WHO yaonya kukosekana usawa chanjo ya Uviko-19

September 15, 2021 6:00 am · Mwandishi
Share
Tweet
Copy Link
  • Imesema itapunguza kasi ya mapambano ya ugonjwa huo.
  • Chanjo yatakiwa kupelekwa zaidi bara la Afrika.

Dar es Salaam. Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya Duniani ( WHO) Dk Tedros Ghebreyesus amezitaka nchi zote duniani kutambua chanjo zilizoidhinishwa na shirika hilo kwa matumizi ya dharura dhidi ya Uviko-19 wakati huu ambao bado kuna pengo kubwa la utoaji wa chanjo hiyo hasa  barani Afrika.

Dk Ghebreyesus amesema hayo Septemba 14, 2021 mjini Geneva, Uswisi wakati wa mkutano na waandishi wa habari kuhusu uwiano wa mgao na utoaji wa chanjo dhidi ya Uviko-19 duniani kote.

Tamko hilo la WHO limekuja wakati baadhi ya nchi hazitambui chanjo zingine ambazo zimeidhinishwa na shirika hilo ili kukinga binadamu dhidi ya Corona.

Chanjo zilizoidhinishwa ni pamoja na Pfizer/BioNTech, Astrazeneca ya Korea Kusini, Astrazeneca ya kutoka taasisi ya Serum nchini India, Janssen, Moderna, Sinopharm na Sinovac.

Hadi sasa ni asilimia mbili  tu ya chanjo zote bilioni 5.7 dhidi ya Corona ndio zimekwenda Afrika. 

Dk Ghebreyesus ametaka  kampuni zinazotengeneza chanjo kutoa  kipaumbele upelekaji wa chanjo kupitia mfumo wa Umoja wa Mataifa wa kusambaza chanjo ya Corona (COVAX) na ule wa Muungano wa Afrika (AVAT) kule ambako bado kuna pengo.

Nchi ambazo tayari angalau zimefikia kiwango kizuri cha utoaji chanjo zimetakiwa kupeleka chanjo dhidi ya Corona maeneo yenye uhitaji zaidi sambamba na kupeleka teknolojia rahisi ya utengenezaji wa chanjo kwenye maeneo ambako kumeanzishwa viwanda vya kutengeneza chanjo hizo.

“Sitojali iwapo nitaonekana narudiarudia hoja hii hadi pale ambapo tutafikia uwiano wa chanjo,” amesema Dk Ghebreyesus.

Amesisitiza kuwa kadri ukosefu wa usawa katika mgao wa chanjo utakavyoendelea, virusi vya Uviko-19 vitaendelea kusambaa na kubadilika.

Pia maisha ya kijamii na kiuchumi yataendelea kuvurugika na kutakuwa na fursa kubwa zaidi ya minyumbuliko ya virusi vya Uviko-19 kuibuka na chanjo kushindwa kuwa na ufanisi.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW