Uthabiti na uwezo wa chanjo dhidi ya Uviko-19

August 25, 2021 1:36 pm · Rodgers Raphael
Share
Tweet
Copy Link
  • Chanjo sita zinazotolewa kwa dharura duniani zimehakikiwa usalama wake.
  • Zimepitia hatua muhimu za kimaabara kutoa matokeo mazuri.
  • Katika nchi zinakotolewa zimeonyesha ufanisi mkubwa. 

Dar es Salaam. Ukweli juu ya kazi ya chanjo ya Uviko-19 na uthabiti wake umekuwa ukikosa nafasi miongoni mwa watu walioathirika na habari za upotoshaji ambao wanaamini chanjo hiyo siyo salama.

Kutokana na uelewa tofauti wa chanjo hiyo, baadhi wanasema chanjo ndiyo kwanza inafanyiwa majaribio, wengine mawazo yao ni kuwa chanjo haiwasaidii watu na ni vita ya kiimani.

Wasichokielewa watu hao ni kuwa, ujio wa chanjo ya Uviko-19 umeambatana na kupatikana kwa ahueni dhidi ya maafa ambayo ugonjwa huo ulikuwa ukiyaacha miongoni mwa familia, biashara na hata uchumi wa nchi mbalimbali duniani.

Mathalan, kabla ya ujio wa chanjo hiyo, zipo nchi ambazo zilikuwa zimeweka zuio (lock down) kwa watu wake na usafiri wa kimataifa ulikuwa umepigwa “stop” na hivyo kuathiri sekta mbalimbali ikiwemo biashara, uchumi, utalii na hata afya kwa wengine.

Baada ya kuanza kutoa chanjo, nchi zimefungua mipaka yake na kuruhusu shughuli mbalimbali kuendelea, hivyo kupanda mbegu mpya ya matumaini kwa nchi ambazo uchumi ulianza kutetereka.

Chanjo zinazotolewa na nchi mbalimbali zimethibitishwa na WHO kuwa ni salama. Picha| BBC.

Uthabiti wa chanjo ya Uviko uko wapi?

Chanjo ambazo zinatolewa katika nchi mbalimbali ikiwemo Johnson & Johnson (Jassen) inayotolewa Tanzania zimepitiwa na mamlaka za afya za kimataifa na hata za ndani ya nchi.

Ikumbukwe kuwa, utafiti na majaribio ya chanjo dhidi ya ugonjwa huo  ilianza kufanyika tangu mwanzoni mwa mwaka 2020 ambapo Shirika la Afya Duniani (WHO) lilishirikiana kwa karibu na wanasayansi na kufanikisha kupatikana kwa chanjo hiyo.

Hata baada ya chanjo hizo kuruhusiwa, nchi kupitia wataalam wake zinafanya uchunguzi wa kina ili kujua kama zinawafaa raia wake kulingana na mazingira waliyopo. 

Hata baada ya chanjo kuanza kutolewa rasmi katika nchi mbalimbali, bado mamlaka za afya za nchi husika huithibitisha ili kuona kama imefikia vigezo vya kuwafaa wananchi wake.

Julai 28, 2021 , Waziri wa Afya nchini Tanzania, Doroth Gwajima alisema kuwa chanjo ya Johnson & Johnson inayotumiwa nchini imethibitishwa na WHO na hivyo ni sahihi kutumiwa na Watanzania.

Hata Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan wakati akipata chanjo hiyo alisema kama kiongozi wa nchi ambaye pia anategemewa siyo tu na Watanzania, bali na familia yake pia, hawezi kuyatoa maisha yake kwa kupata chanjo ambayo haina usalama.

Chanjo zenye uthabiti ni zipi?

Kwa mujibu wa WHO, shirika ambalo ndilo mlezi wa afya za watu duniani, chanjo zenye uthabiti wa kutumika ni zile ambazo zimeorodheshwa na shirika hilo kama chanjo zinazoweza kutumika kwa dharura.

Orodha ya WHO inahusisha chanjo ambazo zimepitia hatua zote za utengenezwaji ikiwemo majaribio huku ubora wake ukihakikiwa kutokuwa na madhara kwa wanadamu baada ya kufanya kazi kwa ufanisi wa zaidi ya asilimia 50.

Orodha ya chanjo za Uviko-19 iliyotolewa na WHO ni pamoja na Sinopharm, Pfizer/BioNTech, Astrazeneca, Johnson & Johnson, Sinovac na Moderna.

Fahamu ya kuwa, kupata chanjo kutamsaidia mtu kutokuumwa kiasi cha kulazwa na kuwekewa gesi ya oksijeni pale anapopata ugonjwa wa Corona.

Chanjo za Uviko-19 siyo ya kwanza kutolewa duniani. Kuna chanjo dhidi ya magonjwa mbalimbali ikiwemo polio, kifua kikuu ambazo zimekuwa na matokeo mazuri. 

Hivyo, madai kuwa chanjo za Uviko-19 hazina ufanisi na uwezo kudhibiti ugonjwa huo siyo ya kweli na watu wanahimizwa kujitokeza kwa kwa wingi kuchanjwa. 

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW