Mambo muhimu ya kufanya mwisho wa mwaka 2022

December 23, 2022 4:16 am · Lucy Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Mambo hayo ni pamoja na kutembelea maeneo mapya, pamoja na kutafakari mambo yaliyopita na yajayo.
  • Fanya uchunguzi wa afya yako.

Dar es Salaam. Kipindi cha mwisho wa mwaka kimezoeleka kuwa cha mapumziko sehemu mbalimbali duniani kutokana na uwepo wa sikukuu za Krismas na Mwaka Mpya.

Baadhi ya watu hutumia kipindi hiki kama nafasi ya kutembeleana na kujuliana hali baada ya miezi 12 ya majukumu na kazi nyingi zilizofanya wengine wasionane kabisa.

Wapo wanaotoka na marafiki kwenda sehemu mbalimbali kusherehekea mafanikio waliyopata mwaka mzima.

Mbali na mapumziko na sherehe za kila namna, yapo mambo mengi unayoweza kufanya kipindi hiki yatakuwezesha kuwa na mwaka mwingine wenye mafanikio na matokeo chanya kuliko mwaka uliopita.


Tembelea maeneo mapya

Pengine kipindi cha mwaka mzima ulikosa muda  wa kutembelea maeneo mengine na kujionea mandhari tofauti na uliyozoea. Kipindi cha mwisho wa mwaka ndio wasaa mzuri wa kufanya hivyo.

Kwa mujibu wa jarida la Forbes kutembelea maeneo mapya kunaweza kupunguza msongo wa mawazo, kuongeza furaha na ubunifu wa mambo mapya maishani.

“Kupumzika kutoka kwa pilikapilika za kila siku  na kutembelea maeneo mapya ni muhimu kwa akili yako kupumzika na kukuchangamsha,” inaeleza tovuti hiyo.

Esther William (24) mtalii wa ndani kwenye vivutio vingi nchini anasema kupanga kutembelea maeneo mapya huongeza shauku na kumpa furaha inayomfanya afanye majukumu yake haraka ili apate kutembelea sehemu hizo alizopanga.

“Napenda kutembelea maeneo mapya sio tu mwisho wa mwaka kila wakati nikipata muda, inanisaidia kuondoa msongo wa mawazo na kunipa furaha,” anasema Esther.


Tafakari  yaliyopita na yajayo ukiwa maeneo tulivu

Nenda maeneo ya ufukweni na kama una uwezo kodi chumba cha hoteli chenye utulivu na kaa ujitafakari ukiwa katika sehemu nzuri na yenye upepo mwanana.

Ikiwa unaishi karibu na bahari, maziwa, au mito ambayo pembeni kuna hoteli za kisasa tembelea maeneo hayo. Kujitoa siku moja moja sio mbaya, ila angalia sana bajeti yako usije kutumia hadi bajeti yako ya Januari.

Ukiwa huko tumia muda mwingi kufikiri mafanikio na changamoto ulizozipitia mwaka uanoelekea kuisha na namna unavyoweza kujipanga kutekeleza mipango na mikakati  mipya ya 2023.


Soma zaidi


Fanya uchunguzi wa afya yako

Pengine majukumu mengi uliyokuwa nayo kwa mwaka mzima yalikuzuia kufanya uchunguzi wa afya yako (Checkup). Mwisho wa mwaka ndiyo wakati pekee wa kufanya jambo hilo.

Kwa mujibu wa tovuti ya healthline, kufanya uchunguzi wa afya yako mwisho wa mwaka kunaweza kupunguza gharama nyingi za matibabu unazoweza kuzitumia endapo ugonjwa ukiwa mkubwa siku za mbeleni.

“Kufanya uchunguzi wa afya (checkups) huwezesha kujifunza njia mpya za kuishi maisha marefu, yenye afya”imeogeza tovuti hiyo.


Gusa mahitaji ya msingi ya watu wengine

Kwa watu wa imani watakubaliana na mimi kuwa maandiko matakatifu ya dini zote yanatutaka kuwasaidia watu wengine wenye mahitaji wakiwemo wajane na yatima.

Wakati wewe umebarikiwa kiasi cha kuwa mzima na uwezo wa kufanya kazi kuna wengine ambao ni wagonjwa mahospitalini na hawana msaada. Kuna watoto yatima, wazee na wajane wanaohitaji msaada na faraja kutoka kwa watu mbalimbali ukiwemo wewe.

Ukipata muda kidogo unaweza kutembelea vituo vya watoto yatima, nyumba za kutunzia wazee, au hospitalini kuwaona wagonjwa. 

Siyo lazima uwe na pesa kuwatembelea tu nakuwatia moyo kunaweza kuleta maana kubwa kwenye maisha yao.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW