Mfahamu kiundani  Profesa Costa Ricky Mahalu

March 11, 2026 5:30 pm · Fatuma Hussein
Share
Tweet
Copy Link
  •  Aliwahi kuwa Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika mashirika ya kimataifa yenye makao yake Roma.
  • Profesa Mahalu pia alikuwa wakili wa Mahakama Kuu ya Tanzania.
  • Ameaga dunia akiwa na umri wa miaka 77, miezi 8 na siku 1.

Dar es Salaam. Tanzania imepoteza mmoja wa wasomi na wanadiplomasia wake mahiri, Profesa Costa Ricky Mahalu,aliyelitumikia vyema Taifa na kuacha alama katika sekta mbalimbali nchini ikiwemo ya elimu ya juu na sheria.

Ukurasa wa maisha yake ulifungwa rasmi machi 9, 2026 wakati akipatiwa matibabu katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) jijini Dar es Salaam baada ya kuishi kwa takribani miongo saba, miaka saba na miezi nane.

Mwenyekiti wa Baraza la Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustino cha Tanzania (SAUT), Askofu Flavian Matindi Kassala, alithibitisha kutokea kwa kifo hicho akitoa pole kwa familia ya marehemu, menejimenti ya chuo, jumuiya nzima ya SAUT pamoja na ndugu, jamaa na marafiki walioguswa na msiba huo.

Kwa vijana waliozaliwa kuanzia mwaka 2,000 huenda wasimfahamu kiundani profesa huyo na nguli wa masuala ya kidiplomasia na mchango wake nchini Tanzania, ndio maana Nukta Habari  tumekuletea makala hii tukiamini kuwa ndani ya dakika chache utaelewa ni kwanini kifo cha Profesa Mahalu ni pigo kwa Taifa.

Je unafahamu Profesa Costa Ricky Mahalu?

Profesa Costa Ricky Mahalu alizaliwa Julai 9, 1948 katika Kijiji cha Katunguru, Wilaya ya Sengerema, mkoani Geita wakati huo ikiwa sehemu ya Mkoa Mwanza. 

Maisha ya awali ya Mahalu yaligubikwa na changamoto za kifedha. Baba yake, ambaye alikuwa dereva wa lori, hakuweza kumudu kulipa ada za shule, jambo lililomlazimu Mahalu kusitisha masomo yake kwa muda.

Kutokana na hali hiyo, mama yake marehemu Naziwa, alimshauri kutafuta kazi ili aweze kujilipia ada ya shule.

Katika harakati hizo alikutana na mfanyabiashara aliyekuwa maduka Sengerema aitwaye Jashbai Patel, ambaye aliamua kumsaidia kwa kulipa ada zake za shule. 

Akiwa kijana mdogo pia alipenda michezo ya kuigiza na mpira wa kikapu, na marafiki zake waliamini angeweza kuwa muigizaji mkubwa siku za usoni.

Baada ya kumaliza elimu ya msingi, alijiunga na Shule ya Sekondari Kibaha kwa masomo ya kidato cha kwanza hadi cha nne, kabla ya kuendelea na elimu ya juu ya sekondari katika Shule ya Sekondari Mkwawa.

Mwaka 1971 alijiunga na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) katika kambi ya Makutupora, Dodoma kwa mafunzo ya msingi ya kijeshi. 

Baadaye alijiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) alikohitimu shahada ya kwanza ya Sheria mwaka 1974.

Prof Mahalu enzi za uhai wake aliwahi kueleza kuwa mtu aliyemshawishi kusomea sheria ni Waziri Mkuu wa Zamani, Jaji Joseph Warioba.

Mwaka 1975 aliajiriwa na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kama mhadhiri msaidizi katika Kitivo cha Sheria. 

Kuanzia mwaka 1976 hadi 1978 aliendelea na masomo ya shahada ya uzamili ya sheria huku akiendelea kufundisha chuoni hapo.

Mwaka 1979 alikwenda Hamburg, Ujerumani Magharibi, ambako alipata shahada ya uzamivu (PhD) katika masuala ya sheria mwaka 1983. 

Baada ya kurejea nchini, alipandishwa cheo na kuwa mhadhiri mwandamizi katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Mwaka 1990 alikwenda tena Ujerumani kufanya kazi ya ualimu, lakini alirejea nchini baada ya mwaka mmoja na kuteuliwa kuwa Profesa wa Sheria katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. 

Mageuzi ya elimu ya juu Tanzania

Profesa Mahalu pia alikuwa na mchango mkubwa katika mageuzi ya sera ya elimu ya juu.

Kati ya mwaka 1992 hadi 1996, Mahalu alihudumu kama Mkurugenzi wa Elimu ya Juu katika Wizara ya Sayansi, Teknolojia na Elimu ya Juu, nafasi ambayo aliacha mchango mkubwa katika maendeleo ya sekta ya elimu nchini.

Akiwa katika nafasi hiyo, aliwahi kumshauri aliyekuwa Waziri wa Sayansi, Teknolojia na Elimu ya Juu wakati huo Benjamin Mkapa, kuruhusu kuanzishwa kwa vyuo vikuu binafsi nchini.

Katika kipindi hicho, alikuwa miongoni mwa waanzilishi wa wazo la utoaji wa mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu, hatua ambayo baadaye ilisababisha kuanzishwa kwa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB). 

Mwaka 1996 alihamishiwa Wizara ya Mambo ya Nje, ambapo baadaye alipelekwa Ujerumani kama Naibu Balozi. 

Mwaka 1999 aliteuliwa kuwa Balozi wa Tanzania nchini Italia na kuhudumu kuanzia mwaka 2000 hadi 2006.

Licha ya mchango wake uliotukuka katika Taifa Mwaka 2007, Profesa Mahalu alikabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi pamoja na aliyekuwa Ofisa Utawala wa ubalozi huo, Grace Martin.

Katika kesi hiyo walidaiwa kula njama, kutumia nyaraka za manunuzi ya jengo la ubalozi wa Tanzania nchini Italia ili kumdanganya mwajiri wao.

Walishitakiwa pia kwa wizi wa Euro 2,065,827(zaidi ya Sh2.5 bilioni kwa viwango vya kubadili fedha za kigeni kwa wakati huo) na kuisababishia Serikali hasara.

Pamoja na kuwa kesi hiyo iliisha miaka mingi iliyopita, kumbukumbu yake imebakia kwenye vichwa vya wengi na kuacha rekodi ya pekee katika historia ya mahakama Tanzania.

Upekee wa kesi hiyo ulitokana na aina ya mashahidi waliotajwa husussan upande wa utetezi akiwemo rafiki yake wa karibu Hayati Benjamin Mkapa aliyekuwa Rais wa awamu ya tatu nchini Tanzania

Mbali ya Rais Mkapa, mashahidi wengine wa utetezi waliosimamishwa ni pamoja na Rais aliyekuwa madarakani wakati huo, Jakaya Kikwete na hayati John Magufuli ambaye wakati huo alikuwa Waziri wa Ujenzi.

Kinachoipa kesi hiyo upekee mkubwa ni pale Rais Mkapa aliposimama kizimbani na kutoa ushahidi uliokinzana na ule wa Jamhuri, akiamini Profesa Mahalu na wenzake hawakuwa na hatia.

Tukio la Rais Mkapa kutoa ushahidi mahakamani liliweka rekodi ya kihistoria, kwani ilikuwa mara ya kwanza kwa  Rais wa Tanzania kusimama kizimbani kutoa ushahidi.

Mpaka hivi leo rekodi  ya kesi yake haijawahi kuvunjwa, ikimaanisha hakuna Rais aliyewahi kusimama upande wa utetezi wa mshtakiwa mahakamani.

Profesa Mahalu pia aliwahi kuhudumu kama Balozi wa Tanzania nchini Athens, Ankara, Ljubljana, Zagreb, Serbia na Macedonia.

Katika kipindi hicho pia aliwahi kuwa Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika mashirika ya kimataifa yenye makao yake Roma, likiwemo Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO), Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) na Mfuko wa Kimataifa wa Maendeleo ya Kilimo (IFAD).

Profesa Mahalu pia aliwahi kufundisha sheria katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Chuo Kikuu cha Hamburg nchini Ujerumani na Taasisi ya Hague ya Mafunzo ya Jamii. 

Aidha, alifanya kazi katika kampuni mbalimbali za sheria barani Ulaya akijikita zaidi katika sheria ya kimataifa ya bahari.

Mbali na kuwa Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agustino cha Tanzania, Profesa Mahalu pia alikuwa wakili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mwenyekiti wa Baraza la Chuo Kikuu cha Ardhi na mshauri wa kisheria kwa taasisi mbalimbali za ndani na kimataifa zinazofanya kazi nchini.

Kwa mujibu wa msemaji wa familia Shariff Maajar mwili wa marehemu utapelekwa katika viwanja vya Karimjee Jumamosi ili kuruhusu wananchi, na viongozi mbalimbali kutoa heshima zao za mwisho kabla ya  kuzikwa katika Makaburi ya Kinondoni jijini Dar es Salaam.

“Asubuhi ya Jumamosi majira ya saa 3:00, mwili wake utapelekwa katika Viwanja vya Karimjee ili kutoa fursa kwa wananchi kutoa heshima zao za mwisho, ambapo pia kutakuwa na huduma ya chai na chakula cha mchana,” amesema Maajar.

Kifo chake kimeacha pengo kubwa katika sekta ya elimu ya juu, sheria na diplomasia nchini Tanzania.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Follow Us on TikTok

Subscribe to Our YouTube Channel

Subscribe

Loading videos...

Loading videos...

Loading videos...

Enable Notifications OK No thanks