Uchumi wazidi kuimarika Tanzania: BoT

February 12, 2019 1:37 pm · Nuzulack Dausen
Share
Tweet
Copy Link

Ujenzi wa reli ya kisasa (Standard Gauge Railway line (SGR)) kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro itakayogharimu Sh2.7 trilioni ikiwa ni sehemu ya mradi wa kilomita 1,219 hadi Mwanza utachochea ukuaji wa uchumi 2019. Picha|Mtandao.


  • Benki Kuu ya Tanzania (BoT) yabainisha kuwa shughuli za ujenzi ziliongoza kukua kwa kasi katika kipindi cha Januari hadi Septemba 2018 zikifuatiwa na mawasiliano, viwanda na madini.
  • Ukuaji katika shughuli za ujenzi ulichangiwa zaidi na ujenzi wa reli, barabara, madaraja na majengo.
  • Benki hiyo inatarajia kuwa uchumi utakuwa kwa wastani wa asilimia 7.3 mwaka 2019 ikilinganishwa na matarajio ya ukuaji wa asilimia 7.2 mwaka jana. 
  • Mchango wa shughuli za madini katika ukuaji halisi wa pato la Taifa umeshuka zaidi ya mara mbili hadi asilimia 5.2 katika robo tatu za kwanza mwaka 2018 kutoka asilimia 12.7 mwaka 2017.

Dar es Salaam. Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imesema kuwa uchumi umeendelea kuimarika baada ya kukua kwa wastani wa asilimia 6.7  katika robo tatu za kwanza za mwaka 2018 kutoka asilimia 6.2 kipindi kama hicho mwaka 2017 ukichangiwa zaidi na shughuli za ujenzi, biashara, kilimo na viwanda.

Katika Muhtasari wa tathmini ya tamko la sera ya fedha wa mapitio ya nusu mwaka wa 2018/19 ya Februari mwaka huu, BoT inaeleza kuwa shughuli za ujenzi ndiyo zilikua kwa kasi zaidi katika kipindi hicho kwa asilimia 13 huku zikiongoza kwa kuchangia kiwango kikubwa cha ukuaji wa pato halisi la Taifa (Real GDP) kwa asilimia 23.1.

“Ukuaji katika shughuli za ujenzi ulichangiwa zaidi na ujenzi wa reli, barabara, madaraja na majengo,” inaeleza sehemu ya muhtasari huo wa sera ya fedha. 

Kwa sasa Serikali inaendelea na ujenzi wa reli ya kisasa (Standard Gauge Railway line (SGR)) kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro itakayogharimu Sh2.7 trilioni ikiwa ni sehemu ya mradi wa kilomita 1,219 hadi Mwanza.

Sanjari na SGR kuna ukarabati wa reli ya kati unaoendelea hasa katika njia ya kuelekea mikoa ya Kaskazini mwa Tanzania na ujenzi wa madaraja mbalimbali ikiwemo la juu katika makutano ya Barabara ya Morogoro na Sam Nujoma/Mandela katika eneo la Ubungo jijini Dar es Salaam.


Soma zaidi:


Shughuli nyingine zilizochangia kwa kiwango kikubwa katika ukuaji wa pato halisi la Taifa katika robo tatu za awali za mwaka jana ni biashara kwa asilimia 11.1, kilimo (10.7) na viwanda zilizochangia kwa asilimia 10.

Ujenzi umeshusha kileleni shughuli za madini ambazo katika kipindi kama hicho mwaka 2017 zilikua kwa kasi ya asilimia 23.8.

Hata hivyo, mchango wake katika ukuaji wa pato halisi la Taifa umeendelea kubaki kama ilivyokuwa katika robo tatu za kwanza mwaka 2017 kwa asilimia 23.1.

Miongoni mwa sekta zilizoporomoka katika uchangiaji wa ukuaji wa pato halisi la Taifa katika kipindi hicho cha mapitio ni shughuli za madini ambazo zimeshuka zaidi ya mara mbili kutoka asilimia 12.7 mwaka 2017 hadi asilimia 5.2 katika robo tatu za kwanza mwaka jana.

BoT inatarajia kuwa uchumi mwaka huu utakua kwa kasi ya asilimia 7.3 kutoka asilimia 7.2 iliyokadiriwa mwaka jana ukichagizwa zaidi na uwekezaji wa umma katika miradi mikubwa ya miundombinu, maratajio ya ukuaji imara wa uchumi duniani na hali nzuri ya hewa.

Enable Notifications OK No thanks