TCU wafungua dirisha dogo la usajili kwa wanafunzi wa vyuo vikuu

TULINAGWE MALOPA 0832Hrs   Septemba 11, 2018 Habari
  • TCU watoa siku tano kwa wanafunzi kuomba vyuo kwa awamu ya pili.
  • Yatoa sifa za makundi ya wanafunzi watakaotakiwa kuomba katika dirisha hilo litakalomalizika Septemba 14, 2018.

Dar es Salaam. Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) imefungua dirisha la pili maombi kwa siku tano  kuanzia jana (Septemba 10, 2018) baada ya idadi ya waombaji  wengi kukosa nafasi za kujiunga na vyuo vikuu kwa sababu mbalimbali katika mwaka wa masomo ujao.

Hatua hiyo ya TCU inakuja baada ya kukamilisha awamu ya kwanza kwa kuhakiki sifa za waombaji waliodahiliwa na taasisi za elimu ya juu katika mwaka ujao wa masomo wa 2018/19.

Taarifa  iliyotolewa na Katibu Mtendaji wa Tume hiyo imesema diirisha hilo ambalo litakalomalizika Septemba 14 litahusiha  makundi ya waombaji wote waliokosa nafasi kwenye awamu ya kwanza na waombaji wa kidato cha sita na stashahada walioshindwa kuomba katika awamu ya kwanza.

''Waombaji waliomaliza mitihani ya “Cambridge” mwaka 2018 na matokeo yao yameshatoka; na  waombaji waliokuwa wamedahiliwa miaka ya nyuma na kuacha au kukatisha masomo nao wataruhisiwa kudahiliwa katika dirisha hili," inasomekan sehemu ya taarifa hiyo.

Tume hiyo imesisitiza kuwa utaratibu wa kutuma maombi ni ule ule wa kutuma maombi moja kwa moja vyuoni kama ilivyokua katika awamu ya kwanza ya udahili.

Waombaji hao wapya watakaopatikana katika dirisha hili la pili wataambatana na wenzao ambao tayari baadhi ya vyuo  vikuu vya umma na binafsi vikiwa vimedahili katika awamu ya kwanza kama Chuo Kikuu Ardhi  (ARU) ambacho kimeshadahili wanafunzi 367. 

Chuo Kikuu Cha Dar-es-Salaam (UDSM) ambacho ni kikongwe kuliko vyote nchini kimeshadahili wanafunzi  2,000 wakati Chuo Kikuu Cha Dodoma (UDOM) kikiwa kimeshatoa majina ya wanafunzi 3450. Chuo Kikuu Cha Mzumbe (MU) chenye makao yake makuu mkoani Morogoro tayari kimeshadahili wanafunzi 2,831.

Related Post