Matamasha ya muziki chachu ya kuongeza utoaji chanjo ya Uviko-19 Tanzania
- Ni moja ya sehemu ya kutoa elimu ya umuhimu wa chanjo hiyo kiurahisi.
- Halmashauri ya Mji wa Njombe watumia tamasha hilo kukamilisha lengo.
- Vijana wamekuwa mstari wa mbele kuchomwa chanjo ya Uviko-19.
Dar es Salaam/Njombe. Katika moja ya viwanja Njombe mjini, kundi kubwa la watu limejitokeza kushuhudia wasanii mashuhuri wa muziki Tanzania. Licha ya kuwa ni asubuhi, uwanja umeshajaa hapa.
Wapo baadhi waliosafiri umbali mrefu kushiriki tamasha hili kubwa la muziki kuwashuhudia wasanii hao wakiwemo Marioo, Young Lunya na Whozu.
Hata hivyo, lengo la tamasha hilo lijulikanalo kama “Muziki Mnene” si burudani pekee. Nyuma ya tamasha hilo ni kuhamasisha watu kujitokeza kwa wingi kuchanja chanjo ya Uviko-19.
Kwa zaidi ya mwaka mmoja sasa Serikali ya Tanzania imekuwa ikihamasisha watu wenye umri wa miaka 18 na zaidi kujitokeza kuchanja kuwakinga dhidi ya Uviko-19 ambao umezimisha maisha ya watu 841 nchini tangu kisa cha kwanza kiripotiwe katikati mwa Machi mwaka 2020.
Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO) hadi kufikia Semptemba 01, 2022 jumla ya watu milioni 600.5 wameripotiwa kuugua ugonjwa huo duniani huku watu milioni 6.4 wakipoteza maisha.
Agosti 13, 2022, Halmashauri ya Mji wa Njombe ilifanya tamasha kubwa la mziki mnene kuhamasisha wananchi kuchoma chanjo ya Uviko-19.
Wananchi wajitokeza kuchanjwa
Baadhi ya washiriki katika tamasha hilo walieleza kuwa walihamasika kwenda kuchanja baada ya tamasha hilo lilofanywa na Kituo cha televisheni cha E-TV kwa ushirikiano na Wizara ya Afya ya Tanzania.
“Wananchi tuendelee kuchanja (Chanjo ya Uviko-19) kwa wingi ili kulishinda janga hili la corona”, Patrick Mienzi alikiambia kituo cha televisheni cha E-TV kilichokuwa kinarusha tamasha hilo mubashara.
Kijana aliyetijokeza kuchanjwa katika tamasha la Mziki Mnene, Njombe. Picha| Halmashauri ya Mji wa Njombe.
Matamasha hayo yanasaidia zaidi wadau wa afya kufikia lengo la kutoa kinga ya maradhi hayo kwa kiwango kikubwa ikilinganishwa na njia za kawaida za kumuomba mtu mmoja mmoja kufika katika vituo vya afya kuchanjwa chanjo ya Uviko-19.
“Mimi ni mhamasishaji wa chanjo na tayari nimeshachanja hivyo wengine nao wakaribie kupata chanjo, haina madhara yoyote,” anasema Evodia Mayunga.
Katika tamasha hilo, mamlaka zinaeleza kuwa watu 4,563 walipatiwa chanjo hiyo huku wengi wao wakiwa vijana.
Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Mji wa Njombe, Dk Yesaya Mwasubila aliiambia Nukta Habari kuwa wameendelea kutoa elimu na kuhamasisha watu kuchanjwa chanjo ya Uviko-19 huku lengo lao ni kufikia watu 97,444
“Lengo letu ni kufikia watu 97,444 lakini hadi sasa tumefikia watu 92,046 sawa na asilimia 94 ya lengo ha hili linatokana na utoaji wa elimu na uhamasishaji tunaofanya,” anasema Dk Mwasubila.
Hata hivyo Dk Mwasubila hakutaja ni muda gani watafikia lengo la kuchanja watu hao. Kwa mujibu wa Wizara ya Afya Tanzania inatarajia kuchanja takribani watu milioni 21.5 ifikapo Disemba 2022.
Mbali na kutumia matamasha ya muziki mtaalamu huyo wa afya anasema watoa huduma za afya ngazi ya jamii wameendelea kupita mtaa kwa mtaa na kijiji kwa kijiji kutoa elimu ya chanjo ya Uviko-19.
Kasi ya utoaji chanjo ya Uviko-19 Tanzania katika baadhi ya maeneo hairidhishi licha ya kuwepo kampeni tangu mwishoni mwa Julai 2021.
Soma zaidi:
Mkoani Njombe, ziara za viongozi kama mkuu wa wilaya na wabunge zimekuwa zikitumika pia katika uhamasishaji wa chanjo.
“Watu sasa wanamwitikio mkubwa hofu imewatoka kwa sababu wamepata elimu ya kuchoma chanjo hii ya Uviko-19,” anasema Dk Mwasubila.
Tamasha la Mziki Mnene lilianzia katika mkoa wa Tanga na limelenga kupita kwenye mikoa mbalimbali kwa lengo la kuhamasisha watu kuchanja chanjo ya Uviko-19.
Hii si mara ya kwanza matamasha kama haya kufanyika
Hii si mara ya kwanza mamlaka zinatumia matamasha ya muziki kuhamasisha kukabiliana na majanga ya afya.
Katika siku ya mtoto wa Afrika Juni 16, 2022 Umoja wa Mataifa (UN) kwa kushirikiana na baadhi ya wasanii nchini Zimbabwe waliaanda tamasha la muziki mubashara lililofanyika mtandaoni na kutoa ujumbe mbalimbali ya namna ya kukabiliana na Uviko-19.
Kumekuwa na upotoshaji juu ya chanjo ya Uviko-19 jambo ambalo mapema mwaka jana liliwaogopesha baadhi ya watu na kupunguza utayari wa kuchanja hata hivyo imani imeanza kurejea kwa kasi baada ya baadhi ya watu waliochanjwa kutopata madhara yeyote kama ilivyokuwa ikidaiwa.