Namna bora ya kupanga, kutimiza malengo yako mwaka 2023

January 31, 2023 11:50 am · admin
Share
Tweet
Copy Link

Kuandika malengo ni miongoni mwa njia itakayokusaidia kuyakumbuka na kuyafuatilia. Pichal Esau Ng’umbi.


  • Ni pamoja na kuwa na utaratibu wa kuyapitia mara kwa mara. 
  • Weka malengo yanayopimika na yenye uhalisia.

Dar es Salaam. Hongera kwa kufika mwishoni mwa mwaka 2022, ni dalili njema kuwa upo uwezekano wa kuuanza mwaka 2023 kwa kishindo. Umetimiza malengo yako uliyojiwekea mwaka huu?

Kongole kwa wale waliokamilisha malengo au sehemu ya malengo yao. Mwanzoni mwa mwaka huwa ni muda mzuri wa kujiwekea malengo na mipango ya kuikamilisha katika mwaka husika. Baadhi huandika, wengine huazimia tu moyoni.

Baadhi ya watu wamekuwa wakianguka katika hatua za mwanzoni tu baada ya kuweka malengo yao, na kujikatia tamaa vipi kama ukijaribu mbinu hizi ambazo zinaweza kukusaidia kujiwekea malengo na namna ya kukamilisha kwa njia rahisi kabisa:

1. Andika malengo yako na yapitie mara kwa mara 

Malengo ambayo hayajaandikwa yana nafasi kubwa ya kutokamilika. Jambo la msingi ni kuyaandika na siyo tu mahali  popote bali yaandikwe katika sehemu ambayo unaweza kuyaona mara kwa mara na kuyafanyia tathmini.

Unaweza kuyabandika chumbani karibu na kitanda ili uyaone kabla ya kulala na baada ya kuamka,  au katika kioo cha bafuni, au unaweza kuyapiga picha na kuyatumia kama picha ya kupamba ukurasa wa mbele wa simu yako, au kompyuta.

2. Weka malengo katika nyanja tofauti za maisha yako

Ni muhimu kuweka malengo katika nyanja zaidi ya moja maishani mwako, hasa zile zinazohusiana. Mfano ukijiwekea malengo ya kukua kiuchumi lazima utazame na mambo ambayo yatakusaidia kupunguza matumizi na kuweka akiba.

Unaweza kuweka malengo katika mahusiano, malengo ya kikazi, kiafya, kiuchumi, kiroho au malengo ya kukua kitaaluma.


Soma zaidi


3. Weka malengo ya kweli na yanayoweza kufikiwa

Baadhi ya watu hujiwekea malengo makubwa ambayo kiuhalisia huwa ni vigumu kuyatimiza. Wakati wa kuweka malengo ni muhimu kuzingatia kwamba yanatakiwa yafanyiwe kazi ndani ya miezi 12.

Hivyo badala ya kuweka malengo makubwa ambayo yanaweza kukupa uvivu wa kuyakamilisha unaweza kuweka malengo madogo madogo lakini yenye uhalisia na yanayoweza kutimia kwa muda uliotenga.

4. Jiwekee malengo yanayopimika 

Ili kusalia katika safari ya kutimiza malengo yako unapaswa kuwa na malengo yanayopimika na unayoweza kuyafanyia tathmini kila wakati na kujua umeyatimiza kwa kiwango fulani badala ya kuwa na malengo ya jumla.

Mathalan,  unaweza kusema nitakuwa natenga Sh20,000 kwa ajili ya kulipa madeni kila mwezi badala ya kusema naweka malengo ya kupunguza madeni.

Au unaweza kusema nitakuwa nashiriki mlo wa kifungua kinywa na familia mara tatu kwa wiki badala ya kusema ntaongeza muda wa kuwa karibu na familia.

Malengo yanayopimika ni rahisi kuyafanyia tathmini na kujua wapi unatakiwa kuongeza nguvu au kupunguza.

Unaposhirikiana na mtu au watu unaowaamini katika malengo yako kunakupa uwezekano mkubwa wa kutimiza malengo hayo. Pichal Esau Ng’umbi. 

5. Shirikiana na watu wengine 

Ni vizuri kuwa na malengo binafsi lakini ni vizuri zaidi ukiwa na malengo ya kutimiza kwa kushirikiana na watu wengine hiyo itakusaidia kukua zaidi kwani mtapeana moyo na ni rahisi kupata suluhu inapotokea changamoto inayoweza kuathiri malengo yako au yenu.

Jambo la muhimu ni kuchagua mtu sahihi wa kushirikiana naye kutimiza malengo husika ambapo unaweza kushirikiana na mke/mume au wafanyakazi wenzako au rafiki wa karibu ambaye unamfahamu vizuri mienendo yake.


6. Jipongeze unapokamilisha sehemu ya malengo

Ndio! Utapata ari na chachu ya kujiwekea malengo mapya ikiwa utakuwa na utaratibu wa kujipongeza pale unapotimiza malengo yako au sehemu ya malengo. Jambo la msingi ni kuhakikisha pongezi yako haiwi sababu ya kuharibu malengo uliyoweka.

Follow us on TikTok

Nukta Habari

FOLLOW NOW
Subscribe to our channel

Nukta TV

SUBSCRIBE NOW
🔴LIVE: LIVE:WABUNGE WAKIWACHAPA MASWALI MAWAZIRI | Bunge la 13 | Kikao cha 28

🔴LIVE: LIVE:WABUNGE WAKIWACHAPA MASWALI MAWAZIRI | Bunge la 13 | Kikao cha 28

Nukta TV

Top 10 ya magari yanayotumia kiwango kidogo cha mafuta

Top 10 ya magari yanayotumia kiwango kidogo cha mafuta

Nukta TV

SGR yaingizia Serikali Sh169.37 bilioni tangu kuanza kwa safari Juni 2024

SGR yaingizia Serikali Sh169.37 bilioni tangu kuanza kwa safari Juni 2024

Nukta TV