Sekta za uwekezaji kuziangazia mwaka 2022

January 8, 2022 8:07 am · Wilson
Share
Tweet
Copy Link
  • Uwekezaji huo unaweza kufanyika katika sekta za utalii, teknolojia na sanaa. 
  • Sekta hizi zinaweza kuwa chanzo kizuri cha mapato.

Dar es Salaam. Wakati tukiuanza mwaka 2022 kumekuwa na maoni mchanganyiko kuhusu mwezi Januari huku baadhi ya watu wakiuona kama mwezi mgumu katika nyanja mbalimbali za maisha.

Hayo yote ni kwa sababu watu huuchukulia Januari kama mwezi ulio na matumizi mengi ya fedha ikiwemo ulipaji wa ada za wanafunzi, kodi za nyumba na malipo ya huduma za maji na umeme.

Mtazamo mwingine ni kuwa watu wanakuwa hawana fedha za kutosha kutokana na kuzitumia katika sikukuu za mwisho wa mwaka 2021 ikiwemo Krismasi na Mwaka Mpya. 

Hata hivyo, mtazamo huo unaweza usiwe na ukweli kwa watu wote kwa sababu kila mtu ana namna yake ya kuendesha mambo. Januari kwa watu wenye malengo huutumia kujipanga namna watakavyoendesha shughuli zao kwa mwaka mzima ikiwemo kufanya uwekezaji.

Ikiwa ni mmoja wa watu hao na bado hufahamu uanzie wapi, hizi ni baadhi ya sekta ambazo unaweza kuziangazia kuwekeza ujuzi na fedha zao ili zikunufaishe: 


1: Sekta ya habari

Habari ni kati ya sekta ambazo Watanzania wanazitegemea katika kupata taarifa muhimu za kuwasaidia kufanya maamuzi. 

Mwanzilishi wa kampuni inayojihusisha na habari za sayansi na utafiti ya  Research Com, Dk Syriacus Buguzi amesema mtu akitengeneza maudhui yenye ubora yanayoweza kuwasaidia watu kufanya maamuzi ni chanzo kizuri cha mapato.

“Kuna fursa nyingi sana katika sekta ya habari hususani katika habari za ubobezi (specialized journalism) wa kitu kimoja kwani hii ni biashara ambayo itakuwa inajikita katika suala moja  tu kwa mfano habari za takwimu kutokana na soko la walaji kubadilika sana hivyo ni bora kuangalia katika vyombo vya habari tofauti na vile vilivyozoeleka,” amesema Dk Buguzi. 

Tasnia ya habari ikitumika vizuri inaweza kumtoa kimaisha mwaka hasa kama maudhui yanayozalishwa yanawanufaisha watu. Picha| European Commission.

2. Sekta ya Utalii

Huwezi kuizungumzia Tanzania bila kutaja uzuri wake uliosheheni mbuga za wanyama, milima na vivutio mbalimbali vya utalii. Kwa mujibu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, utalii unachangia asilimia 17 ya pato la Taifa, asilimia 25 ya fedha za kigeni na huzalisha ajira takribani milioni 1.6 za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja kwa mwaka.

Utalii una uwanda mpana sana kwa mtu kuwekeza ikiwemo biashara ya upigaji picha, kuuza bidhaa za utamaduni na sanaa kwa watalii, kuongoza watalii, kuanzisha migawaha na hoteli.

“Katika uwekezaji ni vema kuelewa ni vitu gani mtu anavipenda na vina fursa zipi  kubwa katika kumletea manufaa, kwa mfano katika sekta ya utalii bado kuna fursa kubwa,” amesema balozi wa vijana katika Jumuiya ya Afrika Mashariki(EAC) na Mkurugenzi wa shule ya msingi Assumpta, Jesca Mshama.


Soma zaidi:


3.Sekta ya elimu na teknolojia

Elimu ni sekta muhimu na yenye manufaa kwani inamgusa kila mtu moja kwa moja, tukiwa katika mapinduzi makubwa ya teknolojia ukuaji wa mifumo ya kidijitali unachagiza mabadiliko katika sekta ya elimu kwani kuna ujuzi au maaarifa ya teknolojia mpya hayafundishwi darasani jambo linaloweza kuwa fursa pia. 

Moja wapo ya fursa hizo ikiwa ni pamoja na kusoma au kujifunza vitu vipya, biashara ya mtandaoni na masoko. 

“Vijana wawekeze katika kusoma, kwa mfano mambo ya digitali kuna vitu vingi vya kujifunza kupita mtandao,’ amesema Mshama.


4. Sekta ya sanaa 

Sanaa ni sekta ambayo inamgusa kila mtu kwa namna moja ama nyingine bila kujali rika wala umri. Kama una kipaji chochote ikiwemo kuimba, kucheza, kuchora, kuigiza kitumie vizuri mwaka huu ili kikunufaishe.

Unaweza kukinoa kipaji chako na kujitangaza kupitia mitandao ya kijamii ikiwemo Facebook na TikTok ili kuwafikia watu wengi.

Tafuta maarifa na ujuzi kukiendeleza kipaji chako ikiwemo kujifunza kwa waliokutangulia na wekeza kukifanya kipaji kama biashara inayoweza kukuingiza kipato ili mwisho wa mwaka huu uwe miongoni mwa watu ambao hawatajuta kutokutimiza malengo yao

Wekeza fedha zako katika sekta ambazo zitajizalisha na kukuongezea kipato. Piacha| Mtandao.

5. Soko la hisa 

Baadhi ya watu hupata fedha nyingi na kushindwa kufanya maamuzi ni wapi wawekeze kutokana na kutokuwa na taarifa sahihi za mawazo ya biashara. 

Vile vile wengine pia husubiri wapate kiasi kikubwa cha pesa kwa mkupuo ndipo wawekeze, hii inakuwa ni kwa sababu ya kutokuwa na elimu na taarifa sahihi za kutumia mifuko ya hisa kukuza kipato.

Kuna mifuko mbalimbali ya hisa kuanzia zile za mashirika binafsi na Serikali ambayo mtu anaweza kuwekeza kwa kununua hisa au kuwekeza kwenye dhamana (bond) 

“Njia nyingine nzuri ni kuwekeza kwenye bond (dhamana) kwa mfano UTT (Umoja Trust Fund)  kwa kufungua akaunti ambayo mtu unaweza kuwekeza kwa  ajili ya watoto au kitu chochote.

“Hii haihitaji uwe na kiasi kikubwa  hata kuanzia Sh1,000 japo kuwa viwango vya uwekezaji vinatofautiana,” amesema mwanzilishi na mmiliki wa kampuni ya kuuza na kusambaza bidhaa za kielektroniki ya Nahitaji Tz, Blessing Rweikiza.

Kuwekeza ni jambo moja na kunufaika na uwekezaji ni jambo lingine. Kila kitu kina changamoto zake kwa hiyo ni muhimu kutafuta taarifa sahihi kabla ya kufanya uamuzi wa kuwekeza katika sekta husika.

Pia tafuta washauri wa uwekezaji unaotaka kuufanya mwaka huu ili kuepuka hasara na makosa yanayoepukika.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW