Mamia wajitokeza kumzika Lowassa, Rais Samia ahimiza kuyaenzi mema aliyoyaacha
- Azikwa kiheshima kwa taratibu za kiserikali, kidini na kimila.
- Mamia ya wananchi, viongozi wa Serikali wajitokeza kumzika
- Rais Samia asema ameliachia Taifa mambo makubwa matatu.
Dar es Salaam. Hatimaye mwili wa hayati Edward Lowassa umepumzishwa kwenye nyumba yake ya milele katika kijiji cha Ngarashi, wilayani Monduli mkoani Arusha ikiwa ni siku saba tangu apoteze maisha Februari 10 mwaka huu.
Maisha ya Hayati Lowassa aliyewahi kuwa Waziri Mkuu wa Tanzania kati ya mwaka 2005 hadi 2008 yalikatishwa na maradhi ya muda mrefu ikiwemo ya kujikunja kwa utumbo na kuiacha familia na watanzania kwenye majonzi.
Leo Februari 17, 2024 saa 6 mchana mwili wa kiongozi huyo umepumzishwa katika nyumba yake ya milele kwa ibada iliyohudhuriwa na viongozi mbalimbali wa dini, kimila na Serikali akiwemo Rais Samia Suluhu Hassan.
Akizinguza mara baada ya ratiba za mazishi hayo kukamilika Rais Samia amewarai Watanzania kuyaenzi mema yote yaliyoachwa na kiongozi huyo katika ngazi za kijamii, kidini na kisiasa.
“Yamesemwa mengi kumuhusu mpendwa wetu Edward Lowas, tuedelee kumuenzikwa kuyaishi yale mema aliyoyaamini na kuyasimamia,” amesema Rais Samia.

Familia ya Lowassa ikitoa salamu za mwisho kwa mpendwa wao kabla ya mazishi.Picha|Ikulu Mawasiliano.
Aidha, Rais Samia amewaambia waombolezaji kuwa kati ya masomo makubwa mabayo kiongozi huyo ameliachai Taifa ni pamoja na ushupavu, ustahimilivu na ulezi.
“Kwa waliomfahamu Edward Lowasa watakubaliana nami alikuwa mlezi, kiongozi alyelea na kukuza wanasiasa vijana wengi ambao wananendelea kulitumia Taifa…
…Sifa hii ilimjengea umaruufu na mapenzi kwa makubwa miongooni mwa wengi,” amebainisha Rais Samia.
Mbali na Rais Samia, viongozi wengine waliohudhuria ni pamoja na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, Naibu Waziri Mkuu Dotto Biteko, Spika wa Bunge Dk.Tulia Ackson, mawaziri, manaibu waziri, wabunge na viongozi wengine kutoka vyama vya upinzani.
Zinazohusiana:Dk. Mpango aongoza Watanzania kumuaga Lowassa Dar es Salaam
Azikwa kwa heshima
Kama ilivyo katika mazishi ya viongozi nwengine wa Serikali mazishi ya Lowassa yalifanyika katika taratibu za kijeshi ikiwemo kupigiwa saluti na mizinga 17 iliyoashiria heshima kwa kiongozi huyo ambaye pia aliwahi kulitumikia Jeshi la Tanzania katika vita ya Tanzania na Uganda.
Kiongozi huyo pia amezikwa kwa kufuata taratibu za kanisa kwa ibada maalum iliyoongozwa na viongozi wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri (KKKT) kisha kufuatiwa na mazishi ya kimila yaliyoongozwa na Mkuu wa Jamii ya Wamasai Laigwanan Ole kisongo Meijo.
Baada ya taratibu hizo wanafamilia na viongozi wa Serikali walipata nafasi yakutoa heshima zao za mwisho kwa kuweka udongo na taji la maua katika kaburi lake lililosakafiwa kwa viagae vyeussi na kupambwa kwa maua meupe.
Fredrick Lowassa, mtoto wa kwanza wa hayati Lowassa aliyekuwa akizungumza kwa niaba ya familia, amewashukuru wananchi na viongozi wa Serikali kwa kuwa pamoja na familia hiyo tangu wanauguza mpaka baba yao anapoteza maisha.