Majaliwa aongoza mamia kuuaga mwili wa Jaji Werema

January 2, 2025 3:38 pm · Fatuma Hussein
Share
Tweet
Copy Link
  • Asema atakumbukwa kwa mengi mazuri aliyoyafanya enzi za uhai wake.
  • Mazishi yanatarajiwa kufanyika nyumbani kwake wilayani Butiama, kijiji cha Kongoto, hapo kesho Januari 3, 2025.

Dar es Salaam. Waziri Mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa, amewaongoza mamia ya Watanzania na viongozi wa Serikali kuuaga mwili wa aliyekuwa Jaji Mkuu Mstaafu Frederick Mwita Werema katika viwanja vya Karimjee jijini Dar es Salaam.

Majaliwa aliyekuwa akizungumza leo Januari 2, 2025, kwa niaba ya Rais Samia Suluhu Hassan wakati wa shughuli ya kuuaga mwili Jaji Werema amesema kiongozi huyo atakumbukwa kwa mengi mazuri aliyoyafanya enzi za uhai wake.

“Tunamengi ya kujifunza na kujiendeleza baada ya kuwa tumempumzisha kwenye nyumba yake ya milele,” amesema Majaliwa, akisisitiza kuwa mchango wa Jaji Werema utaendelea kuishi kupitia kazi zake.

Majaliwa ameeleza kuwa Rais Samia anamkumbuka marehemu Jaji Werema kwa weredi, utendaji kazi, na msimamo wake thabiti katika majukumu aliyokabidhiwa, akisema kuwa walishawahi kufanya kazi pamoja.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akizungumza na waombolezaji katika hafla ya kuuaga mwili wa Jaji Frederic Werema. Picha |OWM/X.

Majliwa ameongeza kuwa marehemu Werema alifanya kazi katika mihimili yote ya Serikali, akihudumu katika nafasi mbalimbali muhimu, akiwemo kuwa Wakili wa Serikali, mbunge, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, na Jaji wa Mahakama Kuu.

“Mheshimiwa Rais anajua kuwa marehemu amefanya kazi kwenye mihimili yote ya Serikali,” ameongeza Majaliwa.

Mbali na Majaliwa aliyemuwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan viongozi wengine waliohudhuria shughuli hiyo ni pamoja na Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria Nkasori Sarakikya, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Albert Chalamila.

Kwa upande wake Rais Mstaafu Jakaya Mrisho Kikwete ambaye alikuwa miongoni mwa wazungumzaji katika shughuli hiyo ameeleza Taifa limepoteza mtu muhimu ingawa kila mmoja ana siku yake ya kuja na siku yake ya kuondoka.

“Wengine mnawauguza kwa muda mrefu mpaka mnajua kwamba heee! Afadhari apumzike…kifo na uhai vimeumbwa na Mwenyezimungu sisi tumshukuru Mwenyenzimungu kwa muda aliotupatia kwa kuhudumiwa na Jaji Werema,’’ amesema Kikwete Rais Mstaafu wa Tanzania.

Naye, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Hamza Johari, amesisitiza kuwa ataendelea kumkumbuka marehemu Werema kwa mchango wake mkubwa kwa Taifa, akimtaja kama kiongozi mwenye maono na mtu aliyejitoa kupigania maslahi mapana ya Taifa.

 “Marehemu Jaji Werema alikuwa ni mtu mwenye maono, mtaalam wa sheria, na kiongozi aliye mstari wa mbele katika kuhakikisha sheria na haki vinatumika kuleta maendeleo ya taifa letu,” amesema Johari.

Majukumu aliyoifanya Jaji Werema enzi za uhai wake

Kwa mujibu wa Jaji Johari marehemu Werema alihudumu katika ofisi na taasisi mbalimbali za Serikali ikiwemo Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, alishiriki pia kwenye utafiti na kutoa ushauri kuhusu mabadiliko makubwa ya kikatiba, hususan mfumo wa vyama vingi mwaka 1993.

Marehemu Werema aliteuliwa kuwa Wakili Mkuu wa Serikali na baadaye alikabidhiwa nafasi ya Msaidizi wa Mwanasheria Mkuu mwaka 1984. Mwaka 2009, Rais Jakaya Kikwete alimteua kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, wadhifa aliohudumu hadi mwaka 2014 alipojiuzulu.

Mwili wa marehemu unatarajiwa kuzikwa nyumbani kwake wilayani Butiama, kijiji cha Kongoto, hapo kesho Januari 3, 2025.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Enable Notifications OK No thanks