Ukuaji wa uchumi duniani kuendelea kuporomoka 2022

January 14, 2022 2:17 pm · Maria
Share
Tweet
Copy Link
  • Ukuaji wa uchumi duniani unatarajiwa kupungua kutoka asilimia 5.5 mwaka 2021 hadi asilimia 4.1 mwaka huu.
  • Hali hiyo imechangiwa na athari za Uviko-19.
  • Watunga sera ulimwenguni waaswa kuwa waangalifu katika utungaji wa sera ya kifedha.

Dar es Salaam. Uchumi wa dunia huenda ukaendelea kuporomoka baada ya Benki ya Dunia kueleza kuwa ukuaji wa uchumi huo unatarajiwa kupungua kwa kiasi kikubwa kutoka asilimia 5.5 mwaka 2021 hadi asilimia 4.1 mwaka 2022.

Benki ya Dunia katika ripoti ya utafiti wake unaohusu matarajio ya kiuchumi  kwa mwaka 2022 imesema hali ya uchumi itaendelea kuwa mnaya hata mwaka 2023 na kukadiria kuwa ukuaji wa uchumi duniani utashuka hadi kufikia asilimia 3.2.

Hali hiyo inaweza kusababisha baadhi ya shughuli za uwekezaji na biashara ikiwemo usaidizi wa kifedha kwa nchi  zinazoendelea kupungua.

Mkurugenzi wa Idara ya kuangalia matarajio ya kiuchumi katika Benki ya Dunia, Ahyan Kose ameeleza kuwa sababu za kupungua kwa ukuaji wa uchumi duniani ni kupungua kwa mahitaji na watungaji wa sera ulimwenguni kote kuondoa hatua za usaidizi zilizopo sasa hali ambayo itasababisha uchumi kukua pole pole. 

Kose akizungumza baada ya kutolewa kwa ripoti hiyo Januari 11, 2022 ameeleza kuwa “bila shaka huko tuendako kutakuwa na hatari zaidi. Janga la Corona bado lipo nasi, madeni bado yapo juu sana na shinikizo la mfumuko wa bei.

 “Watunga sera wanahitaji kuwa waangalifu ili kujiadhari na hatari zinazokuja na kukabiliana nazo.” Benki ya Dunia imesema pia kudorora kwa uchumi kunaenda kuongeza tofauti katika viwango vya ukuaji kati ya nchi zilizoendelea kiuchumi, zinazoibukia na zinazoendelea.

Uchumi wa nchi zilizoendelea unatarajiwa kupungua kutoka asilimia tano mwaka wa 2021 hadi asilimia 3.8 mwaka wa 2022 na asilimia 2.3 mwaka wa 2023. 


Soma zaidi:


Hata hivyo, katika nchi zinazoibukia na zinazoendelea, ukuaji unatarajiwa kushuka kutoka asilimia 6.3 mwaka 2021 hadi asilimia 4.6 mwaka 2022 na asilimia 4.4 mwaka 2023.

Licha ya kuwa uchumi wa dunia unaendelea kudorora, kwa Tanzania hali imekua tofauti ambapo uchumi wa nchi umeanza kuimarika.Ripoti ya vidokezo vya pato la Taifa kwa robo ya Julai hadi Septemba mwaka 2021 iliyotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) na Wizara ya Fedha na Mipango Desemba mwaka jana imeeleza kuwa uchumi wa Tanzania katika robo ya tatu ya mwaka jana ulikua kwa asilimia 5.2.

Hilo ni sawa na ongezeko la asilimia 0.8 ukilinganisha na ukuaji wa uchumi wa asilimia 4.4 kipindi kama hicho wa mwaka 2020.

Kuimarika kwa uchumi wa Tanzania kunachangiwa na shughuli mbalimbali za kiuchumi zikiwemo ujenzi ambao umechangia kwa asilimia 18.1 ukifuatiwa na kilimo (asilimia 15.1), shughuli za madini (asilimia 11.4) na uzalishaji  viwandani kwa asilimia  8.6.

Lakini mbali na shughuli hizo, ukuaji huo wa uchumi ulianza kuimarika kipindi ambacho mapambano dhidi ya janga la corona yalitiliwa mkazo kwa namna mbalimbali ikiwemo utoaji wa chanjo na kuendelea kuchukuliwa kwa tahadhari ili watu waweze kurudi katika  shughuli za uzalishaji.

                     

Suluhu ya kudorora kwa uchumi wa dunia

Benki ya Dunia imeeleza kuwa ili  kukabiliana na kudorora kwa uchumi wa dunia katika ngazi ya nchi, watunga sera wa kitaifa wanatakiwa kuondoa kwa uangalifu sera ya fedha na kufikiria juu ya matokeo ya maamuzi yao, na wakati huo huo kuwasiliana kwa uwazi juu ya kile wanachojaribu kufanya. 

“Hii inamaanisha wawe na mipango ya muda wa kati na mrefu kwa ngazi ya taifa,” amesema Kose.

Pia unahitajika ushirikiano madhubuti wa kimataifa katika kutoa chanjo dhidi ya Uviko-19, msamaha wa madeni na mabadiliko ya tabianchi. 

“Yote haya yatahitaji jumuiya ya kimataifa kufanya kazi kwa pamoja na kuzichukulia changamoto hizi kwa uzito, na kutekeleza sera zinazohitajika,” ameongeza mtaalam huyo wa Benki ya Dunia.

Follow us on TikTok

Nukta Habari

FOLLOW NOW
Subscribe to our channel

Nukta TV

SUBSCRIBE NOW
Rais Samia azindua minara 758, aacha maagizo mazito juu ya mkongo wa taifa

Rais Samia azindua minara 758, aacha maagizo mazito juu ya mkongo wa taifa

Nukta TV

JAJI MKUU: Njia za asili ni mojawapo ya njia halali za utatuzi wa migogoro

JAJI MKUU: Njia za asili ni mojawapo ya njia halali za utatuzi wa migogoro

Nukta TV

Hesabu ya bosi, bei ya mafuta pasua kichwa madereva wa daladala

Hesabu ya bosi, bei ya mafuta pasua kichwa madereva wa daladala

Nukta TV