Rais Samia kuongoza mazishi ya Lowassa Februari 17
- Kabla ya mazishi mwili wa Lowassa utaagwa mara tatu, katika viwanja vya Karimjee, KKKT Azania Front na mkoani Arusha.
Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuongoza maelfu ya Watanzania katika mazishi ya Waziri Mkuu mstaafu Edward Ngoyai Lowassa, yatakayofanyika Februari 17, 2024 kijiji kwao Ngarash, Monduli mkoani Arusha.
Lowassa alifariki dunia mchana wa Februari 10, 2024 wakati akiendelea kupatiwa matibabu ya maradhi ya muda mrefu ikiwemo kujikunja utumbo katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) jijini Dar es Salaam.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, aliyekuwa anatoa taarifa rasmi ya Serikali kuhusu mazishi ya kiongozi huyo, Februari 11, 2024 jijini Dar es Salaam alibainisha kuwa mazishi hayo yataratibiwa na kamati ya mazishi ya Serikali na kuongozwa na Rais Samia.
“Siku ya jumamosi familia pamoja na watanzania tutaongozwa na Rais Samia kuupeleka mwili kwenye nyumba ya milele …tunatarajia zoezi hilo litafanyika mapema ili kuruhusu wanaotoka mbali kuweza kusafiri,” amesema Majaliwa.
Kwa mujibu wa Taarifa iliyotolewa na Msemaji Mkuu wa Serikali, ibada ya mazishi ya kiongozi huyo itatanguliwa na shughuli kadhaa ikiwemo maombolezo na kuuaga mwili katika viwanja vya Karimjee, jijini Dar es Salaam Februari 13 mwaka huu.
Soma zaidi:Rais Samia amlilia Waziri Mkuu Mstaafu Edward Lowassa
Taarifa hiyo inafafanua zaidi kuwa watakaohusika katika kuuaga mwili wa kiongozi huyo ni viongozi wa Serikali pamoja na wananchi shughuli itakayoratibiwa na kamati ya mazishi ya Serikali kisha mwili utarudisha nyumbani kwa ajili ya ibada.
Baada ya shughuli hiyo, Februari 14, mwili wa kiongozi huyo utaagwa tena katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Azania Front, kisha kurejeshwa katika hospitali ya Lugalo kabla ya kusafirishwa kuelekea kijijini kwao Monduli mkoani Arusha.
Wakazi wa Kilimanjaro, Arusha kumlaki
Mwili wa kiongozi huyo utawasili katika uwanja wa ndege wa Kilimanjaro alhamisi ya Februari 15 saa nne asubuhi ambapo atasafirishwa tena kuelekea kijijini kwao Monduli.
Akiwa njiani mamia ya wananchi wa mkoa wa Kilimanjaro na Arusha wanatarajiwa kumlaki na baadhi yao kupata nafasi ya kumuaga Ijumaa, Februari 16, kisha kufuatiwa na shughuli za mazishi jumamosi ya Februari 17.
Aidha, Majaliwa amesema familia ya kiongozi huyo itaweka utaratibu utakaowawezesha waombolezaji kutoka maeneo mbalimbali kupata nafasi ya kuaga na kushiriki ibada ya mazishi.