Huduma, bidhaa bora: Tiketi ya kuwavusha wajasiriamali kimataifa
- Watakiwa kuzingatia ubora kwa bidhaa na huduma wanazotoa.
- Hiyo itawasaidia kulifikia soko la kimataifa kwa urahisi.
Dar es Salaam. Ikiwa zimebaki siku chache kuelekea Siku ya Ubora Duniani, wajasiriamali, watoa huduma na wazalishaji nchini Tanzania wametakiwa kuzingatia ubora wanapozalisha bidhaa na kutoa huduma zao kwa wateja ili kuongeza wigo masoko na mapato.
Siku ya Ubora Duniani huadhimishwa Novemba 10 kila mwaka na dhima ya ya mwaka huu ni “Dhamiri ya ubora Kufanya jambo sahihi”.
Ubora, ni mojawapo ya tiketi ya kuongeza masoko yakiwemo ya nje ya nchi ambapo bidhaa za Watanzania zitaweza kushindana na bidhaa za wazalishaji wengine wa kimataifa.
Mkurugenzi wa Jukwaa la Ubora Tanzania (NQAT) Safari Fungo amesema ubora unatofautisha bidhaa inayofaa na isiyofaa hivyo ni vyema wazalishaji na watoa huduma wa wakalizingatia hilo kama wanahitaji kukuza biashara zao na wigo wa masoko.
“Watanzania wanataka kitu bora. Wanapoingia kufanya manunuzi na kuchagua huduma, mara kwa mara wanaangalia ni bidhaa ipi inasifika kwa ubora na huduma ipi inayotolewa sifa nzuri. Wazalishaji na watoa huduma wakilifahamu hilo, wataanza kuwekeza katika masuala ya ubora,” amesema Fungo.
Licha ya kusisitiza ubora wa bidhaa na huduma, NQAT imekuwa ikitoa mafunzo na semina kwa wafanyabiashara na wajasiriamali namna ya kuzalisha bidhaa zenye viwango na ubora wa kushindana kimataifa.
Soma zaidi:
Taasisi na wadau katika nyanja ya ubora kote ulimwenguni huadhimisha alhamsi ya pili ya mwezi wa Novemba kama Siku ya Ubora Duniani ili kuchochea uelewa wa ubora na inatumika katika kutambua juhudi na michango ya wadau mbalimbali katika kuendeleza tasnia ya ubora.
Ni fursa ya kusherehekea mafanikio waliyopata wadau mbalimbali kwa maana ya makampuni pamoja na watu binafsi katika tasnia ya ubora kwenye kipindi cha mwaka mmoja toka kusherehekea siku ya ubora kwa mwaka uliopita.
“Kaulimbiu ya Siku ya Ubora Duniani ya mwaka huu inatoa fursa ya kutafakari jinsi utamaduni, matendo na dhamiri zetu namna zinaweza kusaidia au kuzuia kufanya maamuzi na ‘kufanya jambo sahihi’ kwa washikadau wote,” amesema Fungo wakati akizungumza na wanahabari mwishoni mwa wiki.
Ikiwa viwango vya ubora vilivyoweka katika nchi na kimataifa vitazingatiwa itasaidia kuongeza uwajibikaji siyo tu kwa wanahisa/mlipakodi, wateja na wafanyikazi, lakini mazingira na jamii kwa ujumla.
Hitaji la wafanyabiashara kutumia dhamiri katika kufanya maamuzi katika kila ngazi huzuia matatizo magumu zaidi ya kimaadili. “Falsafa kubwa katika hili, ni kufanya jambo sahihi wakati hakuna mtu anayekuangalia.” amesema Fungo.
Wazalishaji na watoa huduma wakilifahamu hilo, wataanza kuwekeza katika masuala ya ubora hivyo dhamiri ya ubora katika kufanya jambo linalofaa ni jambo ambalo halikwepeki.
Fungo amesisitiza kuwa usimamizi wa ubora siyo tu kuhusu kuboresha ubora wa bidhaa na huduma, lakini pia inahusisha namna ambavyo makampuni yanafikisha bidhaa au huduma kwa wateja katika mnyoyoro mzima wa thamani ili kuhakikisha kunakuwa na viwango vya juu katika kuwaridhisha wateja.
Latest
