Safari bado ndefu kufikia 50 kwa 50 elimu ya juu Tanzania

Zahara Tunda 0232Hrs   Aprili 23, 2018 Habari
  • Idadi ya wanawake wanaodahiliwa elimu ya juu bado ni ndogo ukilinganisha na wanaume.
  • Wadau watupia lawama wazazi, walezi na jamii kwa kushindwa kuweka mazingira rafiki ya watoto wa kike kupata elimu.
  • Serikali yaeleza kuwa inaendelea kutekeleza mikakati mbalimbali kuhakikisha watoto wakike wanapata elimu bora hadi vyuo vikuu.

Dar es Salaam. Zaidi ya miaka mitano mfululizo sasa, kasi ya udahili wa wanafunzi wakike vyuoni bado ni ndogo licha ya uwepo wa kampeni lukuki za kuhamasisha usawa wa kijinsia katika upatikanaji wa elimu ulimwenguni.

Uchambuzi wa takwimu za udahili wa elimu ya juu nchini wa miaka miaka mitano uliofanywa na Nukta umebaini kuwa kati ya mwaka 2011 hadi 2016 udahili wa wanafunzi wa kike vyuo vikuu umedumu kwa wastani wa asilimia 35.4, sawa na theluthi tu ya wanafunzi wote wanaodahiliwa.

Hii ikiwa na maana kuwa kwa kila wanafunzi 10 waliodahiliwa vyuo vikuu katika kipindi hicho, ni watatu tu walikuwa wa kike.

Vyuo vya Serikali, vinavyoongoza kwa kudahili wanafunzi wengi nchini, katika kipindi hicho vilikuwa na wanafunzi wakike watatu kwa kila 10 waliokuwa wamedahiliwa ikilinganishwa na wastani wa wanafunzi wakike wanne kwa kila 10 katika vyuo vikuu visivyokuwa vya umma.

Uwepo wa kasi ndogo ya ongezeko la wanafunzi wanawake vyuoni unaelezwa na wadau kuwa ni kiashiria kuwa huenda ikachukua muda mrefu kufikia Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs) ya kuwa na elimu bora yenye usawa wa 50/50 ifikapo 2030.

Hali hili inatokea licha ya takwimu za Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) kuonyesha kuwa idadi ya taasisi za juu zimekuwa zikiongezeka mwaka hadi mwaka. 

Hadi kufikia mwaka 2016, takwimu hizo za TCU zilizochapishwa kwenye kitabu cha Takwimu za Mwaka 2016 (Tanzania in Figures 2016) ambazo hutolewa na Ofisi ya Takwimu ya Taifa (NBS) zinaonyesha kulikuwa na taasisi za elimu ya juu 50. Kati ya hivyo, Vyuo vikuu na vyuo vya umma 14 na vyuo binafsi ni 36.

Soma hii pia: Shule 24 vigogo 'zilizoteka' 10 bora kidato cha nne

Vyuo vya umma kwa mwaka wa masomo 2015/2016 vilidahili wanafunzi 116,729 huku wanafunzi wakike wakiwa 38,423 tu (asilimia 32.9) sawa na wastani wanafunzi wakike watatu kwa kila 10. Udahili huo unashabihiana na ule wa mwaka wa masomo wa 2010/11 ambapo vyuo hivyo vilidahili wanafunzi 92,977 huku wakike wakiwa 30,003 sawa na asilimia 32.3 au watatu kwa kila 10 waliodawahili mwaka huo.

Licha ya vyuo binafsi kuwa vingi ikilinganishwa na vya umma bado udahili wao ni mdogo ambapo mwaka wa masomo wa 2015/2016 vilidahili wanafunzi 73,128 huku wanawake wakiwa 28,786 tu ikiwa ni sawa na wanafunzi wakike wanne kwa kila wanafunzi 10. Katika mwaka wa masomo wa 2010/11, vyuo vikuu binafsi vilidahili wanafunzi 42,390 huku wakike wakiwa 17,186 (asilimia 40.5) sawa na wanne kwa 10. 

Tafiti mbalimbali na maoni ya wadau yanaonyesha kuwa moja ya sababu kubwa inayowakabili watoto wengi wa kike au wanawake wengi kutokufikia elimu ya juu ni changamoto wanazokabiliana nazo wakati wakiwa katika ngazi za chini za elimu ikiwemo kukosekana kwa wanawake wengi wasomi wenye ushawishi kwa wanafunzi wa kike.

Changamoto nyingine zinazowakabili watoto wakike ni pamoja na umbali wa kutembea kwenda shuleni na kurudi, ujauzito wakiwa shuleni, ndoa za utotoni, ajira za watoto, utoro, umaskini kukosekaa kwa mahitaji maalumu shuleni kwa baadhi ya wanafunzi na baadhi ya mila na desturi zinazokinzana na utoaji wa elimu kwa watoto wa kike.

Serikali inasema kuwa inaendelea kutekeleza mikakati mbalimbali ya kuongeza udahili wa wanawake vyuo vikuu ikiwapo hatua iliyochukuliwa miaka iliyopita ya kushusha alama na vigezo kwa wanawake wanaojiunga vyuo vikuu ikilinganishwa na wanaume ili wengi wapate fursa ya elimu ya juu. 

“Serikali imejitahidi hata kushusha alama za kuingia vyuoni kwa wanawake, lakini bahati mbaya wasichana ni wachache kwa sababu wengi huishia kidato cha nne, kwa ufaulu hafifu,” anasema Dkt Ave Maria Semakafu, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia.


Bado inahitajika nguvu ya ziada kuhakikisha watoto wa kike wanatengenezewa mazingira ya kufanya vizuri katika masomo waweze kuendelea na elimu ya juu ili kufikia  50 kwa 50.  Picha|The Citizen


Mtazamo hasi wa 50 kwa 50 katika jamii

Hali hii ya uwepo wa wanafunzi wakike wachache vyuoni, inachangiwa pia na mtazamo hasi wa jamii hasa katika suala zima la usawa wa kufikia 50/50.

Mhadhiri msaidizi wa Habari na Taaluma za Maendeleo za Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) Dotto Kuhenga ameiambia Nukta kuwa usawa wa elimu utafikiwa iwapo kutakuwa na usawa katika nyanja zote za maisha yaani usawa katika utawala, uchumi wa viwanda, utamaduni na kisiasa.

“Hatuwezi kuwaambia vyuo vikuu kwanini hamdahili wanafunzi wengi wa kike wakati inawezekana bado hatujabadilika katika masuala kama ya kimila, utamaduni na kielimu,” anasema.

Hata hivyo, bado changamoto kubwa ipo kwa wazazi ambao ndio msingi wa kujenga watoto wakike katika mfumo mzuri utakaoleta matokeo chanya katika nyanja ya elimu.

“Jitihada zianzie kwenye ngazi ya familia, kwa wazazi na walezi kuelimishwa namna ya kuwalea watoto wakike katika misingi ya kuwa wasomi tangu wakiwa watoto wadogo,” anaeleza Yusuphu Lulungu mkazi wa Makumbusho jijini Dar es Salaam.

Mbali na sababu za kiutamaduni na maelezi baadhi ya wadau wanaeleza kuwa Tanzania iweze kufikia 50/50 katika elimu ya juu inatakiwa kuondoa vikwazo vya watoto wakike katika ngazi za chini.

Scholastica Pembe wa Shirika la kiraia la New Hope New Winner Foundation anasema moja ya njia ya kuondoa vikwazo hivyo ni kuanza kuwapa watoto wakike vitaulo vya kijistiri (pads) bure wakiwa mashuleni.

Shamira Mshangama, Mkurugenzi wa Shirika lisilo la serikali la Mwanamke na Uongozi, anasema kuwe na utaratibu wa mashirika yasiyo ya serikali wanayofanya kazi za wanawake kukutana na watoto wakike na kuzungumza nao.

“Lazima tuwe na utaratibu wa kuzungumza nao na kuwaonyesha uhalisia nje ya shule, ili kuwapa motisha ya wanafunzi wakike kusoma kwa bidii ili wawe chachu ya mabadiliko,” anasema Shamira.


Wanafunzi wanasemaje?

Wanafunzi wakike waliopo vyuo vikuu wanaouona mwanya uliopo kati yao na wenzao wakiume kutokana na uchache wao madarasani hususan katika masomo ya Sayansi.

“Tupo wanafunzi 88 darasani kwetu tunaochukua kozi ya uhandisi wa mfumo wa taarifa na mtandao (Information System and network engineering), lakini wasichana tupo 30 tuu,” amesema Eugenia Kinabo mmoja wa wanafunzi kutoka chuo kikuu cha St Joseph.

Watoto wa kike wajengewe uwezo wa kufanya vizuri katika masomo ya sayansi ili kuongeza idadi ya wanataaluma wengi wanawake na kuwa mfano wa kuigwa kwa watoto wa kike wanaochipukia. Picha | Mtandao.

John Kodi ambaye ni mwanafunzi wa Chuo kikuu cha Dar es Salaam, akichukuwa kozi ya uhandisi wa ujenzi (civil engineering) anasema licha ya chuo hicho kuchukua wanafunzi wengi wa kozi hiyo lakini wanafunzi wakike ni wachache.

 “Darasani kwetu wanaume wapo 120, huku wanawake wakiwa 27 tuu,” anasema Kodi.


Nini kinaendelea serikalini? 

Sera ya elimu ya Serikali imeweka wazi kuwa dira ya elimu na mafunzo nchini ina lengo la kila mtanzania aliyeelimika na mwenye maarifa, stadi, umahiri uwezo na mitazamo chanya ili kuweza kuchangia katika kuleta maendeleo ya Taifa.

Na dhima kubwa ni kuinua ubora wa elimu na mafunzo na kuweka mifumo na taratibu zitakazowezesha kupata idadi kubwa ya watanzania walioelimika na wanaopenda kujielimisha zaidi ili waweze kuchangia katika kufikia malengo ya maendeleo ya Taifa.

Hata hivyo, yote hayo hayawezi kufikiwa iwapo hakutakuwa na mabadiliko ya kifikra na mtazamo kwa jamii, juu ya kumkomboa mtoto wakike kielimu.

Dk Semakafu ameiambia Nukta kuwa Serikali inaendelea kuweka mazingira rafiki kwa watoto wakike kupata fursa sawa kielimu nchini kama ilivyo kwa wenzao wa kiume.

“Turekebishe majumbani, tuendelee na kampeni  kila mtu na nafasi yake na wadau kwa ujumla ili tuweze kubadilisha mwonekano wetu na mtazamo wetu kwa watoto wakike,” anasema Dkt Semakafu, ambaye kabla ya kuteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu wizara ya elimu alikuwa ni mwanaharakati wa masuala ya jinsia na demokrasia. 

Related Post