani ya miezi na kiwango cha asilimia kitakachoamuliwa na mamlaka husika.

Kiongozi huyo anayemaliza muda wake pamoja na mwenza au wenza wake atapewa pasipoti ya kidiplomasia na matibabu ndani na nje ya nchi ambayo yatagharamiwa na Serikali.

Atapewa magari mawili ya Serikali, yatakayobadilishwa kila baada ya miaka mitano, nyumba yenye samani, yenye vyumba visivyopungua vitatu, pamoja na nyumba ya mtumishi.

Malipo ya fedha za kutosha kugharamia mishahara, kwa kiwango cha kima cha chini cha mshahara wa watumishi wa Serikali, kwa ajili ya msaidizi mmoja binafsi, mpishi mmoja, mfua nguo mmoja, mtumishi mmoja wa nyumbani, mtunza bustani mmoja na madereva wawili.

Pia gharama za mazishi ya kiongozi huyo na mwenza wake na  huduma muhimu za ulinzi na usalama kwa kiongozi huyo pamoja na makazi yake zitagharamiwa na Serikali.

Kuidhinishiwa 80% ya mshahara

Kifungu cha 13 (1) cha Sheria ya Mafao ya Kustaafu Katika Utumishi wa Kisiasa, (Sura ya 225) kinafafanua kuwa makamu wa Rais  atastahili pensheni ya kila mwezi inayolingana na asilimia 80 ya mshahara wa Makamu wa Rais aliye madarakani.

Yaani kama Makamu wa Rais atakayeingia madarakani analipwa Sh milioni 10, basi Dk Nchimbi  atalipwa Shilingi milioni 8.

Aidha, Makamu wa Rais anastahili kiinua mgongo cha asilimia 50 ya jumla ya mishahara yote aliyolipwa katika kipindi alichokuwa madarakani, pamoja na mafao mengine yaliyoainishwa kwenye jedwali la Sheria hiyo.

Sheria hiyo pia inaeleza kuwa endapo Makamu wa Rais mstaafu ataombwa na Serikali au taasisi ya kimataifa kusafiri nje ya Tanzania, mamlaka husika itagharamia usafiri wa daraja la kwanza, ikiwemo gharama za mwenza wake na msaidizi mmoja binafsi.

Na anaposafiri ndani ya Tanzania kwa ombi la Serikali au taasisi yoyote, Serikali itagharamia safari hiyo, ikiwa ni pamoja na gharama za dereva.

Mwenza/ wenza kulipwa 25% ya mshahara

Kifungu cha 14 (1) kimeainisha kuwa mwenza wa kiongozi anayeachia madaraka anastahili kiinua mgongo cha asilimia 25 ya jumla ya mishahara yote aliyopokea akiwa madarakani.

Aidha, endapo Makamu wa Rais atafariki akiwa madarakani, au baada ya kuacha madaraka kabla ya kupokea mafao yake kifungu cha 15 (1) cha sheria hiyo kinataka wategemezi wake kupewa kiinua mgongo sawa na jumla ya mishahara aliyopokea akiwa madarakani.

Kwa Makamu wa Rais mstaafu aliyefariki, mjane au mgane wake  atastahili pensheni ya kila mwezi ya asilimia 40 ya mshahara wa Makamu wa Rais aliye madarakani, pamoja na mafao mengine yaliyoainishwa katika Sehemu ya II ya Jedwali la Sheria hiyo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Masoko & Zaidi
Loading…
No recent matches
No upcoming matches
/
No matches found for this filter
26 Aug, 2026 · TZS
No forex gainers today
No forex losers today
Forex rates unavailable
26 Aug, 2026 · TZS
No gainers today
No losers today
26 Aug, 2026
No active movers today

Inaendeshwa na Nukta AI

Follow us on TikTok

Nukta Habari

FOLLOW NOW
Subscribe to our channel

Nukta TV

SUBSCRIBE NOW
Elimu ya kodi mwarobaini wa wafanyabiashara kuikwepa TRA, ianzie shuleni

Elimu ya kodi mwarobaini wa wafanyabiashara kuikwepa TRA, ianzie shuleni

Nukta TV

Rais Samia: Serikali chini ya Magufuli haikutaka kuyumbishwa kukamili kwa JNHPP

Rais Samia: Serikali chini ya Magufuli haikutaka kuyumbishwa kukamili kwa JNHPP

Nukta TV

Rais Samia: Umeme wa SGR hautoingiliwa, Dodoma umeme uhakika 24/7

Rais Samia: Umeme wa SGR hautoingiliwa, Dodoma umeme uhakika 24/7

Nukta TV