Jinsi unavyoweza kuishinda sonona isiharibu maisha binafsi, kazi

Zahara Tunda 0554Hrs   Agosti 14, 2018 Habari
  • Zaidi ya watu 300 milioni wameathirika na sonona duniani.
  • Inasababisha karibu watu 800,000 duniani kujiua kila mwaka.
  • Wanawake wanaathirika zaidi kuliko wanaume.

Dar es Salaam. Unahisi hauna umuhimu wa kuishi duniani au hauna amani tena katika moyo wako kwasababu tu unaona dunia yote inakuelemea? Inawezekana kabisa ikawa ni dalili za sonona (depression) na hii imekuwa ni chanzo kikubwa cha magonjwa na ulemavu kwa watu wengi duniani.

Sonona haitokei bila sababu ya msingi ila ni muunganiko wa sababu mbalimbali ambazo zisipodhibitiwa mapema zinaweza kuhatarisha mfumo mzima wa maisha yako ikiwemo afya na kazi na hata kifo.

Sonona ni muitikio wa kihisia ambao hutokea kwa mtu baada ya kushuhudia tukio baya katika maisha yake. Matukio hayo hutofautiana kutoka yale ya kawaida kama kupewa talaka, kuumwa, ajali, kufiwa na ndugu wa karibu mpaka matukio ya kushtusha  ya vita, kubakwa, mateso, maumivu makali na mauaji ya  halaiki (kimbari).

Chama Cha Tiba ya Magonjwa ya Akili cha Marekani (PTSD) kinaelezea kuwa matukio hayo humletea mtu hisia za hofu, mashaka, wasiwasi, kujitenga, kilio na mshtuko na mwingine kuogopa kuwaona watu fulani au kutembelea maeneo ambayo matukio hayo yametokea.

     Sonona humfanya mtu kuwa mpweke, mwenye hofu, mashaka na asipopata matibabu anaweza kupata ugonjwa wa akili. picha| Mtandao

Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), sonona imeathiri watu takribani 300 milioni ambapo kila mwaka husababisha matukio karibu 800,000 ya watu kujiua duniani.

Mila, desturi na mtazamo hasi dhidi ya baadhi ya makundi ya watu una nafasi kubwa kuendeleza sonona katika jamii ambapo wanaoathirika zaidi ni wanawake na watoto.  

“Nilifiwa na mtoto wangu (Marcus Mwemezi) akiwa na umri wa miaka sita kwa kweli ilinitesa hadi ikanipelekea kutaka kujiua, nilikaa miaka miwili bila kufanya biashara yangu hivyo iliniathiri kiafya na kiuchumi pia,” anasema Belinda Nyapili (31) mkazi wa jijini Dar es Salaam.

              Belinda Nyapili akifafanua jambo wakati wa semina za ushauri wa kujilinda na sonona. Picha ya |The Citizen

Belinda hakupenda kumuona mtoto wake anafariki katika umri mdogo na kukatiza furaha ya kukulewa na wazazi wake kama watoto wengine.

Katika hali hiyo hakuona maana ya kuendelea kuishi wakati mwingi alikuwa anajifungia chumbani na mara kadhaa alijaribu kujiua kama njia ya kukabiliana na sonona. Lakini kupitia msaada wa wataalamu wa saikolojia alipata tiba iliyomrejeshea matumaini ya kuishi tena na  kuendelea kufanya shughuli za maendeleo.  

Mwaka 2016 alianzisha taasisi ya Marcus Mwemezi Foundation ili kumuenzi mtoto wake na anaitumia taasisi hiyo kutoa elimu kwa wanawake ambao wameathirika na sonona.

“Ushauri wangu watu waache kujificha na watafute msaada kwa madaktari na washauri hata kuzungumza na marafiki na kuja kwenye sehemu ambazo zinatoa msaada kwa watu wenye matatizo ya sonona,” anasema Belinda.

Wataalamu wa saikolojia wanashauri watu kuchukua hatua muhimu kujilinda kabla sonona haijatokea ili kupunguza athari zinazoweza kutokea ikiwa mtu hajapata elimu.

Mtaalamu wa Afya ya Akili wilaya ya Mbinga, Dk Silvia Ngonyani anawashauri watu kufanya mazoezi mara kwa mara na kuuchangamsha mwili muda wote kwasababu mazoezi yanaupa mwili nguvu za kutosha kukabiliana na hatari yoyote inayoweza kutokea.  

Dk. anabainisha kuwa watu wavinje ukimya na kuzungumza na watu wanaowaamini pale wanapokutana na matatizo ambayo hawawezi kuyatatua wenyewe.

“Tumia muda wako mwingi kujichanganya na marafiki au familia itakufanya ujihisi vizuri na unaweza kupata mtu wa kumweleza kinachokusumbua wanaweza kukusaidia kwa namna moja au nyingine,” anasema Dkt. Ngonyani.

Sonona inatibika kama utakuwa mkweli na kukubali kuzungumza kitu kinachokusumbua kwa kwenda hospitali ambapo kupitia daktari atajua ni kwa kiasi gani umeathiriwa.

“Sonona inatibika kwanza mgonjwa atapatiwa dawa kisha ataanza kupata matibabu ya mazungumzo kitaalamu yanajulikana kama ‘Psychotherapy’ au ‘Talk therapy’,” anaeleza Dk Ngonyani.


Related Post