Usiyoyajua kuhusu virusi vya Corona

March 28, 2020 5:51 am · Joshua
Share
Tweet
Copy Link
  • Mpaka sasa hakuna dawa wala kinga dhidi ya Corona iliyothibitishwa.
  • Hakuna ushahidi wa kitabibu uliothibitishwa kuwa ugonjwa huo unawapata baadhi ya watu tu. Haubagui.
  • Barakoa huvaliwa tu pale mtu anapokuwa ana maambukizi au anamuhudumia mtu mwenye maambukizi.

Mojawapo ya tamaduni zinazonivutia mikoa ya kaskazini mwa Tanzania hasa kabila la Wachaga ni visa na mikasa na hekaya zinazoongelewa katika vijiwe vya pombe ya kienyeji yaani mbege. 

Niweke bayana vile mimi binafsi ninavyovutika na kinywaji hiki cha asili lakini zaidi muda wa kubadilishana mawazo na jamii ya wazee na watu wazima ambao hupatikana katika vijiwe hivi. 

Baada ya tatizo hili kugundulika kuwepo Tanzania nikiwa na wazee hawa wakaniambia “daktarin hebu tupatie mbivu na  mbichi za ugonjwa huu maana tunasikia kila aina za hekaya na hadithi za alfu lela ulela kuhusu hili.”

Nami bila hiana nikavuta fundo moja la mwisho la mbege nikaanza kuwapa mbivu na mbichi kuhusu ugonjwa wa homa ya mapafu unaoletwa na virusi vya Corona (COVID-19).

Hauna ubaguzi kabisa iwe ni kijana ama mzee. Hakuna ushahidi wa kitabibu kutenga baadhi ya kundi na lingine. Japokuwa sasa, wazee na watu ambao tayari wana magonjwa mengine sugu kama asthma, kisukari ama magonjwa ya moyo na figo hawa huwa na hatari zaidi ya kuumwa sana watakapopatwa na Corona

Nikasikia wengine wakisema mazingira ya joto au baridi huathiri kirusi huyu. Hapana, virusi vya Corona huambukiza eneo lolote liwe na joto au baridi. Na hivyo mazingira hayaathiri hilo.


Zinazohusiana


Hapajawa na ushahidi kuwa wadudu kama mbu huweza kuleta maambukizi ya Corona. Pia Wanyama tunaoishi nao kama mbwa, paka hawawezi kupelekea kupata maambukzii ya Corona kutoka kwa mtu mmoja kwenda kwa mwingine.

Mwingine ataniuliza vile vipima joto navyo vinapima Corona au la? Kimsingi kipima joto hakipimi Corona. Bali hupima joto ambalo silo la kawaida baada ya kuwa na homa kali ikiwa ni moja ya dalili za hatari za kuwa na maambukizi ya ugonjwa huo.

Kuna wengine wanashauri kutumia vitunguu swaumu. Ni kweli vitunguu swaumu husaidia sana kiafya. Lakini hapana uhusiano wa kujikinga na virusi vya Corona kwa kula vitunguu swaumu. Tuendelee kuvitumia kama viungo na kama sehemu ya tiba lishe lakini sio kwa minajiri ya kujikinga na Corona.

Mpaka sasa hakuna dawa wala kinga dhidi ya Corona iliyothibitishwa. Hivyo dawa za antibaiotiki hazitibu Corona. Wala chanjo za magonjwa mengine hazikukingi dhidi ya Corona.

Mzee wangu mmoja akataka kunishika mkono, nikamwambia hapana, wakati huu ni wakati wa kukaa kwa kutulia  mzee. Kujiepusha na mizunguko isiyo ya lazima. Lakini pia ni vyema kunawa mara kwa mara kwa maji safi ya kutiririka na sabuni. Pia usishikane mikono wala kugusa vitu ovyo.

Nikaona mwingine ananunua barakoa, nikamuuliza ni ya nini na unajua matumizi yake sahihi? Akasema hapana ila ameona watu wananunua.

 Ikabidi nimueleze kuwa barakoa huvaliwa tu pale mtu anapokuwa ana maambukizi au anamuhudumia mtu mwenye maambukizi au anahisi ana dalili hatarishi. Na pia kuna utaratibu wa namna ya kuivaa. Ukikosea unajipa hatari zaidi ya kupata maambukizi kupitia hiyo hiyo barakoa.

Tukutane wiki ijayo.

Dk Joshua Lameck Sultan ambaye kitaaluma ni daktari wa mafunzo ya mazoezi tiba ni Mshauri katika taasisi ya Nakua na Taifa Langu (NTL) na Mkurugenzi wa Indigo Afya. Hufanya semina mbalimbali kuhusu masuala ya afya akijikita katika magonjwa yasiyoambukiza (NCD) pamoja na yale yanayoendana na mtindo maisha. Anapatikana kwa namba: +255 789 311 481, Baruapepe: joshualameck9@gmail.com.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW