Mikoa mitano yenye ATM chache zaidi Tanzania
- Katavi ndio mkoa wenye idadi ndogo zaidi ya ATM Tanzania ikiwa na mashine saba tu.
- ATM zilizopo Katavi ni chache kuliko zilizopo kutoka Morocco hadi Mwenge jijini Dar es Salaam.
- Wataalamu wa uchumi na fedha waonya kupungua kwa ATM kunaweza kukaathiri jitihada za kuongeza ujumuishi wa kifedha
Dar es Salaam. Wakati baadhi ya watumiaji wa huduma za kifedha wakikimbilia kwenye huduma za kifedha kwa kutumia kiotomotela (ATM ) kupunguza kidogo maumivu ya tozo kwenye miamala ya simu, baadhi ya wakazi hawajawahi kuiona ATM maishani mwao au hulazimika kutembea umbali mrefu kuifuata huduma hiyo kutokana na uchache wa mashine hizo wanapoishi.
Baadhi ya mikoa na wilaya zake zote nchini Tanzania zina ATM zisizozidi 10 ambazo huenda ni chache kuliko mashine zinazopatikana kando kando ya barabara moja au mbili tu za Dar es Salaam kama kutoka Morocco yalipo makao makuu ya kampuni ya mawasiliano ya simu ya Airtel hadi Mwenge.
Ripoti ya Usimamizi wa sekta ya fedha ya mwaka 2021 ya Benki Kuu ya Tanzania (BOT) iliyotolewa Septemba 13, 2022 inaonyesha kuwa idadi ya ATM zinazidi kupungua nchini mwaka hadi mwaka huku mkoa wa Katavi ukishika mkia kwa kuwa na idadi ndogo ya ATM ambazo ni saba tu.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, idadi ya ATM nchini imekuwa ikishuka kwa asilimia tano kutoka mashine 2,158 mwaka 2017 hadi ATM 2,048 mwaka 2021, mwenendo ambao si rafiki sana kwa wanaopenda kutumia mashine hizo kutoa na kuweka fedha.
Katavi wa mwisho kwa idadi ya ATM Tanzania
Takwimu hizo zinaonyesha kuwa mkoa wa Katavi mwaka 2021 ulikuwa na ATM saba tu ambazo zimedumu kwa miaka mitatu baada ya kuongezeka kutoka mashine 5 mwaka 2018.
Mfano, wakazi wa vijiji jirani kama Kawajense na Makanyagio wao hulazimika kutembea kilomita zisizopungua tatu ili kuifikia ATM ya benki ya CRDB kwa ajili ya mahitaji ya huduma za kifedha jambo linalowafanya kutokuwa na mbadala wa kutumia mawakala wa benki na huduma za kifedha za simu.
Idadi ya ATM mkoani humo ni chini ya zile zinazopatikana katika kata tatu za Makumbusho, Kijitonyama na Mikocheni jijini Dar es Salaam.
Mikoa mingine iliyoshika mkia kwenye idadi ya huduma ya ATM ni pamoja na Pemba (Kusini Pemba na Kaskazini Pemba) yenye ATM 11, Simiyu (mashine 12), Rukwa (mashine 15) na Songwe ukiwa na mashine 22.
Benki ya CRDB ilizindua mashine ya kisasa ya kuweka pesa (Depository ATM) yenye teknolojia inayomuwezesha mteja kuweka pesa mwenyewe kwa kiasi cha hadi milioni 100 kwa mara moja. Uwepo wa ATM za kisasa kama hizi zinasaidia kuongeza upatikanaji wa huduma za kifedha na kuongeza ujumuisha katika sekta hizo. Picha|CRDB Bank PLC/Twitter.
Dar es Salaam makao makuu ya ATM Tanzania
Kati ya ATM 2,048 zilizokuwepo Tanzania mwaka 2021, BoT inabainisha kuwa theluthi moja au ATM 683 zilikuwa Dar es Salaam au sawa na asilimia 33.3 ya mashine zote. Hii ina maana kuwa kwa kila ATM tatu zilizopo nchini, moja ipo katika jiji la kibiashara la Dar es Salaam.
Dar es Salaam ndiyo mkoa unaoongoza kwa kuwa na ATM nyingi zaidi Tanzania ukifuatiwa na Mwanza yenye ATM 128, Arusha (128), Dodoma (113) na Kilimanjaro iliyokuwa na ATM 102.
Huenda kupungua kwa mashine za ATM kumechochewa zaidi na kuongezeka kwa upatikanaji wa huduma za kifedha kwa kutumia simu ya mkononi na mawakala wa benki licha ya kuwa miezi ya hivi karibuni zimekuwa na makato makubwa kutokana na tozo kuliko kwenye ATM.
Mapema Jumatatu hii Waziri wa Fedha na Mipango Mwigulu Nchemba alieleza kuwa jopo la wataalamu wa wizara hiyo wameanza mchakato wa kupitia tozo hizo kuleta unafuu kwa wananchi baada ya kupewa maagizo na Rais Samia, Chama cha Mapinduzi (CCM) na kupokea maoni ya watumiaji.
Soma zaidi:
-
Serikali yaeleza sababu za ATM kukosa miundombinu kwa wasioona
-
Mtandao wa 5G wazinduliwa kwa mara ya kwanza Tanzania
Licha ya idadi ya ATM kupungua baadhi ya benki kama CRDB ziliongeza idadi ya miamala kupitia mashine hizo kwa zaidi ya asilimia 10.
Mfano, Ripoti ya mwaka 2021 ya CRDB inabainisha kuwa idadi ya miamala iliyofanywa kwenye ATM iliongezeka kutoka miamala milioni 19 mwaka 2020 hadi miamala milioni 21.4 mwaka jana.
Takwimu hizo mpya za BoT zinabainisha kuwa mawakala wa benki zaidi ya 8,500 walisajiliwa nchini ndani ya mwaka mmoja kutoka mawakala 40,410 mwaka 2020 hadi mawakala 48,923 mwaka jana.
Hata hivyo, kasi ya asilimia 21 ya ongezeko la mawakala wa benki mwaka 2021 ilikuwa ndogo takriban mara mbili kuliko ile iliyorekodiwa kati ya mwaka 2019 na 2020 ambapo idadi ya mawakala iliongezeka kwa asilimia 42.5.
Mawakala wapya 12,052 walisajiliwa mwaka 2020 na kufikia 40,410 kutoka mawakala 28,358 waliokuwepo mwaka 2019.
Mapema Septemba mwaka huu benki ya ABSA ilizindua ATM ya kisasa ambayo mtu anaweza kufanya miamala kwa kutumia msimbo wa QR. Teknolojia kama hii inaongeza ufanisi katika upatikanaji wa huduma za kifedha hata kama kadi ina shida. Picha|Absa Tanzania/Twitter.
Wataalamu waonya upungufu wa ATM
Wachumi na wachambuzi wa sekta ya fedha wanaonya kwamba uchache wa huduma za ATM kwenye baadhi ya mikoa una hatari kubwa ya kupunguza mzunguko wa fedha na kuongeza gharama za huduma hizo kupitia miamala ya simu.
“ATM haina gharama kubwa kwa mtumiaji ukilinganisha na huduma nyingine, kivyovyote vile upungufu huo utawaathiri na kuwaongezea gharama zisizo za lazima,” amesema Dk Sylvester Jotta Mhadhiri wa Uchumi wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agustino kilichopo mkoani Mwanza.
Hata hivyo, Jotta amesema kuna faida nyingi mkoa ukiwa na huduma za kibenki ikiwemo ATM ambazo zinarahisisha upatikanaji wa fedha bila kuhusisha makato makubwa jambo linaloongeza ujumuishi wa huduma za kifedha.
“Huduma za kibenki ndio chombo pekee cha wao pia kuweza kupata huduma mbalimbali za kifedha ikiwemo mikopo ukilinganisha na huduma nyingine za kifedha zenye gharama,” amesema Dk Jotta.
Jotta amezitaka benki kuacha fikra hasi kuwa maeneo yenye wakulima wengi hayahitaji huduma za kisasa za kibenki zikiwemo ATM na matawi au mawakala wenye uwezo wa kutoa mikopo kwa kuwa kila mtu ana haki ya kupata huduma hizo za kifedha.
Nyongeza na Nuzulack Dausen.