Rais Samia amlilia Waziri Mkuu Mstaafu Edward Lowassa
- Asema taifa limepoteza kiongozi mahiri aliyejitoa kuitumikia nchi yake.
- Alitaka Taifa kuwa pamoja na familia hiyo katika kipindi hiki kigumu.
- Atangaza bendera kupepea nusu mlingoti kwa siku tano za maombolezo.
Dar es Salaam. Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amesema amepokea kwa masikitiko makubwa taarifa ya kifo cha Waziri Mkuu mstaafu, Edward Lowassa ambaye amefariki dunia leo Februari 10, 2024.
Taarifa ya kifo cha Lowassa imetangazwa leo majira ya alasiri na Makamu wa Rais wa Tanzania Dk. Philip Mpango aliyebainisha kuwa kiongozi huyo amefariki wakati akiendelea kupatiwa matibabu ya maradhi ya muda mrefu ikiwemo kujikunja utumbo katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) jijini Dar es Salaam.
Kupitia taarifa yake iliyochapishwa kwenye mitandao ya kijamii, Rais Samia amebainisha kuwa Tanzania imempoteza kiongozi mahiri, aliyejitoa na kuitumikia nchi yake.
“Nimepokea kwa masikitiko makubwa taarifa ya kifo cha Waziri Mkuu mstaafu, Mheshimiwa Edward Ngoyai Lowassa. Mheshimiwa Lowassa ameitumikia nchi yetu katika nafasi mbalimbali kwa zaidi ya miaka 35, akianzia ushiriki wake katika Jeshi la Wananchi wa Tanzania, Chama Cha Mapinduzi (CCM), mbunge, waziri katika wizara mbalimbali na Waziri Mkuu.”
“Tumempoteza kiongozi mahiri, aliyejituma na kujitoa kwa nchi yetu. Natoa pole kwa mjane, Mama Regina Lowassa, watoto (Mheshimiwa Mbunge wa Monduli, Fredrick Lowassa na wadogo zako), ndugu, jamaa, marafiki na Watanzania wote kwa msiba huu mzito,” ameandika Rais Samia kwenye mitandao yake ya kijamii ikiwemo Instagram.
Aidha, Rais Samia ameiambia familia ya kiongozi huyo kuwa kama Taifa lipo pamoja nao katika kipindi hiki kigumu, na kamwe wasiache kumtegemea mwenyezi Mungu na kutafakari neno lake, hasa Kitabu cha Ayubu 1:21.
Sambamba na hilo Rais Samia ametangaza siku tano za maombolezo ambapo bendera zitapepea nusu mlingoti kuanzia leo Februali 10 hadi 15, 2024.
Edward Lowassa ni nani
Edward Lowassa alizaliwa Agosti 26, 1953 katika Kijiji cha Ngarash, Monduli na ndiye mtoto mkubwa wa kiume kwa Mzee Ngoyai Lowassa.
Alianza kusoma katika Shule ya Msingi Monduli kati ya mwaka 1961–1967 na kisha akaendelea kwenye Shule ya Sekondari Arusha kwa kidato cha kwanza mpaka cha nne kati ya mwaka 1968 – 1971, kabla ya kumalizia kidato cha tano na sita katika Shule ya Sekondari Milambo mkoani Tabora mwaka 1972–1973.
Alijiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam mwaka 1974–1977 na kuhitimu Shahada ya Sanaa katika Elimu na baadaye Chuo Kikuu cha Bath, Uingereza kwa Shahada ya Uzamili ya Sayansi katika Maendeleo (mwaka 1983–1984).
Baada ya kumaliza chuo kikuu, Lowassa alifanya kazi ndani ya CCM akiwa ofisa wa ngazi ya juu kuanzia wilaya, mkoa na baadaye makao makuu kati ya mwaka 1977–1989.
Aliajiriwa kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Mikutano ya Kimataifa Arusha (AICC), mwaka 1989–1990.
Lowassa amemuoa Regina na wana watoto watano, wasichana wawili na wavulana watatu. Watoto hao ni Fredrick, Pamella, Adda, Robert na Richard.
Lowassa alichaguliwa kuwa Mbunge wa Monduli mwaka 1990 na 1993 aliteuliwa kuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu na Makamu wa Kwanza wa Rais (Haki na Mambo ya Bunge), kabla ya kuhamishiwa Wizara ya Ardhi na Makazi akiwa Waziri mwaka 1993–1995.
Kwenye Uchaguzi Mkuu wa kwanza wa vyama vingi (mwaka 1995), Lowassa alishinda ubunge kwa asilimia 87.3.
Alikaa bila uteuzi wowote kwa miaka miwili na mwaka 1997–2000, Rais Benjamin Mkapa alimteua kuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira na Kuondoa Umasikini).
Kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2000 aligombea tena ubunge wa Monduli na kushinda kwa mara ya tatu ambapo Rais Mkapa akamteua kuwa Waziri wa Maji na Mifugo hadi mwaka 2005.
Kwenye Uchaguzi Mkuu wa 2005, aligombea ubunge na kushinda kwa asilimia 95.6 ndipo Rais mstaafu wa awamu ya nne Jakaya Kikwete alimteua kuwa Waziri Mkuu wa Tanzania na Bunge likamthibitisha kwa kura 312.
Kukoma kwa Uwaziri Mkuu
Uwaziri mkuu wa Lowassa ulikoma Februari 2008, alipojiuzulu kutokana na kashfa ya Richmond. Kamati Maalumu ya Bunge ya watu watano iliyoongozwa na Dk Harrison Mwakyembe ilisisitiza kuwa Wizara ya Nishati na Madini na Ofisi ya Waziri Mkuu ndizo zinazopaswa kubeba lawama ya uingiaji wa mkataba mbovu na Richmond, kampuni ambayo uchunguzi ulionyesha kuwa ni ya mfukoni mwa watu, huku Serikali ikilazimika kulipa mabilioni ya fedha katika mkataba ambao una upungufu mkubwa.
Wakati Lowassa analitaarifu Bunge kuwa amemuandikia Rais barua ya kujiuzulu, alisisitiza kuwa “…anafanya hivyo ili kulinda taswira ya chama chake na Serikali na kuwa shida ya wabaya wake ni u-waziri mkuu na siyo kingine…”
Baada ya kujiuzulu, Lowassa aligombea ubunge kwa mara nyingine Monduli (mwaka 2010) na kupata asilimia 90.93 ya kura zote.
Lowassa ni miongoni mwa wana-CCM 17 waliochukua fomu kuwania urais mwaka 1995 lakini aliyepitishwa ni Mkapa.
Latest



