Mbinu zinazoweza kuwasaidia wajasiriamali kunufaika na fursa zinazowazunguka

Daniel Mwingira 0056Hrs   Februari 05, 2018 Habari
  • Kujituma, kujiamini na hamu ya kuongeza mtandao wa kujifunza na kufanya nao biashara ndiyo nguzo kwa kila mjasiriamali.


Arusha. Vijana wenye ndoto za kuwa wajasiriamali wametakiwa kujituma na kuacha uoga ili kutumia vyema fursa zilizopo mbele yao kwa kuchangia kutatua matatizo yanayoikabili jamii. 

Sisty Basil, Mratibu wa taasisi ya Energy Change Lab Tanzania alieleza wakati wa tamasha la Energy Safari 2018 lililofanyika jijini hapa kuwa vijana wengi wa Tanzania ni waoga wa kujaribu vitu na hata kujenga mtandao wa kibishara pale wanapopata nafasi ya kukutana na watu muhimu katika kuendeleza mawazo au biashara zao.

Tamasha la Energy Safari ambalo limefanyika kwa mara ya pili tangu kuanzishwa mwaka 2015, huwakusanya vijana  na kampuni mbalimbali zinazojihusisha na nishati mbadala hapa nchini. Katika tamasha la mwaka huu vijana 31 walifanikiwa kushiriki baada ya kufanikiwa kupita katika mchujo uliowahusisha waombaji 201 ikilinganishwa na waombaji 101 wakati linaanzishwa miaka mitatu iliyopita.

                                                                Sisty Basil, Mratibu wa taasisi ya Energy Change Lab Tanzania.

Basil amewataka vijana kuheshimu kila kitu wanachofanya na kutumia muda wao kwa ungalifu zaidi na kwamba matamasha kama Energy Safari ni njia bora ya kujenga mtandao mzuri wa kibiashara.

 Meneja wa vijana wa Energy Change Lab, Nuria Mshare amesema alikuwa anatarajia vijana wangekuja na kushiriki kama matamasha mengine na kuondoka bila  matokeo makubwa sana lakini mwishoni wa tamasha alishangazwa kuona vijana walijituma na kutumia muda mfupi kutatua matatizo makubwa katika jamii.

"Kwa kweli vijana walioshiriki katika tamasha hili tulitegemea matokeo fulani kutoka kwao na malengo hayo kwangu yamezidi matarajio. Ni furaha kuona kwa kutumia zile mbinu tulizowafundisha kutatua matatizo katika jamii kama nadharia ya U (U theory) wameweza kutatua changamoto hizo na kuongezea ubunifu waliokuwa nao," Mshare ameiambia Nukta. 

Mshare amesema lazima vijana wajue kuwa wana uwezo mkubwa ndani yao hivyo wana jukumu kubwa la kutatua matatizo hayo na siyo lazima mpaka mtu atoke nje ili kutoa suluhu ya matatizo ya taifa.

"Ni vyema kwa kila  mshiriki wa Energy Safari 2018 kwenda mtaani na kuwa balozi mzuri wa nishati jadidifu na pia akatatue changamoto katika eneo lake," anasema.


Washiriki wanena

Mwanaharakati Neema Samweli kutoka Serengeti mkoani Mara anasema aliiona fursa ya kushiriki tamasha hilo kupitia mtandao wa Opportunities For Africans jambo linaloonyesha nguvu ya mtandao katika kutoa fursa zaidi kwa vijana. 

"Ilikuwa ni nafasi ya kipekee  kwangu kuja kujifunza kuhusu umemejua ili nikirudi Serengeti niweze kuwakomboa wakinamama kwenye kilimo hata kuja na kilimo cha umwagiliaji kwa kutumia mashine za nishati jadidifu,’’anasema Samweli.

                                           Mwanaharakati Neema Samweli akieleza jambo wakati wa Tamasha la Energy Safari 2018. 

Anasema kuna tofauti kubwa kiuelewa kuhusu nishati jadidifu baada ya kujifunza kuhusu nishati  hiyo katika tamasha hilo na kukutana na vijana wengi wakiwemo wadogo waliogundua mambo makubwa jambo lilompa imani kuwa  hakuna kinachoshindikana iwapo utajituma.

"Matamasha kama haya ni mazuri ni vema waandaji wakaendelea kuyaandaa kila mwaka  kwa kuwa yanawasaidia sana vijana," anasema Samweli. 

Mbali na kuwa na washiriki wa ndani ya nchi, tamasha hilo ambalo ni miongoni mwa machache yanayofanyika nchini katika kukuza vipaji na kubuni miradi ya kibunifu katika nishati, lilishirikisha vijana wengine wa nje ya nchi akiwemo Turner Adornetto kutoka jimbo la Ohio nchini Marekani.

Adornetto anayesomea uhandisi wa umeme amesema amejifunza mengi kutoka katika tamasha hilo licha ya kuwa Marekani imeendelea katika masuala ya kinishati. 

Mshiriki huyo kutoka Marekani anasema amejifunza vitu vingi anaeleza Marekani watu wanapenda kutumia nishati mbadala ila  hawewezi kutokana  labda na sheria au sera lakini kwa Tanzania ameona watu wengi wanatumia nishati hiyo mbadala kwa uhuru na urahisi zaidi.

"Watu wengi wanatamani kutumia nishati mbadala Marekani na hata hapa Tanzania. Nilipofika Tanzania nilishangaa sana  kila mtu anaweza kwenda kununua vifaa vyake vya sola dukani  au kutafuta nishati nyingine mbadala  wakati upande wa  Marekani mtu hawezi kufanya hivyo sijui kwanini inawezakana ikawa sera au sheria,’’anasema Adornetto.

                        Mshiriki wa tamasha la Energy Safari 2018 kutoka  Ohio nchini Marekani akishiriki moja ya mazoezi ya kijasiriamali. 

Mwanafunzi huyo anasema amejifunza sana kuhusu uwezo wake wa kuwa kiongozi kwa kufanya kazi na vijana wenye elimu mbalimbali na mawazo tofauti na amefurahi kuona vijana wakizungumzia mada ya nishati jadidifu ambayo ni muhimu kwa sasa kutokana na mabadiliko ya tabianchi.

"    Nashauri muda uongezwe ili kuwapa vijana fursa zaidi ya kuweza kutatua matatizo hayo ya nishati jadidifu kwa ufanisi zaidi," Ukeme ofon Etuknwa  kutoka Nigeria.


 Ukeme ofon Etuknwa  kutoka Nigeria mwenye koti la bluu akisikiliza maelezo kutoka wataalamu wa Enda Solar.


Related Post