Mambo ya kupewa kipaumbele na vijana mwaka 2022

December 27, 2021 1:42 pm · Rodgers Raphael
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni pamoja na mafunzo ya takwimu.
  • Kingine ni kuangazia fursa za uongozi kimataifa.
  • Badala ya kulalamika ukosefu wa ajira, waangazie ujasiriamali.

Dar es Salaam. Mwaka 2021 ndiyo hivyo, tunauaga ndani ya siku chache zilizosalia na kuukaribisha mwaka 2022.

Pamoja na ukweli huo, siyo sawa kuingia kwenye mwaka mpya bila malengo. Kama kijana unapaswa kuwa “smart”, kuwa na vitu ambavyo ungependa kuona vinatimia kabla ya Desemba mwaka 2022.

Inaweza ikawa ni kupanga geto lako, kuwasaidia wazazi kitu fulani, kununua kiwanja na hata kuanza ujenzi wa nyumba ya ndoto yako. 

Yote hiyo ni mipango ambayo mtu anatakiwa kuweka maazimio ya mwaka mpya kuikamilisha.

Je, wewe hadi sasa umeweka maazimio gani?

Pamoja na mipango yako, siyo busara kufumbia macho mambo yanayokuzunguka ambayo yanakua kwa kasi kutokana na mwenendo wa maendeleo na ukuaji wa teknolojia. 

Ukishupaza shingo yako, huenda ukaachwa nyuma na treni ya mafanikio.

Kwa mwaka 2022, jenga mazowea ya kujifunza zaidi. Picha Include.

Kutokana na hali halisi ya maisha, kwa mwaka 2022, angazia kati ya haya:

Uelewa, uchambuzi wa takwimu

Katika karne ambayo shughuli nyingi zinafanyika mtandaoni, elimu ya takwimu ni kati ya maarifa muhimu kuwa nayo.

Elimu hii inamsaidia mtu kufanya maamuzi kutokana na takwimu (data) na hata kutabiri mambo yanayokuja, maarifa ambayo ni muhimu kwa mtu binafsi na hata kwa kampuni au biashara.

Mkurugenzi mtendaji wa kampuni ya habari na teknolojia ya Nukta Africa inayojishughulisha na Teknolojia ya Habari, Nuzulack Dausen amesema vijana kukosa maarifa ya uchambuzi wa takwimu ni hatari kwani itasababisha kampuni zilizopo nchini kuajiri watu wa nje ya nchi kufanya kazi hizo.

“Sehemu kubwa watu wanafanya maamuzi kwa kutumia takwimu. Tunahitaji vijana ambao wataweza kufafanua na kutafsiri takwimu ili kuweza kuzisaidia taasisi na watu wa kawaida kupata picha kamili na kufanya maamuzi,” amesema Dausen.

Mdau huyo wa takwimu amesema kwa ambao wanafanya maamuzi ya masomo, huenda ni sahihi kuangazia masomo ya takwimu yanayotolewa na badhi ya kampuni ikiwemo Nukta Africa na vyuo vya mtandaoni.

“Vijana wajifunze siyo lazima kwa ajili ya kazi lakini kwa kupata uelewa na kuweza kumudu mahitaji ya ulimwengu wa sasa,” ameshauri Dausen.


Soma zaidi


Fursa za uongozi za kimataifa

Ukizungumzia uongozi, kwa baadhi ya vijana wa Kitanzania wanawaza udiwani, ukuu wa mkoa, ubunge na nyadhifa mbalimbali za kitaifa. 

Ni wachache ambao wanaona fursa katika ngazi za kimataifa ikiwemo ngazi zilizopo kwa ajili ya vijana katika Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), jumuiya za kikanda na Umoja wa Mataifa (UN).

Balozi wa vijana wa EAC, Jessica Mshama amesema mwaka 2022 ni muda wa vijana kuangalia fursa zilizopo nje ya mipaka ya Tanzania kwani ushiriki wa Watanzania siyo mkubwa.

“Kuna fursa nyingi za uongozi ambazo vijana wa Tanzania hawazichangamkii. Baadhi ni kutokana na kutokuzijua na wengine kujidogosha kwa kuona hawakidhi vigezo,” amesema Mshama.

Kwa mwaka 2022, vijana walio na chachu ya uongozi wanashauriwa na balozi huyo kuangazia fursa za kimataifa ili kuongeza ushiriki wa Watanzania kwenye uongozi wa ngazi hizo.

“Unaweza kujiona duni au haustahili fursa hizo lakini ukweli ni kuwa, fursa hizo zipo kwa ajili ya kila mtu. Ukiziona, jiandikishe, zifuatilie, huenda ni fursa yako,” amesema Mshama.

Jitahidi kukamata fursa za uongozi hasa za ngazi za kimataifa. Picha| TEDSF.

Kuongeza vyanzo vya mapato

Kama ulikuwa na miaka 26, miaka 27 ndiyo inagonga hodi hiyo. Sikupatii presha ya umri lakini nakukumbusha tu kuwa haurudi utotoni.

Mbali na ajira za ujasiriamali unaoufanya, huenda kwa mwaka 2022 ikawa ni busara kuongeza mirija ya yako ya kukuingizia kipato.

Mtengeneza maudhui ya kidijitali, Wilson Nkya amesema kwa mwaka unaoanza siku chache zijazo, ni busara kwa kijana kuangazia hali yake ya kiuchumi na kuwajibika nayo.

Nkya amesema, “nadhani vijana waweke kipaumbele katika menejimenti ya fedha na waongeze mianya ya kipato, wawekeze kwenye ujuzi wa kidijitali kwa maana tupo kwenye karne ya dijitali na wajifunze kupata fedha kutokana na vipaji vyao.”

Hiyo inamaanisha, kama wewe una kipaji cha kucheza mpira, huenda ni muda wako kukitumia kipaji chako katika kuingiza kipato.

Mbali na hayo, zipo fursa katika sekta za kilimo, utalii, fedha za kidijitali (forex na bitcoin) pamoja na hati fungani ambazo vijana wanaweza kuwekeza fedha kidogo wanazozipata huko.

Afisa maliasili watu kutoka kampuni ya masuala ya ajira, Cv People, Noemi Museveni ameshauri vijana kutokutunza fedha zao kwenye vibubu kwani hazizaliani.

Badala yake, wawekeze fedha hizo kwenye mifumo ambayo inaweza kuwalipa ikiwemo hati fugani.

“Ni kweli vijana hujitahidi kuhifadhi fedha lakini kuziacha zikakaa tu haina faida. Badala yake, waziwekeze kwenye kilimo, forex, bitcoin ambapo kuna uwezekano wakafaidika nazo kadri siku zinavyokwenda,” ameshauri Museveni.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW