Ahueni: Uchumi waanza kuimarika Tanzania

January 10, 2022 12:23 pm · Maria
Share
Tweet
Copy Link

                     


  • Katika robo ya tatu ya mwaka jana uchumi ulikua kwa asilimia 5.2 kutoka asilimia 4.4 mwaka 2020.
  • Ulichangiwa na kuimarika kwa mapambano dhidi ya Uviko-19.
  • Pia ukuaji wa shughuli za ujenzi, kilimo na madini.

Dar es Salaam. Licha ya Tanzania kuwa miongoni mwa nchi zilizoathiriwa na janga la Corona (Uviko-19), uchumi wake umeanza kuimarika, jambo linatoa matumaini mapya kwa raia wake kuboresha maisha yao.

Ripoti ya vidokezo vya pato la Taifa kwa robo ya Julai hadi Septemba mwaka 2021 iliyotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) na Wizara ya Fedha na Mipango Desemba mwaka jana imeeleza kuwa uchumi wa Tanzania katika robo ya tatu ya mwaka jana ulikua kwa asilimia 5.2.

Hilo ni sawa na ongezeko la asilimia 0.8 ukilinganisha na ukuaji wa uchumi wa asilimia 4.4 kipindi kama hicho wa mwaka 2020.

Ukuaji huo wa uchumi umeanza kuimarika katika kipindi ambacho mapambano dhidi ya Uviko-19 yameimarishwa maeneo mbalimbali duniani ikiwemo utoaji wa chanjo na kuendelea kuchukuliwa kwa tahadhari ili watu warejea katika shughuli za uzalishaji mali.

Ripoti hiyo ambayo inapatikana katika tovuti ya NBS inaeleza kuwa kiwango hicho cha ukuaji wa uchumi kimechangiwa na shughuli mbalimbali za kiuchumi zikiwemo ujenzi ambao umechangia kwa asilimia 18.1 ukifuatiwa na kilimo (asilimia 15.1), shughuli za madini (asilimia 11.4) na uzalishaji  viwandani kwa asilimia  8.6.

Mbali na shughuli mbalimbali za kiuchumi zilizochangia katika ukuaji wa uchumi, zipo sekta zilizorekodiwa kukua kwa kasi katika kipindi ikiwemo malazi na huduma za chakula ambayo imekua kwa asilimia 14.3. 

Sekta nyingine ni shughuli za madini kwa asilimia 12.2, sanaa na burudani, waajiri wa kaya (asilimia 12.1), elimu (asilimia 10.3), usambazaji wa umeme (asilimia 10) na habari na mawasiliano kwa asilimia 9.3.


Soma zaidi:


Ukiachilia mbali Tanzania, nchi zingine za Afrika Mashariki ambazo zimerekodiwa kufanya vizuri katika ukuaji wa uchumi katika robo ya tatu ya mwaka 2021 ni pamoja na Rwanda ambayo imekua kwa asilima 10.1 ukilinganisha na kipindi kama hicho kwa mwaka 2020 ambapo uchumi wake ulikua kwa asilimia 3.6.

Uganda uchumi wake umekua kwa asilimia 3.8 ukilinganisha na mwaka juzi ambapo uchumi wake ulikuwa kwa asilimia 0.8.

Katika nyanja za kimataifa, ukuaji wa uchumi wa dunia umekadiriwa kukua kwa asilimia 5.9 katika robo ya tatu ya mwaka 2021 ambao ni pungufu ya asilimia 0.1 ikilinganishwa na ule wa robo ya pili. 

Sababu zilizochangia kushuka kwa uchumi wa dunia mwaka jana ni athari za janga la Uviko-19 katika sekta ya utalii na uzalishaji.

Uchumi wa dunia kwa mwaka 2022 unakadiriwa kukua kwa kiwango cha asilimia 4.9. Makadirio hayo yamehusisha mwenendo wa janga la Uviko-19 katika nchi zenye kipato cha chini.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW