Kenya yathibitisha maambukizi mapya ya Ebola, idadi yafikia nane
- Taarifa hii inakuja siku moja baada ya kuripotiwa visa vinne vya ugonjwa huo.
Dar es Salaam. Mamlaka za afya nchini Kenya zimethibitisha mgonjwa wa nane wa Ebola, baada ya mwanaume mwenye umri wa miaka 49 kubainika kuwa na maambukizi hayo kati ya watu 38 waliopimwa Jumapili, Oktoba 18, 2026.
Mkurugenzi Mkuu wa Huduma za Afya nchini humo, Patrick Amoth, ameiambia televisheni ya Citizen TV kuwa mwanaume huyo, ambaye si mhudumu wa afya, alianza kuonesha dalili za homa, maumivu ya kichwa na misuli.
Kwa mujibu wa Amoth, mgonjwa huyo alikuwa akifanya kazi ya kuwahudumia wagonjwa, ikiwemo kusafisha vyombo na mashuka, na anadaiwa kuwa huenda aliambukizwa baada ya kukutana na mgonjwa wa kwanza wa Ebola aliyegunduliwa nchini Kenya mwezi huu.
Taarifa kutoka Wizara ya Afya nchini Kenya zinaeleza kuwa mwanaume huyo alianza kuonesha dalili Jumamosi, Oktoba 17, 2026, kabla ya kutengwa na kufanyiwa vipimo vya kuthibitisha maambukizi ya virusi vya Ebola.
Hatua hiyo imekuja siku moja baada ya wizara hiyo kutangaza wagonjwa wengine wanne wa Ebola, wakiwemo wahudumu watatu wa afya waliomhudumia mgonjwa wa kwanza wa ugonjwa huo nchini Kenya.
Mgonjwa wa kwanza alikuwa mwanaume aliyesafiri kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) kwenda Nairobi, ambako alifariki dunia Oktoba 5, 2026.
Tanzania yaimarisha uchunguzi wa afya mipakani
Wakati mlipuko wa Ebola ukiendelea kuripotiwa katika ukanda wa Afrika Mashariki, Serikali ya Tanzania imeimarisha hatua za uchunguzi wa afya katika mipaka ya nchi, viwanja vya ndege na bandari, kwa lengo la kupunguza hatari ya kuingia na kuenea kwa ugonjwa huo nchini.
Miongoni mwa hatua zilizotangazwa ni kuwafanyia wasafiri uchunguzi wa afya, ikiwemo kupima joto la mwili, katika viwanja vya ndege, mipaka ya nchi kavu na bandari.
Aidha, mtu yeyote atakayeshukiwa kuwa na dalili za Ebola au ugonjwa mwingine wa kuambukiza atafanyiwa uchunguzi na kushughulikiwa kwa kuzingatia taratibu za kitaifa za ufuatiliaji, kinga na udhibiti wa magonjwa.
DRC yaendelea kukabiliwa na mlipuko
Takribani miezi mitano tangu mlipuko wa Ebola ulipoanza kuripotiwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, takwimu zilizotolewa na Kituo cha Ulaya cha Kuzuia na Kudhibiti Magonjwa (ECDC) zinaonesha kuwa hadi Oktoba 13, 2026, nchi hiyo ilikuwa imerekodi visa 9,277 vilivyothibitishwa na vifo 4,478 vilivyohusishwa na mlipuko huo.
Kwa upande mwingine, Uganda, ambayo inapakana na DRC, iliripoti visa 20 vilivyothibitishwa vya Ebola, vikiwemo 15 vilivyotokana na maambukizi kutoka DRC, pamoja na vifo viwili. Hata hivyo, mamlaka za afya nchini humo zilitangaza kumalizika kwa mlipuko huo mwezi Agosti 2026.