Vita mbichi: Wakazi wa Pangani wanavyohamasishana kupata chanjo ya Uviko-19

May 16, 2022 1:06 pm · Nuzulack Dausen
Share
Tweet
Copy Link
  • Baadhi wasema watu wasisubiri kuambiwa kwenye mambo yanayohusu uhai.
  • Asilimia 13 ya Watanzania wapata chanjo ya Uviko-19.

Pangani, Tanga. Mara baada ya habari za ujio wa chanjo ya ugonjwa wa virusi vya korona (Uviko-19) kusambaa nchini, yeye hakutaka kabisa kusikia wala kuchomwa licha ya kuwa ni mzee. 

Habari za uzushi zilizokuwa zikitolewa na baadhi ya watu ambao hawakuwa na uelewa kuhusu kinga hiyo zilimuopesha zaidi. 

“Walikuja vijana (watoa huduma ya chanjo) hapa, wakaniambia bibi haya njoo tukupatie chanjo nikawaambia miye mzee mkanipige masindano yenu makali hata sitaki,” anasema Mwasi Yusuf mkazi wa kijiji cha Bushiri wilayani Pangani. 

“Lakini wakaniambia bibi hakuna tatizo lolote litakalokupata ukichoma chanjo kwa kuwa hii itakuepusha na ugonjwa, nikakakubali,” anasema bibi huyo mwenye miaka 80. 

Bibi huyo ni miongoni mwa wazee waliopata chanjo ya Uviko-19 wilayani Pangani wanaoshuhudia kuwa hadi sasa hakuna madhara waliyopata na wanaamini wamesalimika baada ya kuipata kinga hiyo. 

Chanjo ya Uviko-19 ni moja ya afua muhimu za kukabiliana na maradhi hayo yanayozidi kuangamiza mamilioni ya watu ulimwenguni sanjari na kunawa mara kwa mara na sabuni na maji tiririka, kuvaa barakoa na kutokaribiana kwa angalau mita moja. 

Mkazi wa Pangani katika Kijiji cha Mwera, Khadija Mkumbukwa akihojiwa na mwandishi wa habari kutoka Nukta kuhusu ugonjwa wa Uviko-19 na anavyochukua hatua kujikinga na ugonjwa huo Februari 15, 2022. Picha| Benezeth Kahwa.

Uviko-19 wazidi kuua watu duniani

Hadi Mei 13, Shirika la Afya Duniani (WHO) linaeleza kuwa watu milioni 517.64 wameripotiwa kuambukizwa Uviko-19 tangu ulipogundulika mwishoni mwaka 2019 huku watu milioni 6.26 wakipoteza maisha.

Nchini Tanzania jumla ya watu 33,928 wameripotiwa kuwa na Uviko-19 tangu Machi 2020 ambao 803 kati yao walipoteza maisha kutokana na maradhi hayo. 

Ujio wa chanjo ya maradhi hayo umesaidia zaidi kupunguza wagonjwa wapya licha ya kirusi hicho kujibadili katika anuai tofauti tofauti ikiwemo Omicron ambayo ilijipenyeza Tanzania pia. 

Wazee ni miongoni mwa makundi yaliyopo hatarini zaidi kuathiriwa na ugonjwa huo ulioingia Tanzania Machi 2020. 

“Mimi nimepata chanjo ndugu yangu. Nawashauri wazee wanzangu wapige chanjo ili tupate huo uzima,” anasema bibi Mwasi huku akiongeza habari zaidi za Uviko-19 alikuwa akisikia kwenye redio na hajawahi kuugua. 

Nje kidogo ya mji wa Pangani katika Kijiji cha Mwera, Khadija Mkumbukwa (70) anaendelea na shughuli zake lakini tofauti na Mwasi, yeye hajachanja chanjo ya Uviko-19 kwa kuwa wakati wa kampeni ya kuchanja hakuwepo nyumbani. 

“Walipokuwa wamekuja hao watu wa kuchanja sikuwepo,” anasema Mwasi. Hata alipoulizwa iwapo aliwajulisha wahudumu wa afya kuwa anahitaji chanjo Mwasi anasema “niseme ukweli tu kuwa sikuwajulisha.”

Pamoja na kuwa hadi sasa hajapata chanjo hiyo, Khadija anasema yupo tayari kupata kinga hiyo muhimu kwa afya yake.

“Kama chanjo itakuwepo nikiambiwa chanja, nitachanja. Hii ni kinga maalum tumeletewa. Huwezi kukataa kuhudumiwa,” anasema Khadija akieleza kuwa kwa hali yake ni vigumu hata kupiga simu kuomba huduma ya chanjo. 


Soma zaidi: 


Bibi huyo anasema ni vigumu kupata taarifa mara kwa mara kwa kuwa hana redio na simu anaitumia kwa ajili ya kupokea simu na iwapo anatumiwa meseji huomba msaada wa kusomewa kwa kuwa hawezi tena kusoma. 

“Haya mambo ya korona yanakupasa uwe na redio ndiyo unaelewa vizuri lakini hizi simu, aah,” anasema Mwasi akionyesha kutofurahia kutumia simu mara kwa mara kupata taarifa za maendeleo na masuala ya Uviko-19. 

Baadhi ya wakazi wa Pangani kwa kushirikiana na wahudumu wa afya, viongozi wa Serikali na asasi za kiraia wanahamasisha wenzao kupata chanjo ya Uviko-19 pamoja na baadhi kuanza kujisahau kuwa “ugonjwa umetoweka.”

Wananchi wajitolea kuhamasisha wengine

Majuto Rashid (68), Mkazi wa Kijiji cha Mwera anasema watu wanapaswa kujilinda kwa magonjwa yote na korona tu na wasisubiri kuambiwa kila kitu. 

“Korona ipo, Ukimwi upo, jilinde mwenyewe usingoje kuambiwa kwa sababu vyombo vya habari vilishakuambia uende kupata chanjo,” anasemaRashid.

“Ukifa kwa kupuuzia korona wao Serikali hata hawaji pale lakini kwenye familia yako umeshaacha pengo ndiyo maana sisi tunahamasisha wengine waende wakachanjwe…mbona tangu tuzaliwe tumechanja chanjo kibao hatujafa,” anasema Rashid ambaye alikuwa miongoni mwa watu wa mwanzo kuchanja na familia yako. 

                       

Viongozi wa serikali za mitaa katika eneo hili waliiambia Nukta Habari (www.nukta.co.tz) kuwa hadi sasa wapo watu wanaojitokeza kupata chanjo hiyo wakati uhamasishaji ukiendelea.

“Wapo waliojitokeza sasa wakitaka kupata chanjo hiyo ya Uviko-19 lakini waliombwa wasubiri kidogo kwa kuwa ilikuwa imekosekana pale zahanati na wapo wanaosubiria kupata dozi ya pili,” anasema Mwinyimkuu Sultan, Afisa Mtendaji wa Kata ya Bushiri.  

Sultan anasema wanaendelea kuwahamasisha wakazi wao kuchukua tahadhari dhidi ya Uviko-19 japo wapo wachache wanaoupuuza wakiamini ugonjwa huo umeshaisha. 

Watu milioni 4 wapata chanjo Tanzania

Katika mapambano ya maradhi hayo Tanzania imeendelea kutoa chanjo ya Uviko-19 ambapo hadi Mei 4 takwimu za Wizara ya Afya zinabainisha kuwa watu takriban milioni 4 sawa na asilimia 13 ya watu milioni 30.74 wenye umri wa miaka 18 na kuendelea walikuwa wamepata dozi kamili. 

Hata hivyo, idadi hiyo ya watu ni ndogo ikizingatiwa imesalia miezi miwili tu kutimiza mwaka mmoja tangu Tanzania ianze kutoa huduma ya chanjo ya Uviko-19 mapema Agosti 2021. 

 “Katika mwezi Aprili 2022 kumekuwa na ongezeko la wagonjwa kutoka watu wanane wiki ya tatu hadi 32 wiki ya nne. Hakuna kifo chochote kilichotolewa taarifa katika cha Aprili hadi Mei, 4 2022,” alieleza Mganga Mkuu wa Serikali Dk Aifello Sichalwe kwenye taarifa ya mwenendo wa Uviko-19 iliyotolewa Mei, 7. 

Pamoja na visa kuongeza katika wiki ya nne ya Aprili, Dk Sichalwe alieleza kuwa bado idadi ya visa vipya imekuwa ikipungua kutoka 116 kwa mwezi Machi 2022 hadi 68 katika mwezi Aprili, 2022.

Siku za hivi karibuni baadhi ya watu wamekuwa wakipuuza kufuata masharti na taratibu zilizowekwa kukabiliana na Uviko-19 licha ya WHO kuripoti ongezeko la virusi katika baadhi ya mabara ikiwemo Afrika. 


Tangazo:


Serikali yataka watu wasipuuze Uviko-19

Hivi karibuni China iliweka zuio la kutoka nje (lockdowns) kwa baadhi ya majiji ya Shanghai na Beijing kukabiliana na ongezeko la kasi la wagonjwa katika robo ya kwanza ya mwaka huu. 

Majiji hayo ni injini ya ukuaji wa uchumi wa China na maradhi hayo kwa mara ya kwanza yaliripotiwa katika taifa hilo la mashariki mwa Asia lenye watu zaidi bilioni 1.41 kwa mujibu wa Benki ya Dunia. 

Licha ya kuwa visa vinapungua siku hadi siku nchini Tanzania, Serikali inawataka watu ambao hawajachanjwa kupata chanjo ili kuzuia ugonjwa mkali na vifo pale mtu atakapopata maambukizi hasa pale visa vitakapoongezeka kwenye jamii. 

“Wizara inaendelea kutoa tahadhari kwa wananchi wote kuendelea kuchukua hatua za kujikinga na kuzuia ugonjwa wa Uviko-19 ikiwa ni pamoja na kupata kwa wakati dozi kamili ya chanjo ya kujikinga ugonjwa huu, kuepuka mikusanyiko isiyo ya lazima na kuvaa barakoa kwa usahihi kwenye mikusanyiko,” alisisitiza daktari huyo. 

Enable Notifications OK No thanks