Mbinu zitakazowasaidia wajasiriamali kuzalisha bidhaa, huduma bora

November 15, 2022 11:59 am · Mwandishi
Share
Tweet
Copy Link

Mkurugenzi Mtendaji wa NAQT, Safari Fungo (kulia) akiwaongoza watalaam wa masuala ya ubora katika mjadala wa ubora wa bidhaa na huduma uliofanyika Novemba 10, 2022 jijini Dar es Salaam. Picha | NAQT.


  • Ni pamoja na kujenga utamaduni wa ubora kwa kila hatua ya uzalishaji.
  • Kuongozwa na viongozi bora wenye maono.

Dar es Salaam. Wewe ni mjasiriamali unayechipukia au tayari uko katika soko la ushindani na umekuwa ukitafuta sababu ya kwanini biashara yako haikui kwa kasi unayokusudia. 

Huenda umefanya kila jitihada za kujitangaza na hata kuajiri watu wa kukusaidia kusonga mbele lakini bado matokeo siyo mazuri. Changamoto inaweza kuwa ni ubora wa bidhaa au huduma unazotoa kwa wateja wako.

Ubora tangu unatafuta malighafi, uzalishaji mpaka bidhaa au huduma inapomfikia mteja ni lazima ipitie viwango vinavyokubalika katika soko. Ukishindwa kufuata mchakato huo unaweza kuishia kulalamika wakati wenzako wakipenya katika soko la kimataifa. 

Hata hivyo, bado hujachelewa. Unaweza kuanza leo na ukatoboa katika soko la ushindani la bidhaa na huduma.

Novemba 10, 2022, ilikuwa ni Siku ya Ubora Duniani, ambapo kwa Tanzania iliadhimishwa jijini Dar es Salaam kwa Jukwaa la Ubora Tanzania (NQAT) kuwaleta pamoja wasomi, wataalam wa ubora na wajasiriamali kujadili kwa kina suala la ubora na mambo ya kuzingatiwa ili biashara zijengwe katika misingi na utamaduni wa ubora. 

Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya ulinzi ya SGA Security Tanzania, Eric Sambu amesema wajasiriamali wengi hawazingatii ubora wakati wa kutengeneza bidhaa au kutoa huduma lakini wamekuwa wanawaza tu kupata faida.

Sambu ambaye ni mtaalam wa masuala ya uongozi na kodi amesema ikiwa wajasiriamali wadogo kwa wakubwa wakajenga utamaduni wa kuzalisha bidhaa bora, basi uwezekano wa kufanikiwa ni mkubwa hasa nje ya mipaka ya Tanzania.

“Tengeneza vitu vinavyodumu katika fikra za watu na hili haliwezekani kama havina ubora kukidhi mahitaji ya soko,” amesema Sambu wakati akizungumza katika mjadala huo.

Kwa mujibu wa Sambu, utamaduni wa ubora unaanzia kwa kiongozi wa kampuni na kusambaa kwa wafanyakazi wengine ili kukidhi mahitaji halisi ya wateja ambayo hubadilika kulingana na wakati. 

Hilo linawezekana kwa kuanza kubadilisha tabia na kuwaelemisha watu unaofanya nao kazi kutambua thamani ya bidhaa na huduma zinazotolewa huku zikizingatia ukweli.

“Hilo ni suala muhimu la kuzingatia kwa sababu katika masoko ya kimataifa ambayo tunatamani tupeleke bidhaa, kigezo namba moja viwango vya ubora. Tukivuka hapo fursa ni nyingi sana mbele yetu ndani na nje ya nchi,” amesisitiza Sambu.

Kwa mara ya kwanza Siku ya Ubora Duniani iliadhimishwa mwaka 2008 huku akisisitiza kudumisha ubora katika biashara kunamaanisha wateja walioridhika na waaminifu. Bidhaa bora pia husababisha faida ya muda mrefu na ustawi wa kiuchumi.


Soma zaidi: 


Ubora ni zaidi ya bidhaa na huduma

“Hatuwezi kuwa na ubora kama hatuna uongozi bora. Kazi hii siyo nyepesi kuna changamoto nyingi unazotakiwa uzitatue ili ufikie malengo ya kukuza biashara,” amesema mtaalam wa masuala ya utafiti wa kisera na utawala, Dk Haphsa Hincha.

Dk Hincha aliyekuwa akizungumza katika mjadala NQAT amesema kama biashara haina kiongozi bora na mwenye maono haiwezi kukua katika viwango vilivyokusudiwa. 

Bidhaa na huduma hutegemea ubora wa kiongozi wake na watu anaowaongoza.

Mtalaam huyo aliyebobea katika masuala ya usimamizi ya miradi amesema lazima awe na uwezo mkubwa wa kutatua kila changamoto inayoibuka katika biashara yako bila kulalamika kwa sababu kwa kila hatua atakayopiga atakutana na ushindani. 

Kufanikisha ubora wa uongozi wa biashara wenye matokeo chanya kwenye soko la ushindani, Dk Hincha anasema ni lazima kuwe na  nidhamu, uaminifu, kutoa huduma kwa wakati, mawazo ya pamoja katika kuwahudumia wateja na kuwekeza katika rasilimali watu.

“Hakikisha watu unaofanya nao kazi wana afya ya akili iliyo njema ili kuwawezesha kutimiza majukumu yao kwa ufanisi na mwisho wa siku bidhaa na huduma ziwe bora,” amesema mtaalam huyo mbele washiriki wa mjadala wa ubora. 

Ikiwa ubora utazingatiwa katika uongozi wa biashara yoyote basi kuna uwezekano mkubwa bidhaa zitakazozalishwa zikawa na muonekano na uwiano mzuri, mvuto kwa wateja, zikadumu muda mrefu na kutatua changamoto za wateja wako.

“Tuepuke njia za mkato, tubaki katika viwango vya ubora ili tupate matokeo mazuri,” amesisitiza Dk Hincha. 

Hata hivyo, ubora hutegemea dhamira ya dhati ya mtu binafsi na watu wanaowajibika kuhakikisha bidhaa na huduma zinatolewa kwa kiwango kinachotakiwa.

Mkurugenzi Mtendaji wa NAQT, Safari Fungo aliyekuwa akizungumza wakati wa ufunguzi wa mjadala ubora amesema ubora siyo bidhaa na huduma tu bali  ni pamoja na namna bidhaa na huduma inavyomfikia mteja yaani mlaji wa mwisho. 

Fungo amesema kazi yao ni hakikisha ubora unazingatiwa nchini kwa kutoa mafunzo kwa wajasiriamali na wafanyabiashara kujenga utamaduni wa kuendesha mambo yao kwa viwango.

“Tunahakikisha jamii inaweza kuyaishi haya mambo. Kama viwango hivi kwenye jamii haviko vizuri itakuwa ni jamii yenye changamoto kubwa,” amesema Fungo huku akibainisha kuwa mwamko na uelewa wa masuala ya ubora unaongezeka nchini, jambo ambalo linaweza kuwa na matokeo mazuri hapo baadaye. 

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW