Usidanganyike: Kinywaji hiki hakiambukizi Uviko-19
- Wazushi wanadai soda aina ya Twist inaambukiza Corona.
- Kampuni Sayona inayotengeneza soda hiyo yasema taarifa hizo si za kweli na zinalenga kupotosha.
- Hakuna uthibitisho wa kisayansi kuwa soda zinasambaza Uviko-19.
Dar Es Saalam. Wapenzi wa bidhaa kutoka Sayona aina ya Twist huenda wamepatwa na hofu kubwa baada kuona taarifa inasambaa mtandaoni kuwa zina sumu ya Corona na zimeingizwa kisiri nchini Tanzania huku zikisababisha vifo vya watu 4,000 huko China.
Hata hivyo, wanatakiwa kuondokana na hofu hiyo kwa sababu kinywaji hicho hakisababishi Uviko-19 na madai yaliyotolewa hayana ukweli wowote.
Katika mitandao ya kijamii ikiwemo Whatsapp, kuna ujumbe umekua ukisambaa ukisomeka “TAARIFA KWA SAMIA SULUHU HASAN :- kuna soda zinajulikana kama twist chini ya kizibo zimeandikwa 666 ambazo zimetoka CHINA inasadikika kuwa zina sumu ya CORONA na zimeingizwa kisiri nchini Tanzania na zimesababisha vifo vya watu 4000 huko CHINA. Hata ukipewa bure usinywe chonde chonde naomba utoe taarifa hii kwa watu wote wenye namba yako ili kuokoa maisha ya wengine. Foward kama unawapenda watanzania wenzako USIPUUZIE SIO UTANI”

Ni kweli soda ya Twist inaweza kuambukiza Corona?
Kwa mujibu wa Shirika la Afya duniani (WHO) ugonjwa wa Uviko-19 unaambukizwa kwa njia maji maji yanayotoka kwa mgonjwa kwa kukohoa, kupiga chafya au kuongea.
“Virusi vinaweza kusambazwa kwa maji maji kupitia mdomoni au puani mwathirika anapokohoa, kupiga chafya au kuhema.” inaeleza WHO katika moja ya andiko lake.
Hivyo, madai kuwa kinywaji hicho Twist kuwa kinaweza kusababisha maambukizi ya Uviko-19 hayana ukweli kwa sababu virusi hivyo havijathibitishwa kuwa vinakaa kwenye soda hiyo.
Vile vile timu ya Nukta Fakti imewasiliana na kampuni ya Sayona iliyopo mkoani Dar es Salaam inayozalisha bidhaa ya soda ya Twist, ambapo imesema taarifa hiyo haina ukweli wowote.
“Kampuni kubwa kama hii haiwezi kufanya kitu kama hicho. Uzushi unasambaa sana huenda hata kwa makampuni mengine yanayozalisha vinywaji kama sisi,” amesema mmoja wa watoa huduma kwa mteja wa Sayona aliyekuwa akiongea na Nukta Habari.
Pia sehemu ya ujumbe huo unadai chini ya kizibo cha soda hizo kuna alama ya 666 ambayo kidini inajulikana kama alama ya mpinga Kristo. Hata hivyo, vizibo vya kinywaji hicho hazina alama kama hiyo.
Kama umekutana na taarifa hiyo, usiwe mwepesi wa kuisambaza kwa watu wengine kabla ya kujiridhisha kama ni kweli ili kupunguza madhara ya habari za uzushi kwenye jamii.
Latest
