Mfumuko wa bei Tanzania: Tafsiri hafifu na athari zake

January 16, 2022 8:24 am · Daniel Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Unasababisha kupanda kwa gharama za maisha kwa wananchi wa kawaida.
  • Suluhu ni kuelekeza mikopo kwenye sekta ya viwanda na kilimo.

Mapema juma hili, Benki ya Dunia ilitoa matarajio yake ya hali ya uchumi wa dunia mwaka 2022 ikibainisha kuwa uchumi utakua kwa wastani wa asilimia 4.1 mwaka 2022 ukilinganisha na asilimia 5.5 mwaka 2021.

Benki hiyo inatarajia kuwa ukuaji huo utashuka zaidi hadi kufikia asilimia 3.2 mwaka 2023. Huenda mambo yakabadilika mbeleni kwa kuwa haya ni matarajio tu.

Kwa upande wa Afrika, taarifa ya Shirika la Fedha Duniani (IMF) inaonesha kuwa kasi ya ukuaji wa uchumi Kusini mwa Jangwa la Sahara itaongezeka tu kwa asilimia 0.1 kufikia asilimia 3.8 mwaka 2022.

Pamoja na ukuaji huo, Benki ya Dunia inaeleza kuwa ongezeko la mwanya wa vipato duniani ni jambo la kuogofya. Inaeleza kuwa mwanya wa vipato unaokihirisha ni ule uliojizingira kwenye mifumo ya uchumi na kwamba nchi maskini ziko kwenye utelezi zaidi kwenye hali hii hasa zinapojaribu kudhibiti mfumuko wa bei.

Rais wa Benki ya Dunia, David Malpas anazilaumu nchi zilizoendelea katika kuchagiza mwanya huu wa vipato katika kipindi hiki zinapokabiliana na mfumuko wa bei.

Wakati nchi nyingi zilizoendelea kama Marekani zikitarajiwa kuongeza viwango vya riba ili kudhibiti kuongezeka kwa gharama za bidhaa, Malpas anatahadharisha kuwa gharama kubwa za mikopo zinaweza kuathiri nchi zenye uchumi dhaifu.

Athari za uongezaji viwango vya riba ni bayana kwa watu wanaohitaji pesa kwa ajili ya shughuli za haraka za kuanzisha biashara mpya, biashara za akina mama na biashara kwenye nchi zinazoendelea.

Katika hili la mfumuko wa bei, lililo wazi ni kuwa umetanda duniani kote iwe Rio de Jeneiro kule Brazil; Dodoma, Beijing (China), Washington (Marekani) hadi London nchini Uingereza.

Katikati ya mtanziko huu ni kwamba kila taifa lina jukumu la kulinda uchumi wake, kuhakikisha raia wake wanaishi vema na kuimarisha masuala ya kijamii na kisiasa.

Matokeo muhimu kwenye hili ni kuwa na raia wanaostawi kwa kutumia njia za kiuchumi zinazofanya kazi kwa wengi. Na hapa ndipo penye utofauti.

Hapa nyumbani gharama za bidhaa zinaongezeka, watu tunalia na kusaga meno.

Mwanafunzi wangu mmoja aliniuliza; “kwa nini mamlaka hapa nchini zinajidhatiti sana kudhibiti mfumuko wa bei kwenye takwimu wakati kuna ongezeko kubwa la gharama za bidhaa na huduma kila kukicha?

Mwanafunzi huyu alikuwa ameona taarifa ya Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) mapema wiki hii iliyobainisha kuwa kasi ya mfumuko wa bei kwa mwaka ulioshia Desemba 2021 ulikuwa asilimia 4.2 ikilinganishwa na asilimia 4.1 iliyorekodiwa Novemba 2021.

Kiwango hicho ni cha juu kabisa kuwahi kurekodiwa kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita. Aidha, taarifa hiyo inaonesha kuwa bado kiwango hicho kipo ndani ya mpango wa Serikali wa chini ya asilimia 5.

 

Walaji hupata wanachostahili?

Hapa kuna jambo la kufikirisha. Tumeaminishwa kwa muda mrefu na taasisi kama IMF, Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Wizara ya Fedha na NBS kuwa mfumuko wa bei umedhibitiwa chini ya asilimia 5. Kiwango cha wastani kinachopigiwa chapuo ni kile cha mwaka 2018 cha asilimia 3.4.

Ukilinganisha na nchi ilipokuwa mwanzoni mwa miaka ya tisini (1990’s) wakati mfumuko wa bei rasmi ukiwa kwenye tarakimu mbili, na hivi karibuni kati ya mwaka 2006 na mwaka 2013, kiwango cha sasa kinaonekana kuridhisha mno.

Hata hivyo, ukiweka kiwango hiki cha mkakati wa muda mfupi cha Serikali kwa muda mrefu kila kitu kinabadilika na unaweza kupatwa na mizigizigi kwenye roho yako.

Kwa mtazamo wangu ukweli ni kwamba kuna wakati tunatengenezewa kimya kimya mazingira ya kuamini kuwa mfumuko wa bei ni himilivu na tunapata thamani halisi ya pesa yetu. Nafikiri hata wajuzi wetu wengi ndani ya IMF, BOT, NBS au Wizara ya Fedha nao wanaingizwa kwenye boksi hili.

Tunatakiwa kuanza kutazama suala la mfumuko wa bei kwa njia hii; Kiwango cha mfumuko wa bei cha asilimia 3.4 kwa mwaka maana yake ni asilimia 34 kwa muongo mmoja, au asilimia 102 kwa miongo mitatu.

Lakini kimsingi wastani wa mfumuko kwa mwaka huenda ni zaidi ya huo. Hii ni moja ya sababu ya kwa nini Watanzania wanahisi kuwa gharama zao za maisha zimeongezeka.

Aidha, sababu nyingine inafikirisha zaidi. Badala ya kampuni kuongeza bei za bidhaa kwa ajili ya kuhimili ongezeko la mfumuko wa bei kwa muda mrefu, kampuni hizi zimebuni mbinu ya kuwapa wateja wake kiwango kidogo cha bidhaa kwa bei ile ile au kubwa zaidi. Mfano hai ni ule wa vinywaji baridi.

Ujazo wa soda umepunguzwa kutoka chupa ya mililita 500 mpaka mililita 350 ili kucheza na saikolojia ya wanywaji.

Mfumuko wa bei wa kimya kimya (Silent Inflation)

Wiki iliyopita, nikiwa kwenye mjadala wa WANAZUONI kwenye Club House ambao ulikuwa unahusu deni la Taifa niligusia kidogo hii “silent inflation” ama mfumuko wa bei wa kimyakimya.

Rafiki yangu mmoja mchumi alionesha kushangaa lakini walau akakiri kuwa hafahamu kitu kama kama hicho. Nikiwa kwenye mjadala mwingine, mtu mwingine alieleza kuwa naye ni mchumi pia alinishambulia kuwa nilisema “silent inflation” na kuwa sifahamu ninachosema.

Tofauti na rafiki yangu aliyekiri kutokufahamu, huyu “alijivisha ujinga” kuwa hakipo. Wachumi wetu silent inflation ipo na mantiki yake ni kuwahadaa wanywaji wa soda kuwa bei haijabadilika sana.

Kwa mfano, pesa ambayo inanunua soda ya mililita 350 leo, ingeweza kununua nusu lita (mililta 500) miaka kumi iliyopita.

Kwa maoni yangu, unapojumuisha hatua za kupunguza gharama, utagundua kuwa kiwango cha mfumuko wa bei huenda ni kikubwa kuliko wanachosema NBS. Hiki ndicho wachumi hukiita ‘silent inflation’.

Kupitia aina hii ya mfumuko wa bei, watu huitazama hali ya wakati uliopo na kusahau athari za muda mrefu jambo ambalo muda mwingine linaweza kutumika kuficha ukweli.

Muhimu kufahamu ni kuwa mfumuko wa bei wa kimya kimya haupo tu kwenye nchi zinazoendelea kama Tanzania. Profesa wa Uchumi wa Mienendo ya Binadamu (Behavioral Economics) na mshindi wa tuzo ya Nobel ya Uchumi mwaka 2013 kutoka Chuo Kikuu cha Yale (Marekani), Robert Shiller aliandika makala mwaka 2018 iliyoifungua dunia kuhusu jambo hilo.

Kabla ya makala yake, wengi walifikiri kuwa mfumuko wa bei kwenye nchi zilizoendelea kama Marekani, Sweden, Korea Kusini au Japan siyo kitu cha maana kwenye uchumi mpana. Hivi sasa, kwenye nchi hizi malengo ya mfumuko wa bei kwa serikali ni asilimia 2.

Hapa Tanzania, malengo ya Banki Kuu ni usizidi asilimia 5 kwa muda wa kati. Lakini hii hali ni ya hatari kwa uchumi wa watu na mara kadhaa nimeandika kuwa BoT inahitaji kubadili majukumu yake siku zijazo.

 

Namna BoT inavyoweza kuchochea uchumi zaidi

Kwa muda sasa, magavana wa BOT wameifanya benki hii kuwa mdhibiti wa mfumuko wa bei (inflation targeter). Watumishi wanaohusika huueleza umma kuwa na mfumuko wa bei chini ya malengo ya ya asilimia 5 huleta matokeo mengine bora ya kiuchumi. Lakini hoja hii inakinzana na baadhi ya tafiti na hasa juu ya hali ya mambo hapa Tanzania.

Ushahidi wa kitafiti unaonesha kuwa nchi zilitengeneza uchumi unaozalisha ajira kuanzia Marekani mpaka Ujerumani, Japan, Italia, Korea Kusini mpaka Sweden, benki kuu zao zilielekeza mikopo kwenye kuendeleza viwanda na wafanyabiashara wadogo wakati wa ukuaji wa viwanda.

Kama nilivyowahi kuandika hapo awali, benki kuu ipeleke au ishawishi mikopo kuelekea kwenye sekta ya viwanda na hasa kwenye kuchochea tija kwenye kilimo kwa kutoa ruzuku kwenye teknolojia mpya, kuzuia upotevu wa mazao baada ya mavuno, kuongeza thamani. Ni kwa sababu madirisha ya kilimo yaliyopo kwenye banki zetu hayawezi kufanya zaidi ya yalipofikia.

Muelekeo wetu wa kiuchumi uwe wa kuwekeza kwenye rasilimali watu (elimu na ujuzi), kurekebisha sera yetu ya mkakati wa viwanda, kuratibu uchumi na kushughulika na nidhamu kwenye pesa ya umma.

Nafahamu kuwa kuna mikakati “kufungua uchumi” kuanzia kwenye kuongeza thamani kwenye kilimo, utalii na kwenye sekta ya ngozi.

Ila nina maswali kidogo yakiwemo ni vigezo vipi vimetumika kwenye uchaguzi wa vipaumbele? Vigezo hivi vina ushahidi kiasi gani wa kitafiti? Kama ushahidi upo, ni kwa jinsi gani sekta hizi zitafunguka na kuendelezwa zikiwa zinaongeza uzalishaji na ajira?

Nani anafanya nini serikalini, kwenye sekta binafsi, taasisi za kiraia, wananchi na “wabia wa maendeleo”?

Haya ni masuala ambayo mijadala yetu ya kiuchumi ndani na nje ya Serikali inabidi kuyajibu. Siyo kuyajibu kwa kuwa huwa tunayajibu, tutajibu kwa kuyajibu kweli.

Lakini muhimu kwa yote kwa sasa ni kuchukua hatua za dharura kuwalinda wananchi dhidi ya huu mfumuko wa bei wa kimya kimya ambao nimeueleza vema hapo juu.

Dk Bravious Kahozya ni mtaalamu wa uchumi. Haya ni maoni yake binafsi wala si msimamo wa Nukta Habari. Anapatikana Twitter kupitia @BraviousKahyoza au tuma barua pepe kwenda newsroom@nukta.co.tz.

Enable Notifications OK No thanks