Gharama za usafirishaji zachangia bei ya petroli, dizeli kupanda Tanzania

March 3, 2021 12:44 pm · Daniel Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Bei hizo mpya kikomo za ni mafuta ya petroli, dizeli na mafuta ya taa za mwezi Machi 2021. zilizotangazwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura). 
  • Bei zilizopanda ni mafuta yanayopitia bandari za Dar es Salaam na Tanga.
  • Bei za mafuta hazijabadilika zitaendelea kutumika za toleo la mwezi uliopita. 

Dar es Salaam. Watumiaji wa mafuta Tanzania watalazimika kutoboa mifuko yao zaidi baada ya kutangazwa kwa bei mpya za rejareja za nishati hiyo ambazo mwezi huu zimepaa ikilinganishwa na Februari kutokana na kubadilika kwa bei za mafuta katika soko la dunia na gharama za usafirishaji. 

Bei hizo mpya kikomo mafuta ya petroli, dizeli na mafuta ya taa za mwezi Machi zilizotangazwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura) zinaanza kutumika leo machi 3, 2021. 

Bei za rejareja za petroli iliyoingizwa kupitia Bandari ya Dar es Salaam imeongezeka kwa asilimia 4.99.

Kutokana na ongezeko la bei hiyo, watumiaji wa vyombo vya moto watalazimika kutoboa mifuko yao, ambapo watalipia Sh94 kwa lita zaidi ya bei ambayo walikuwa wananunulia petroli mwezi Februari. 

Pia bei za rejareja za dizeli imeongeza kwa Sh82 na mafuta ya taa kwa Sh94 kwa lita. 

“Mabadiliko haya ya bei yanachangiwa na kubadilika kwa bei za mafuta katika soko la dunia na gharama za usafirishaji,” amesema Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Ewura, Gerald Maganga katika taarifa iliyotolewa na Ewura.

Vilevile, ikilinganishwa na toleo la mwezi uliopita, bei za jumla za petroli  zimeongezeka kwa Sh93.7 kwa lita huku dizeli (Sh81.4) na mafuta ya taa kwa Sh94.2 sawa na asilimia 5.7.


Soma zaidi: 


Maumivu hayo pia yatawagusa watumiaji wa nishati hiyo wa mikoa ya Tanga, Arusha, Kilimanjaro na Manyara, inayotumia mafuta yanayopitia Bandari ya Tanga ambako nako bei imepanda. 

Kwa mwezi Machi 2021, bei ya rejareja ya petroli imeongezeka kwa Sh163 na dizeli imeongezeka kwa Sh85 kwa lita (sawa na asilimia 4.64).

“Hata hivyo, bei za mafuta ya taa hazina mabadiliko na zitaendelea kuwa zile zilizotangazwa katika toleo la tarehe 3 Februari 2021. Hii ni kwa sababu, kwa Februari 2021 hakuna shehena ya mafuta ya taa iliyopokelewa kupitia bandari ya Tanga,” amesema Maganga. 

Aidha, bei za rejareja na jumla kwa bidhaa za mafuta ya petroli na dizeli kwa mikoa ya kusini (Mtwara, Lindi, and Ruvuma) zitaendelea kuwa zile zilizotangazwa katika toleo la tarehe 3 Februari 2021 kwa sababu mwezi uliopita hakuna shehena ya mafuta iliyopokelewa kupitia bandari ya Mtwara. 

Kwa mujibu wa Sheria ya Mafuta ya mwaka 2015, kifungu namba 166, bei za bidhaa za mafuta ya petroli zitaendelea kupangwa na soko na Ewura  itaendelea kuhamasisha ushindani kwa kutoa taarifa za bei kikomo za bidhaa za mafuta. 

Ewura katika taarifa hiyo imesema kampuni za mafuta ziko huru kuuza bidhaa za mafuta ya petroli kwa bei ya ushindani mradi tu bei hizo zisivuke bei kikomo.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW