Uchumi wa Tanzania kukua kwa asilimia 6.1 ifikapo 2025
- Hatua hiyo imechangiwa na ushirikishwaji wa wadau mbalimbali wa maendeleo.
- Makadirio hayo ya muda mfupi ya Benki ya Dunia yapo sanjari na makadirio ya Serikali.
Dar es Salaam. Benki ya Dunia (WB) inatazamia uchumi wa Tanzania kukua kwa kasi ya asilimia 6.1 ifikapo mwaka 2025 ikichagizwa zaidi na uboreshaji wa mazingira ya ufanyaji biashara huku ikihofia kuongezeka kwa tofauti ya kipato kati ya wenye nacho na wasionacho.
Makadirio hayo ya Benki ya Dunia yanatoa matumaini kuwa huenda kasi ya ukuaji wa uchumi wa Tanzania ikarejea katika kiwango cha wastani wa asilimia 7 kilichorekodiwa kwa takriban muongo mmoja kabla ya kuporomoshwa na madhara ya Uviko-19 mwaka 2020.
Katika kipindi cha muda mfupi, ripoti ya 19 ya hali ya uchumi wa Tanzania ya benki hiyo (19th Tanzania Economic Update) inaeleza kuwa uchumi wa Tanzania unatarajiwa kukua kwa wastani wa asilimia 5.1 mwaka huu kutoka asilimia 4.7 iliyorekodiwa mwaka 2022.
“Pato la nchi linarajiwa kukua kwa asilimia 5.1 kwa mwaka 2023 ikichangiwa na mazingira bora ya biashara na mabadiliko ya kisera…ikiwa ni matokeo ya Serikali kuboresha miundombinu ya kilimo kilichoajiri asilimia 70 ya wakazi wa vijijini,” Mkurugenzi mkazi wa Benki ya Dunia, Nathan Belete ameeleza leo wakati wa uzinduzi wa ripoti hiyo.
Zinazohusiana
- Kasi ya mfumuko wa bei yang’ania kiwango cha Julai
- Mambo yatakayozisaidia nchi za Afrika kuongeza mapato ya kodi
Hata hivyo, makadirio hayo ya Benki ya Dunia yapo sanjari na makadirio ya Serikali ya kufikia kasi ya ukuaji wa uchumi ya asilimia 5.2 mwaka huu.
Miaka mitano iliyopita matarajio ya ukuaji wa uchumi kati ya B enki ya Dunia na Serikali yalikuwa yakitofautiana kwa kiasi kikubwa jambo lililozua mjadala miongoni mwa wadau juu ya ubora wa takwimu za Serikali.
Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba aliyekuwa akizungumza wakati wa kuzindua ripoti hiyo amesema licha ya madhara yatokanayo na Uviko-19 pamoja na vita vya Urusi na Ukraine, ripoti hiyo imeonyesha matumaini ya ukuaji wa uchumi nchini.
Amesema hatua hiyo ya ukuaji imechangiwa na ushirikishwaji wa wadau mbalimbali wa maendeleo katika utungaji wa sera rafiki zilizowawezesha kukabiliana na changamoto hizo zilizosababisha uchumi wa dunia kuzorota.
“Ukuaji wa uchumi wetu unatokana na sera na programu za kushughulikia athari za vita, uwekezaji wa kimkakati katika miundombinu ya nishati, maji, elimu, afya, usafirishaji na kuongezeka kwa shughuli za utalii,” amesema Nchemba.

Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba akizungumza wakati wa kuzindua ripoti ya hali ya uchumi wa Tanzania jijini Dar es Salaam.Picha|World BankTanzania/Twitter
Katika ripoti hiyo iitwayo ‘Ripoti ya 19 ya hali ya uchumi: Ufanisi na ubora wa sera ya fedha Tanzania’ WB imeeleza kuwa uchumi wa Tanzania umeimarika katika viashiria mbalimbali ikiwemo uhimilivu wa deni la taifa, mfumuko wa bei pamoja na hifadhi ya fedha za kigeni.
Ripoti hiyo inaeleza kuwa Serikali ilitumia asilimia 4.6 ya pato la taifa mwaka 2020/202 kwa ajili ya sekta ya maendeleo ya kiuchumi hususan kuwezesha shughuli mbalimbali kama biashara, kilimo, nishati, madini pamoja ujenzi wa miundombinu ya barabara.
WB inaeleza kuwa kwa sasa Tanzania inahitaji kuboresha ufanisi matumizi ya umma na kukuza mapato.
“Serikali inapaswa kutathmini na kudhibiti uhamishaji wa bajeti kwenda kwa mashirika ya umma ili kuhakikisha ukuaji endelevu,” inaeleza sehemu ya ripoti hiyo.