Wanawake wajasiriamali walia gharama nembo ya ubora wa bidhaa

December 30, 2021 12:00 pm · Mariam John
Share
Tweet
Copy Link

Kwa wapenzi wa samaki aina ya kambale waliokaushwa vizuri, hiyo nayo ni fursa ya kuinua maisha ya akina mama wa soko la Soni,Wilaya ya Lushoto mkoani Tanga. Picha| K15 Photos.


  • Waiomba Serikali ipunguze masharti ya kuipata.
  • Wasema utoaji uendane na gharama, aina ya biashara.
  • Wabeba matumaini makubwa kukuza biashara mwaka 2022.

Mwanza. Wanawake wajasirimali mkoani Mwanza wameiomba Serikali kupunguza masharti ya upatikanaji wa nembo ya ubora wa bidhaa inayotolewa na Shirika la Viwango Tanzania (TBS) ili kurahisisha mazingira ya ufanyaji biashara zao.

Mwenyekiti wa Chemba ya Wanawake Wafanyabiashara Tanzania (TWCC) Mkoa wa Mwanza, Mariam Munanka amesema ili kupata nembo ya ubora kutoka TBS kunahitajika jengo ambalo thamani yake si chini ya Sh10 milioni.

“Kiwango ni kikubwa na wajasiriamali wengi mitaji yao ni midogo wengi ni chini ya Sh1 milioni, masharti hayo ni ngumu kutekelezeka hivyo ombi letu kwa Serikali mwaka 2022 kipengere hicho kiboreshwe ili wajasiriamali waweze kumudu,” amesema Munanka wakati akiongea na Nukta Habari.

Mjasirimali anayejishughulisha na kusaga unga wa lishe kwa ajili ya uji wa watoto, Arian Mussa ni amekiri kuwa gharama za kufungua ofisi inayokidhi vigezo vya ubora ziko juu hivyo kuna umuhimu wa kuzipitia upya ziendane na halisi ya maisha.

Hata hivyo, TBS imeeleza kuwa Serikali hutenga fedha kila mwaka kwa ajili ya kuhudumia wajasiriamali wadogo na wa kati pale wanapoomba bidhaa zao wanazozizalisha wenyewe zithibitishwe ubora. 

“Kati yao wapo ambao wanasamehewa kulipa ada yoyote kwa sababu ya mitaji yao kuwa midogo,” imeeleza TBS katika ufafanuzi wake kuhusu nembo ya ubora.

 Ili kupata msamaha huu, mjasiriamali anatakiwa kuwa na leseni ya biashara na kupata barua ya utambulisho kutoka Shirika la Viwanda Vidogo Vidogo Tanzania (SIDO).

Wajasiriamali waliokwishapata leseni ya kutumia alama ya ubora wanapaswa kutunza taarifa za uzalishaji na mauzo ambazo watatakiwa kuzionesha kwa wakaguzi wa TBS pindi zinapohitajika.


Zinazohusiana


Mlolongo mrefu wa kupata vibali vya biashara nayo imekuwa changamoto kwao kufanikiwa katika shughuli za ujasiriamali.

“Tumekuwa tukipokea mafunzo kutoka sehemu mbalimbali kukuza uchumi wetu lakini bado kuna changamoto pale tunapotaka kusajiri biashara zetu na kupatiwa nembo ya biashara mlolongo unakuwa mrefu,” amesema Elizabeth Marko, mjasirimali anayetengeneza ubuyu.

Amesema  kuwajengea wanawake uwezo wa kukuza uchumi wao na  kaya ni njia ya haraka ya kuibadilisha jamii na kuleta maendeleo.

Amesema jitihada za wanawake huwa na matokeo makubwa kwenye jamii nzima kwa sababu wanawake wanapofanikiwa mara nyingi wanawekeza mapato yao katika familia na jamii zao.

“Katika dunia ya leo wanawake wamebeba mzigo mkubwa katika kuhudumia mahitaji ya familia, ni ombi letu tunapoanza mwaka 2022 tunahitaji maboresho kwenye vipengele hivyo lakini pia kipengele cha kupata mikopo iongezwe ili iwasaidie wanawake kuongeza mitaji yao,” amesema Elizabeth.

Mjasiriamali anayeotesha miche ya miti, Violeth Muhamusi amesema mwaka 2022 angetamani kuona vijana wanohitimu vyuo wakishirikishwa katika masuala ya ujasirimali ili kuondokana na tatizo la utegemezi wa ajira.

“Wanawake wanatakiwa kuendelea kuchukua hatua na kuachana na fikra za utegemezi ikiwemo kujiunga na vikundi mbalimbali vya maendeleo ili kuwawezesha kukuza uchumi wao,” amesema mjasiriamali huyo.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW