Mambo yatakayosaidia wajasiriamali kupenya soko la kimataifa
- Ni kuzingatia viwango vya ubora katika uzalishaji.
- Sekta binafsi kushirikishwa na kuwajengea uwezo wajasiriamali.
- Kuendelezwa kwa tuzo za ubora za Afrika Mashariki nako kwatajwa.
Dar es Salaam. Wafanyabiashara Afrika Mashariki wametakiwa kuzalisha bidhaa na kutoa huduma zenye ubora na viwango ili kufaidika zaidi na soko la kimataifa lenye faida lukuki.
Miongoni mwa masoko muhimu la kimataifa kwa wajasiriamali ni Eneo la Biashara Huria la Afrika (AfCFTA) ambalo ni makubaliano ya biashara huru ya Afrika kati ya nchi 54 wanachama wa Umoja wa Afrika (AU).
Mkataba huo ulitiwa saini Kigali, Rwanda Machi 21, 2018 ikiwa na lengo kurahisisha uuzaji wa bidhaa katika bara hilo bila vikwazo.
Mkurugenzi wa Biashara wa Jumuisha ya Afrika Mashariki (EAC), Rashid Kibowa ameeleza leo Oktoba 20 jijini Dar es Salaam wakati wa utoaji wa tuzo za ubora za Afrika Mashariki kwa mwaka 2022 kuwa moja ya changamoto inayowakabili wafanyabiashara wa EAC ni kuzalisha bidhaa zenye ubora wa chini.
Amesema changamoto hiyo inafanya biashara za wafanyabiashara wengi katika ukanda huu zisivuke mipaka ya jumuiya hiyo na hivyo kushindwa kushindana na wafanyabiashara wengine wa Afrika na kimataifa.
“Tunatakiwa kujiimarisha ili kushindana na watu wengine duniani,” amesema Kibowa.Kibowa amesema kuna muamko mkubwa wa wajasiriamali kuzalisha bidhaa ili kujipatia kipato lakini wengi wao hawana ujuzi na maarifa yanayowawezesha kuzingatia viwango vya ubora vya kimataifa.
Kutokana na hali hiyo, nchi za EAC zinaagiza zaidi bidhaa mbalimbali kutoka nje na kulazimika kusafirisha malighafi kama mazao ya kilimo ili yakachakatwe nje na kurejeshwa tena katika nchi zao.

Washindi wa tuzo za ubora za Afrika Mashariki kwa mwaka 2022 waliotangazwa leo jijini Dar es Salaam. Washindi hao wanatoka Tanzania, Uganda, Burundi na Rwanda. Picha| EACMarkup.
Njia za kuongeza ubora
Amesema kuna umuhimu wa kuwajengea uwezo wafanyabiashara na wajasiriamali wakubwa kwa wadogo katika michakato yao yote ya utengenezaji bidhaa kuhakikisha suala la viwango vya ubora haliachwi nyuma. Njia nyingine itakayosaidia wazalishaji wa bidhaa kushindana na wenzao wa Afrika na kimataifa ni kuwaondolea vikwazo mbalimbali ikiwemo kodi na masharti magumu ya kusafirisha bidhaa kutoka nchi moja kwenda nyingine.
Frank Dafa, Meneja Sera za Viwango wa Baraza la Biashara la Afrika Mashariki (EABC) amesema katika jumuiya hiyo wanaendelea kuondoa vikwazo vinavyowarudisha nyuma wafanyabiashara na kuwafungulia fursa za kufaidika na masoko ya bidhaa ya kimataifa.
“Afrika Mashariki tumekuwa na hatua mbalimbali zinazochukuliwa kuweka mifumo ya kuoanisha sheria zetu za bidhaa ili kuhakikisha haziwi kikwazo kwenye biashara,” amesema Dafa.
Soma zaidi:
Wafanyabiashara wawekewa mkakati
Katika kuongeza motisha ya wafanyabiashara na wajasirimali kuzalisha bidhaa zinazoweza kupenya katika soko la ushindani la kimataifa, wadau wa biashara wameanzisha tuzo za ubora za Afrika Mashariki.
Kwa mujibu wa Mratibu wa tuzo hizo, Safari Fungo amesema tuzo hizo zinatolewa kwa mara ya kwanza kuwahamasisha wazalishaji wa bidhaa kutambua umuhimu wa kutoa bidhaa zenye ubora zitakazowahakikishia soko zuri kimataifa.
Amesema tuzo hizo zikitekelezwa vizuri zitachochea ushindani wa biashara, upatikanaji wa masoko ya kimataifa, kuimarisha ushirikiano wa EAC na kuyatambua mashirika na watu wanaofanya vizuri katika uzalishaji.