Serikali: Taratibu mazishi ya Rais Magufuli kujulikana Machi 19
- Msemaji Mkuu wa Serikali adokeza kuwa Makamu wa Rais Mama Samia atalihutumia Taifa muda wowote kuanzia Saa 3:30 asubuhi.
Dar es Salaam. Msemaji Mkuu wa Serikali Dk Hassan Abbasi amesema Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan anatarajia kulihutubia Taifa Ijumaa ya Machi 19 kuhusu taratibu na ratiba nzima ya mazishi ya hayati Dk John Magufuli.
Dk Abbasi ameliambia Shirika la Utangazaji la Taifa (TBC) kuwa leo Alhamis kulikuwa na mfululizo wa vikao vya maandalizi ya mazishi ya Dk Magufuli aliyefariki Machi 17 mwaka huu kwa maradhi ya moyo jijini Dar es Salaam na kwamba ratiba imeshakamilika.
Mama Samia alilieleza Taifa jana kuwa Dk Magufuli alikuwa akipatiwa matibabu katika hospitali ya Mzena iliyopo Dar es Salaam kabla umauti haujamkuta Saa 12 jioni.
“Wananchi wasione leo Serikali ilikuwa kimya tulikuwa kwenye maandalizi hayo, huu ni msiba mkubwa, tumeondokewa na kiongozi mwenye maono, kiongozi mpenda mapinduzi, kiongozi mzalendo, kwa hiyo aina ya maziko ya kiongozi inahitaji sana maandalizi,” amesema Dk Abbasi ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Michezo, Sanaa na Utamaduni.
Soma zaidi:
- Siku ya mwisho Rais Magufuli kuzungumza hadharani
- Rais Magufuli afariki dunia kwa maradhi ya moyo Tanzania
Miongoni mwa vikao vilivyofanyika leo ni kile cha kamati tendaji cha makatibu wakuu na kingine kilichofanyika jioni kikihusisha mawaziri na makatibu wakuu ambao hawapati fursa ya kuingia kwenye kamati tendaji.
“Ratiba imeletwa na kimsingi imekamilika sasa tutarajie wakati wowote kuanzia Saa 3:30 asubuhi Mh Makamu wa Rais atatoa taarifa kwa umma na kwa Taifa kuhusu ratiba na mtiririko mzima wa maziko,” ameeleza Dk Abbasi katika mahojiano na TBC.
Kiongozi huyo amedokeza kuwa shughuli ya mazishi za Dk Magufuli (61) zitaanzia Dar es Salaam na kisha Dodoma ambako wananchi wa mkoa huo ambao ni makao makuu ya nchi watapata fursa ya kumuaga kabla ya kuagwa Mwanza, Geita na Chato na hatimaye kuzikwa kwa mujibu wa tarehe zitakazotangazwa na Mama Samia.
Amewataka Watanzania kumuombea kiongozi huyo na kuendelea kuwa watulivu.
“Tumempoteza kiongozi wetu. Ametimiza wajibu wake, tunatamani na tungetamani tuwe naye kwa kipindi kirefu lakini Mungu alimleta duniani na ametwaa kiumbe chake. Naomba wananchi kutulia, tusijiingize kwenye vitendo vyovyote, tusipanic (tusiwe na hofu), tusiwe na taraharuki, Serikali inaendelea kuratibu kipindi hiki cha mpito na naamini tutavuta salama,” Dk Abbasi.