Kwa nini ATM zinaongezeka Tanzania?
- Katavi yaendelea kuwa na ATM chache zaidi nchini huku Dar es Salaam ikibaki kinara.
- Wataalamu wasema kuimarika kwa uchumi na kuongezeka kwa faida kutoka kwenye huduma za ATMs kumechochea benki kuwekeza zaidi.
Dar es Salaam. Licha ya kuwepo msukumo wa kuimarisha huduma za fedha za kidijitali, benki za biashara Tanzania zimeongeza uwekezaji katika mashine za kuweka na kutolea fedha (ATMs) baada ya kuongezeka mashine 725 ndani ya miaka miwili.
Ndani ya miaka minne kati ya mwaka 2018 na 2021, kwa mujibu wa Ripoti ya Usimamizi wa Sekta ya Fedha mwaka 2023 iliyotolewa na Benki Kuu ya Tanzania (BoT), idadi ya ATM nchini zilikuwa zikipungua mwaka hadi mwaka huku idadi ya mawakala wa benki na simu pesa ikiongezeka.
Ripoti hiyo inabainisha kuwa idadi ya ATMs imeongezeka kutoka 1,410 mwaka 2021 hadi 2,135 mwaka 2023, ikiwa ni ongezeko kubwa kuwahi kurekodiwa ndani ya miaka sita ya hivi karibuni.
Mwaka 2022 pekee, benki ziliongeza sokoni ATM 501, sawa na ongezeko la takriban asilimia 36% ndani ya mwaka mmoja. Mwaka 2023 taasisi hizo za kifedha ziliongeza ATM nyingine 224 sokoni sawa na ongezeko la asilimia 12, kasi ya ukuaji ambayo ni ndogo mara tatu ya ile iliyorekodiwa mwaka 2022.
Tofauti na miaka hiyo miwili, uchambuzi wa data hizo uliofanywa na Nukta Habari umebainisha kuwa kati ya mwaka 2018 hadi 2021 idadi ya ATMs ilikuwa inashuka kwa kasi ya wastani wa asilimia 2.4 kwa mwaka.
Kiwango cha ATM mpya 224 zilioongezwa mwaka 2023 ni sawa na jumla ya mashine zote zilizokuwepo mwaka huo katika mikoa nane nchini ikiwemo ya Njombe, Rukwa, Ruvuma, Shinyanga, Singida, Songwe, Tabora na Simiyu.
Wataalamu wa uchumi na fedha wanaeleza kuwa hali hiyo inatokana na kukua kwa uchumi, mahitaji ya kuokoa muda, kukua kwa uelewa, ongezeko la watu, biashara na kuongezeka kwa faida katika sekta ya fedha.
ATM bado mtihani Katavi
Baadhi ya mikoa ilirekodi ongezeko kubwa la idadi ya ATM mwaka 2022 ikiwemo Katavi ambayo mwaka 2021 ilikuwa inashika mkia kwa kuwa na mashine sita tu za kutolea fedha mkoa mzima.
Hata hivyo, katika mwaka 2022 idadi ya ATM Katavi iliongezeka zaidi ya mara tatu hadi kufikia mashine 20 na kuipiku rasmi Simiyu iliyorekodi mashine 11 mwaka huo. Mwaka mmoja baadaye, idadi ya ATM Katavi ilishuka hadi mashine 11 na kuwa mkoa wa mwisho tena kwa mashine hizo nchini.
ATM huwasaidia wateja wa benki kutoa fedha taslimu wanapokuwa na mahitaji nazo na umaarufu wake uliongezeka zaidi miaka mitatu iliyopita baada ya Serikali kuweka tozo kwenye miamala ya fedha kwenye simu. Ilikuwa ni ahueni kutoa fedha kwenye ATM kuliko kwa wakala wa benki au simu pesa.
Joseph Iddi, mkazi wa Katavi na mtumiaji wa huduma za kibenki aliimbia Nukta Habari kuwa ATM zimeongezeka mkoani mwao kutokana na kuongezeka kwa shughuli za kiuchumi kulikochochea ongezeko la wafanyabiashara hasa wakulima, wavuvi na wachimbaji wa madini.
Dar yaongoza kwa ATM Tanzania
Wakati Katavi na Simiyu zikijikokota, Dar es Salaam ni kinara wa mashine nyingi za ATM baada ya ripoti ya BoT kuonyesha kuwa ilikuwa na ATM 710 mwaka 2023, ikiwa ni ongezeko la ATM 114 ndani ya mwaka mmoja.
Kwa mwaka 2022, jiji la Dar es Salaam lilifikia rekodi ya mashine 596 za ATM kutoka idadi ya mashine 452 iliyorekodiwa mwaka 2021 kabla ya kupanda zaidi mwaka jana.
CRDB, NMB zaongoza kwa ATM nchini
Uchambuzi zaidi wa data unaonyesha kuwa benki kubwa za biashara za CRDB na NMB zinamiliki karibu theluthi mbili (asilimia 63) za ATM zote nchini, kwa mujibu wa ripoti za mwaka 2023 za benki hizo mbili.
Mwaka 2023 CRDB ilikuwa na ATM 648 zikiwemo za kuweka fedha huku NMB ikiwa na ATM 715 kuifanya kuwa benki yenye mtandao mkubwa zaidi wa ATM Tanzania. ATM 350 au takriban nusu ya mashine za NMB zipo maeneo ya vijijini.
Benki ya CRDB ni miongoni mwa benki zilizowekeza kwenye benki za kuweka fedha (Deposit ATM) kupunguza msongano kwenye matawi na wakala. Picha|CRDB Bank PLC/X.
Hata hivyo, NMB imepunguza idadi za ATM zaidi ya 60 kutoka mashine 781 mwaka 2022 wakati CRDB iliongeza ATM 94 kutoka mashine 554 zilizorekodiwa mwaka 2022.
Ongezeko la ATM limeenda sambamba na ongezeko la miamala inayofanyika kupitia mashine hizo katika baadhi ya benki.
Mwaka 2023 miamala ya NMB kwenye ATM iliongezeka kwa milioni 3.8 au asilimia 8.1 na kufikia miamala milioni 50.6, mara mbili zaidi ya jumla ya miamala iliyofanywa na CRDB kwa mwaka huo huo.
Ripoti ya CDRB inabainisha kuwa miamala ya ATM ilishuka kwa miamala 361,442 na kufikia milioni 24.12 kwa mwaka 2023. Hata hivyo, mwaka mmoja nyuma idadi ya miamala kwenye ATM iliongezeka kwa miamala milioni 3.3 hadi kufikia miamala 24.49 mwaka 2022.
“Miamala ya ATM ilishuka kutokana na kuongezeka kwa miamala katika huduma za kifedha za kidijitali,” inaeleza CRDB kwenye ripoti ya mwaka 2023.
Ulitarajia ukuaji huu wakati uchumi wa kidijitali?
Uwekezaji mkubwa kwenye ATMs miaka miwili iliyopita ni kinyume cha matarajio ya baadhi ya wachambuzi wa uchumi na fedha waliotarajia kuwa idadi ya mashine hizo ingeendelea kupungua kutokana na msukumo wa kujenga uchumi wa matumizi ya fedha mtandaoni (Cashless economy).
Hata hivyo, baadhi ya wachambuzi wameiambia Nukta Habari kuwa uwekezaji mkubwa uliofanywa kwenye ATM si wa bahati mbaya.
Kuna viashiria vikubwa kuwa sekta ya benki imegundua uhitaji mkubwa wa wananchi kutolea pesa taslimu kwenye ATM nchini kutokana na gharama ndogo za kutolea pesa kwenye mashine hizo kuliko mtandaoni.
Iddi anasema hutumia zaidi huduma za simu pesa kuliko benki kwa sababu huduma hizo zinapatikana kwa wingi zaidi katika mkoa wa Katavi.
Wataalamu wa uchumi wa fedha wanasema ongezeko la ATM kwa kiwango kikubwa ni matokeo ya ukuaji wa uchumi na tabia ya wananchi kutaka kupunguza gharama za huduma za kifedha.
Ukuaji uchumi wachangia
Mhadhiri mwandamizi wa uchumi katika Chuo Kikuu Cha Mtakatifu Agustino (SAUT) jijini Mwanza Dk Isaack Safari anasema ongezeko la ATM limechangiwa zaidi na kukua kwa uchumi wa Tanzania kutoka kiwango cha chini hadi kiwango cha kati cha chini.
“Uchumi wa Tanzania kukua katika mtizamo wa Benki ya Dunia (WB) ni kipato kuongezeka, kipato cha mtu mmoja kimeongezeka na karibu tutafikia Dola 1,200 za Marekani…kukua huko maana yake mzunguko wa pesa umeongezeka hivyo watu wanataka uharaka katika ‘transaction’ (miamala) kwa hiyo akienda ATM anamaliza shida yake haraka anaendelea na shughuli zake,” anasema Dk Safari.
Baadhi ya wachambuzi wanasema mwenendo wa kushuka kwa uwekezaji wa ATM katika kipindi cha mwaka 2018-2021 ulitokana na kudorora kwa shughuli za kiuchumi ambazo baadhi ziliathirika na utawala uliokuwepo madarakani.
Wakati huo, Mchambuzi wa masuala ya uchumi Dk Sylvester Jotta anasema biashara nyingi zilifungwa, watu wengi walihamisha mitaji kupeleka nchi nyingine na kusababisha ukwasi kupungua kwa watu pamoja na taasisi za benki.
Dk Jotta ameongeza kuwa jitihada za Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan za kuchochea ukuaji wa sekta binafsi na kutengeneza mazingira bora ya uwekezaji kumechangia kwa kiasi kikubwa kuifungua nchi kiuchumi.
Baadhi ya wataalamu wa fedha na uchumi wanaeleza kuwa ATMs bado ni nafuu na zinahitajika zaidi na watumiaji na zina faida kwa benki husika. Picha|ABSA Bank Tanzania.
Ni faida kwa benki
Hata hivyo, ongezeko la ATM si neema tu kwa watumiaji kwa kuwarahisishia upatikanaji wa huduma ya fedha kwa saa 24, baadhi ya wataalamu wa uchumi wanasema uwekezaji huo umechangiwa na upatikanaji wa faida kwa taasisi za benki.
Profesa Abel Kinyondo, mtaalamu wa uchumi, ameiambia Nukta Habari kuwa ATM zinanufaisha benki zaidi kwa kuwa hupunguza gharama za uendeshaji na kuongeza mapato kupitia makato yatokanayo na watumiaji.
Kwa Prof Kinyondo, ongezeko la ATM ndani ya miaka miwili ya hivi karibuni haliwezi kuathiri jitihada za kuhamasisha matumizi ya fedha mtandaoni kwa kuwa bado maeneo mengi nchini watu wanatumia fedha taslimu (cash) kuliko fedha mtandao.
Anasema matumizi ya ATM yanasaidia kudhibiti utakatishaji wa fedha haramu kwa kuwa ni rahisi kufuatilia na kupata taarifa za mhusika pale anapotiliwa shaka.
Ripoti hii maalum imeandikwa na John Paul na Esau Ng’umbi. Nyongeza na Nuzulack Dausen.