Jiografia, historia kupewa kipaumbele vyuo vya Tanzania
- Masomo hayo yataanza kufundishwa Chuo cha Mtakatifu Agustino (SAUT).
- Itawasaidia kuijua historia ya Tanzania kwa undani.
Mwanza. Baada ya Rais John Magufuli kuagiza vyuo kuanza kufundisha historia na Jiografia kuhusu Tanzania, hatimaye masomo hayo yataanza kufundishwa katika Chuo cha Mtakatifu Agustino (SAUT) katika mhula huu wa masomo ili kuwawezesha wanafunzi kuweza kujua mambo mengi ikiwemo historia ya nchi yao.
Kwa mujibu wa Mkuu wa Chuo cha SAUT, Profesa Costa Ricky Mahalu amesema historia inaeleza kuwa licha ya vijana wengi kuhitimu vitivo mbalimbali vya elimu ya juu lakini wengi hawana uelewa wa kutosha kuhusua historia yao na nchi yao.
Kutokana na changamoto hiyo, Professa Mahalu amesema wametenga kitengo maalum chuoni hapo kitakachoshughulika na suala hilo huku vijana wakipewa kibarua cha kuandaa makala inayohusiana na masomo hayo.
“Kiujumla somo la historia na jiografia halijapewa umuhimu mkubwa na vijana wengi hawajui nchi na bara la Afrika lilipotoka na lilipo na hata mipaka ya nchi yao,” amesema Profesa Mahalu
Profesa Mahalu amesema wazo hilo la kufundisha masomo hayo vyuoni ni kutokana na wito wa Rais Magufuli kuwa wanafunzi waanze kufundishwa ili kuwaongezea vijana uelewa wa kutosha kuhusiana na nchi yao pamoja na rasilimali zake.
Zinazohusiana:
- Safari bado ndefu kufikia 50 kwa 50 elimu ya juu Tanzania
- TCU wafungua dirisha dogo la usajili kwa wanafunzi wa vyuo vikuu
- TCU yaacha maumivu vyuo vikuu, ikivifuta vituo viwali.
Amesema maono ya Rais Magufuli yalilenga mbali na dhana yake ililenga kuona nchi yake iliyopata uhuru miaka 56 iliyopita inaendelezwa katika masuala ya kisiasa na kiuchumi.
“Kwa vijana wengi hawajui historia ya Tanzania na hawajui kwanini wazee na wahenga walianzisha vyama vya siasa Afrika na Tanzania na kwamba kutokujua hayo yote ni vigumu kujua kwanini Tanzania ilitawaliwa na ikaomba uhuru,” amesema.
Msukumo wa kufundisha somo hilo utasaidia kutoa elimu kwa wanavyuo ili kuwa na uelewa wa namna watakavyoisaidia nchi katika masuala hayo.
“Tunapenda kuona vijana wanatumia maarifa wanayoyapata vyuoni katika kujiajiri, wawe wabunifu na si kutegemea ajira za Serikali na asasi za kiraia pekee,” amesema.
Latest