Fursa mafunzo ya uhifadhi maliasili kwa wanahabari Tanzania
- Yatatolewa na Nukta Africa kwa ufadhili kutoka katika Shirika la Maendeleo ya Kimataifa la Marekani (USAID) kupitia mradi wa USAID Tuhifadhi Maliasili.
- Ni mafunzo ya uhifadhi wa bioanuai yatakayosaidia kuzalisha maudhui yatakayotunza mazingira na maliasili.
- Wanahabari watakaonufaika ni kutoka mikoa ya Arusha, Manyara, Morogoro, Lindi, Tanga na Pwani.
Dar es Salaam.Wanahabari wa vyombo vya habari vilivyopo katika baadhi ya shoruba nchini watanufaika na mafunzo ya uhifadhi wa bioanuai yatakayosaidia kuzalisha maudhui yatakayotunza mazingira na maliasili.
Mafunzo hayo muhimu kwa mustakabali wa kizazi kijacho, yatatolewa na Nukta Africa kwa ufadhili kutoka katika Shirika la Maendeleo ya Kimataifa la Marekani (USAID) kupitia mradi wa USAID Tuhifadhi Maliasili.
Fursa hiyo mpya ya mafunzo ni mwendelezo wa jitihada za Watu wa Marekani katika kutoa elimu kwa wanahabari katika kutunza maliasili.
Mafunzo hayo, yanayotarajiwa kuanza Novemba 2023, ni maalum tu kwa waandishi wa habari, wazalishaji (producers) na wahariri wa baadhi ya vyombo vya habari visivyo vya kitaifa vinavyopatikana katika shoruba za Kwakuchinja, Amani-Niro na Nyerere Selous Udzungwa.
Mradi huu wa mwaka mmoja unalenga kuwawezesha wanahabari wa vyombo vya habari vya kijamii na mikoa iliyopo karibu au pembezoni mwa shoroba hizo kuandika habari zenye ubora wa hali ya juu zinazochagiza uhifadhi endelevu wa maliasili.
Wanahabari watakaobahatika kupata mafunzo hayo mbali na kujifunza masuala ya uhifadhi wa bioanuai, pia watajifunza uandishi wa habari za takwimu, matumizi ya zana za kidijitali kuzalisha habari za uhifadhi na uthibitishaji habari (Fact-checking).
Soma zaidi
-
Mapato vituo vya makumbusho ya taifa yaendelea kupaa Tanzania
-
Mataifa 10 yaliyoongoza kuleta watalii wengi Tanzania Oktoba 2022
Wanahabari mikoa hii kunufaika
Wanahabari watakaonufaika na mradi huu ni kutoka mikoa sita ya Tanzania Bara ya Arusha, Manyara, Morogoro, Lindi, Tanga na Pwani.
Shughuli zitakazofanyika chini ya mradi huu ambao ni pamoja na namna ya kuripoti habari za wanyamapori, baiyoanuai, utalii, mazingira, na matumizi ya teknolojia ya kidijitali na takwimu katika kuzalisha habari zenye mchango mkubwa kwa jamii.
Pia wanahabari watakaoteuliwa katika mradi huu ujulikanao kama “Habari Bora kwa Uhifadhi Endelevu” watapata fursa ya kutembelea shoroba hizo tatu ili kuongeza uelewa wa masuala ya uhifadhi na kukutana na wataalamu mbalimbali na wadau wengine wa uhifadhi maliasili.
Mkuu wa Utafiti na Mafunzo, Daniel Samson amesema wanahabari watakaofanya vizuri wakati wa mafunzo watapata fursa nyingine ya kujifunza zaidi kutoka kwa wakufunzi wa Nukta Africa na washirika wake ili kubobea katika uandishi wa habari za uhifadhi wa maliasili na teknolojia za kisasa za uandishi wa habari.
Wanahabari watakaofanya vema watavipatia vyombo vyao tiketi ya kupewa zaidi mafunzo na ushauri elekezi namna ya kuongeza thamani ya maudhui ya uhifadhi na kuimarisha mifumo ya uandishi wa habari kidijitali yaani kwa kimombo ‘Digital transformation’ katika vyumba vyao vya habari ikiwemo kuboreshewa tovuti.
“Kipaumbele kimewekwa kwa wanahabari vijana, wanawake na watu wenye ulemavu na wale wote wanaopenda au waliobobea kuandika habari za uhifadhi maliasili ikiwemo utalii na mazingira,” amesema Samson.
Wanufaika wa mradi huu
Wanufaika wa moja kwa moja wa mradi huu ni waandishi wa habari na wazalishaji vipindi 45 na wahariri 15 kutoka katika vyombo vya habari 15 katika mikoa sita iliyotajwa hapo juu.
Mafunzo hayo ya aina yake ni mwendelezo wa kampuni ya habari na teknolojia ya Nukta Africa kuongeza ujuzi katika sekta ya habari baada ya kuwa moja ya kuwa miongoni mwa washirika mahiri katika utekelezaji wa mradi wa USAID Boresha Habari uliokuwa ukisimamiwa na Internews.
Tangu kuanzishwa kwake takriban miaka sita iliyopita, Nukta Africa imeshatoa mafunzo kwa wanahabari, wahariri, wazalishaji maudhui na wataalamu wa mawasiliano takriban 2,000 katika nyanja mbalimbali hasa matumizi ya teknolojia na takwimu na uhifadhi wa mazingira na nishati safi.
Wanahabari ambao watakaofurahi fursa hii watatakiwa kutuma maombi kwa kujaza fomu hii >> https://forms.gle/65ynyPvRB6N12Wo77. Mwisho wa kutuma maombi ni Septemba 10, 2023. Wanahabari watakaoteuliwa pekee ndiyo watakaojulishwa.