Matumizi huduma za kibenki mtandaoni yapaa Tanzania, thamani yafikia Sh123 trilioni
- Miamala yaongezeka mara mbili hadi milioni15.5 ndani ya mwaka mmoja.
- Wachambuzi wa uchumi wasema ni hatua nzuri kuelekea uchumi wa kidigitali.
Dar es Salaam. Ili upate huduma za kibenki miaka 10 iliyopita wakazi wa maeneo mengi Tanzania walilazimika wafike kwenye matawi ya benki au mashine za kutolea pesa (ATM), jambo lilogharimu muda na kuhatarisha usalama wa fedha.
Wafanyabiashara walilazimika kubeba maburungutu ya fedha hadi benki huku baadhi wakitembea umbali mrefu kwa kuwa matawi ya benki yalikuwa maeneo ya mijini pekee.
Kwa sasa mambo yamebadilika. Matumizi ya huduma za kibenki kwa njia ya mtandao yanazidi kuongezeka jambo linalorahisha shughuli nyingi za kiuchumi.
Ripoti ya Usimamizi wa sekta ya fedha ya mwaka 2022 inayotolewa na Benki Kuu ya Tanzania (BOT) inaonyesha kuwa matumizi ya huduma za kibenki kwa njia ya mtandao (internet banking) yameongezeka takribani mara mbili ndani ya mwaka mmoja.
Matumizi hayo hupimwa kwa idadi ya miamala ya kifedha inayofanyika kwa njia ya benki kupitia vifaa vilivyounganishwa na mtandao kama simu, kompyuta, kompyuta mpakato na vinginevyo.
Miamala yaongezeka mara mbili
Hadi kufikia Desemba, 2022 miamala ya kibenki milioni 15.5 ilifanyika kupitia mtandao ikilinganishwa na miamala milioni 8.4 iliyofanyika mwaka 2021.
Wakati miamala ya kibenki mtandaoni ikiongezeka, thamani ya huduma hizo pia imepaa zaidi kushinda huduma nyingine za kifedha nchini.

Mwaka 2022 thamani ya miamala hiyo ilikuwa Sh123 trillioni ikilinganishwa na Sh100 trillioni iliyorekodiwa mwaka 2021 ikiwa ni sawa na ongezeko la asilimia 23.
Uchambuzi wa Nukta Habari umebaini kuwa ongezeko la matumizi ya huduma za kibenki mtandaoni yanaenda na kasi ya ongezeko la watumiaji wa intaneti nchini.
Miamala juu, intaneti juu
Kwa mujibu wa takwimu za Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) watumiaji wa intaneti walifikia milioni 31.1 Desemba 2022, idadi iliyoongezeka kutoka watumiaji milioni 29.8 waliokuwepo mwaka 2021.
Hiyo ni sawa na kusema karibu nusu ya watumiaji wa intaneti Tanzania waliokuwepo Desemba 2022 walitumia huduma za kibenki kwa njia ya mtandao.
Kutokana na takwimu hizo kuna matarajio kuwa watumiaji wa huduma za kibenki kwa njia ya mtandao wanaweza kuongezeka zaidi kutokana na watumiaji wa intaneti kuongezeka maradufu kwa mwaka 2023.
TCRA inasema hadi kufikia Juni, 2023 watumiaji wa intaneti Tanzania ni milioni 34 inayotarajiwa kuongezeka zaidi ifikapo Desemba mwaka huu.
Huduma za za kibenki mtandaoni zinakuwezesha kupata taarifa za akaunti yako kwa urahisi na kufanya miamala mbalimbali kwa usalama na kwa urahisi zaidi. Picha|Suits Me.
Thamani ya miamala kwa njia ya simu yashuka
Wakati thamani ya miamala ya huduma za kibenki kwa njia ya mtandao ikiongezeka, thamani ya miamala kwa njia ya simu imeshuka kwa asilimia 0.8.
Mwaka 2021 thamani ya miamala hiyo iliyofanyika kwa njia ya simu za mkononi ilikuwa Sh115.2 trilioni iliyopungua zaidi hadi Sh114.3 trilioni ndani ya kipindi cha mwaka mmoja.
Licha ya kupungua kwa thamani ya miamala inayofanyika kwa njia ya simu bado idadi ya miamala inayofanyika kwa njia hiyo imeongezeka kutoka miamala bilioni 3.1 hadi bilioni 3.5.
Huenda ongezeko hilo la asilimia 13 ni kiashiria kuwa bado idadi kubwa ya watanzania wanatumia huduma za kifedha kwa njia ya simu katika shughuli zao za kila simu.
Njia nyingine zilizotumika zaidi kufanya miamala ya kifedha ni pamoja mashine za kutolea fedha na malipo kwa njia ya kadi iliyokuwa na jumla ya miamala milioni 266.7 kwa mwaka 2022.
Huduma za kibenki kwa njia ya simu mwaka 2022 zilikuwa na jumla ya miamala milioni 91.2 iliyoongezeka kidogo kutoka miamala milioni 71.5 mwaka 2021.
Soma zaidi
-
Kitendawili: Kwa nini ‘ngada’ inalimwa zaidi Tanzania licha ya operesheni kali za dawa za kulevya?
-
Hizi ndio hifadhi tano kubwa za Taifa Tanzania

Safari njema uchumi wa kidijitali
Wataalamu wa uchumi na biashara wanaeleza kuwa kuongezeka kwa matumizi ya huduma za kibenki mtandaoni kunachangiwa na mabadiliko makubwa ya kidijitali na yatachochea ujumuishi wa kifedha kwa Watanzania wengi wakiwemo wa vijijini.
Profesa Omari Mbura, mchambuzi wa masuala ya uchumi na Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) anasema kuongezeka kwa watumiaji wa huduma za kibenki kwa njia ya mtandao kunamaanisha kuwa teknolojia hiyo ni rahisi, nafuu na ni muhimu kwa Watanzania.
“Ni mfumo ambao sasa umezidi kuaminika kwa maana hiyo uwezekano pia wa kukosea kufanya malipo unakuwa mdogo pia…mfano unapolazimika kufanya miamala ya kifedha kwa nchi mbalimbali unajikuta unatamani kutumia ‘internet banking’,” amesema Profesa Mbura huku akibainisha kuwa ni hudumu hiyo ni rahisi na rafiki.
Kuongezeka kwa matumizi ya huduma kibenki kwa njia ya mtandaoni, kwa mujibu wa Prof Mbura, ni kiashiria kizuri kuwa Tanzania inapiga hatua kuufikia uchumi wa kidigitali unaohamasishwa sana na wadau na viongozi wa Serikali.
Miaka ya hivi karibuni Serikali ya awamu ya sita imekuwa iwekeza nguvu nyingi katika kuimarisha miundombinu ya Tehama ikiwemo ya intaneti inakayowezesha kukua kwa uchumi wa kidigitali..
“Serikali ya Awamu ya sita imedhamiria kuwezesha nchi kuelekea katika uchumi wa kidijitali hususani kuhimiza mfumo wa kufanya biashara bila fedha taslimu (cashless economy) ambao unawezeshwa na kuendeshwa na Tehama,” Waziri wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye, alisema bungeni wakati akisoma bajeti ya wizara yake kwa mwaka 2023/2024 mapema Mei mwaka huu.
Naye Rais Samia Suluhu Hassan aliyekuwa akizungumza katika uzinduzi wa mtandao wa kasi ya 5G na mkongo wa Taifa wa baharini wa 2Africa amesema Serikali inafanya jitihada za kukuza uchumi wa Tehama kwa lengo la kukuza uchumi jumuishi wa kidigitali.
Latest