Wanaoishi na VVU ‘wajikongoja’ kupata chanjo ya Uviko-19 Njombe
- Kasi yao kupata chanjo bado hairidhishi.
- Wasema wakipata elimu na kuhakikishiwa usalama watachanja.
- Serikali, wadau waendelea kutoa hamasa ya chanjo.
Njombe. “Baada ya kuchanjwa nilipata shida sana, siyo shida ya mwili lakini maneno niliyokuwa naambiwa na watu wanaonizunguka yalikuwa yananipa stress (msongo wa mawazo),” anaeleza Atu Nyamike anayeishi na virusi vya Ukimwi (VVU) kwa miaka 10 sasa.
Atu (37) ni mmoja kati ya watu wachache waliokubali kupokea chanjo ya Corona (Uviko-19) katika Halmashauri ya Wilaya ya Makete mkoani Njombe.
Mwanamke huyo anayeishi kata ya Tandala wilayani humo alishutumiwa na wenzake kwanini amekubali kuchanjwa kwa kile wanachodai kuwa ‘ina madhara ya kiafya’.
Hata hivyo, dhana hizo walizona watu hao hazina ukweli wowote kwa sababu wataalam wa afya wanasema chanjo hiyo ni salama na imefanyiwa utafiti wa kisayansi.
Anasema hana hofu kabisa na chanjo kwani maneno ya watu huwa hayaishi kwa sababu hata alivyoanza kutumia dawa za kupunguza makali ya VVU watu walisema maneno mengi wakimwambia atavimba mwili na mengineyo, lakini mwaka mmoja sasa anatumia dawa hizo na hajapata madhara yoyote.
Atu, mfanyabiashara mdogo anayemiliki genge siyo tu amekubali kuchanjwa lakini ameendelea kuchukua tahadhari dhidi ya Uviko-19 ikiwemo kunawa mikono kwa maji tiririka, kuvaa barakoa na kuepuka mikusanyiko isiyo ya lazima.
Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), watu wanaoishi na maambukizi ya VVU ni moja kati ya makundi yaliyo hatarini kupata maambukizi ya virusi vya Uviko-19 na hivyo kuhimizwa kupata chanjo ili kuwaongezea kingamwili.
Wakati WHO na Serikali ya Tanzania ikihimiza watu hawa kupata chanjo mapema, hali imekua tofauti katika Halmashauri ya Wilaya ya Makete kwa sababu muitikio wa watu kupata chanjo siyo wa kuridhisha.
Atu Nyamike akionyesha cheti chake baada ya kupata chanjo ya Corona aina ya Johnson&Johnson. Picha| Imani Henrick.
Kiongozi wa vikundi vitatu vya watu wanaoishi na VVU kata ya Tandala, Constansia Chengula anasema kati ya wanachama 42 wa vikundi hivyo ni mwanachama mmoja tu ndiye aliyechanjwa chanjo.
Licha ya kupata elimu ya kujikinga na Uviko-19 lakini wanakikundi hao wamekuwa ‘wazito’ kupata chanjo, jambo linalowaweka katika hatari ya kuambukizwa na ugonjwa huo kirahisi.
“Sijachanja kwa sababu naogopa. Pia process (mchakato) ni ndefu sana, kwenda kwa mtendaji kujiandikisha na kujaza fomu. Sijapata elimu ya kutosha kuhusu chanjo na elimu niliyoipata ni kutoka kwenye kikundi ila bado nahitaji elimu zaidi.
“Kingine kinachoniogopesha ni kwenye zile fomu za kujaza tunaambiwa chochote kitakachokupata wao hawahusiki, sasa hapo nitafanyaje? Nikipata elimu zaidi na nikaridhika naweza nikachanja,” anasema Grace Mlowe, mmoja wa wanachama wanaoishi na VVU kata ya Tandala.
Grace ambaye ni mama lishe anasema licha ya kuwa hajachanjwa lakini anazingatia tahadhari zote za ugonjwa huo ikiwemo kuvaa barakoa wakati akiendelea na shughuli za kuhudumia wateja katika biashara yake.
Mwanamke huyo anaungana mwenzake Zabron Mbilinyi anayesema hawezi kuchanja kwa sababu anafuata hatua zote za kujikinga na Corona kama kunawa mikono na kuvaa barakoa.
“Tumepewa elimu kuhusu chanjo, lakini mimi nilishapewa chanjo wakati nazaliwa sasa hizi chanjo nyingine za mara ya pili mimi sizielewi. Mimi naendelea kutumia dawa za kupunguza makali ya VVU kama nilivyoelekezwa hospitali na niko safi kabisa, sina shida yoyote ya kiafya,” anasema Mbilinyi ambaye ameishi na VVU kwa zaidi ya miaka 10.

Tatizo ni kubwa zaidi
Nukta Habari (www.nukta.co.tz) ilitembelea Hospitali ya Ikonda ambayo ni moja ya kituo cha kutolea chanjo wilayani Makete ili kufahamu mwenendo wa watu wenye VVU kuchanja chanjo.
Kwa mujibu wa Mkuu wa kitengo maalumu cha kuhudumia watu wanaoishi na maambukizi ya VVU, Dora Mwasa, kituo hicho kinahudumia wanachama 2,280 wenye VVU wilayani humo.
Hata hivyo, Mwasa anasema kati ya wenye maambukizi hayo wanaowahudumia hospitalini hapo, ni watu 42 tu ndiyo wamejitokeza kupata chanjo ya Uviko-19 hadi kufikia Oktoba 21, 2021.
“Tunawahimiza kuchukua tahadhari zaidi wanapokuja maeneo yenye mikusanyiko kama hapa hospitali ambapo kuna magonjwa ya kila aina na ukizingatia kinga zao ni ndogo, ingawa hatuwalazimishi kuchanja anayetaka kuchanja basi anachanja kutokana na jinsi alivyopokea elimu,” anasema Mwasa.
Hali hiyo haitofautiana na watu wa kawaida. Nao mwamko wao bado siyo wa kuridhisha kwa sababu hospitali hiyo ilipokea dozi za chanjo 600 lakini mpaka Septemba 13 walikuwa wamechanja watu 233 tu sawa na asilimia 22.5.
Baadhi ya wanachi wa Wilaya ya Makete wakiendelea na shughuli za kijamii na mazungumzo baada ya kuongea na Nukta Habari hivi karibuni. Picha| Imani Henrick.
Nini kinafanyika kuongeza kasi ya kuchanja?
Mratibu wa huduma za chanjo katika Hospitali ya Ikonda, Wema Pandakilima anasema licha idadi ndogo ya watu wanaojitokeza kupata chanjo, wanaendelea kutoa elimu ili kuwahamasisha kuchanja na kujikinga.
Pia wanatumia fursa ya watu wanaokwenda kutibiwa hospitalini hapo kuwatangazia ili wapate hamasa ya kuchanjwa.
“Kwa sasa tumeanza mkakati wa kufanya mikutano ya hadhara kuelimisha juu ya elimu ya chanjo na tumeanza na kijiji cha Usagatikwa, pia tunawatumia viongozi wa kijiji na madiwani watusaidie kupita kila nyumba kuhamasisha juu ya elimu.
“Microphones (vipaza sauti) zinatatangaza kila siku hapa hospitali kuhamasisha kuchanja,” anasema Pandakilima.
Innocent Grant, Afisa Miradi kutoka taasisi ya Young and Alive Initiative inayojihusisha na elimu ya afya ya uzazi na maabukizi ya VVU wilayani Makete anasema wanaendelea kufanya semina na warsha kuwaelimisha watu kwenda kuchanjwa.
Grant anapendekeza viongozi wa dini na mila washirikishwe kutoa elimu ya chanjo kwa wananchi ili waamke na kuwa tayari kuchanjwa.
Aidha, anabainisha kuwa tatizo kubwa linalosababisha wananchi kutokua na mwitiko katika chanjo ni usambazaji wa habari za uzushi wilayani humo, jambo ambalo wamekuwa wakitumia majukwaa yao kuzikanusha.
Licha ya kuhamasisha chanjo ya Uviko-19, Mratibu wa chanjo Mkoa wa Njombe, Linda Chatilla anasema wanaendelea kutoka elimu kwa watu kujikinga na ugonjwa huo kwa kuvaa barakoa, kunawa mikono na kuepuka mikusanyiko isiyo ya lazima.
“Tunaendelea kufanya uhamasishaji kwa kushirikisha wadau mbalimbali kama viongozi wa dini, wanahabari, viongozi wa siasa na watendaji ngazi mbalimbali,” anasema Chatilla.
Makala hii imefadhiliwa na Shirika la maendeleo ya habari la International Media Support (IMS) na Umoja wa Ulaya (EU).

Latest