31 wafutiwa matokeo darasa la saba kwa udanganyifu, matusi
- Kati ya watahiniwa hao, watahiniwa 26 wamebainika kufanya udanganyifu huku watano wakifutiwa matokeo yao baada ya kuandika lugha za matusi.
Dar es Salaam. Baraza la Mitihani Tanzania (Necta) limefuta matokeo ya watahiniwa 31 waliofanya Mtihani wa Kumaliza Elimu ya Msingi (PSLE) mwaka 2026 kutokana na udanganyifu na matumizi ya lugha za matusi katika karatasi za kujibia.
Kati ya watahiniwa hao, watahiniwa 26 wamebainika kufanya udanganyifu huku watano wakifutiwa matokeo yao baada ya kuandika lugha za matusi katika mitihani.
Akizungumza wakati wa kutangaza matokeo hayo leo, Novemba 3, 2026, jijini Dar es Salaam, Katibu Mtendaji wa Necta, Profesa Said Mohamed, amesema hatua hiyo imechukuliwa kwa mujibu wa sheria na kanuni zinazosimamia uendeshaji wa mitihani ya kitaifa.
“Matokeo hayo yamefutwa kwa mujibu wa Kifungu cha 5(2)(i) na (j) cha Sheria ya Baraza la Mitihani, Sura ya 107, pamoja na Kifungu cha 30(2)(b) cha Kanuni za Mitihani za mwaka 2016,” amesema Profesa Mohamed.
Milango ya kurudia mtihani ipo wazi
Hii si mara ya kwa kwanza kwa watahiniwa kufutiwa matokeo kuokana na kuandika matusi au kufanya udanganyifu katika mitihani mbalimbali ya kitaifa licha ya Necta kuonya na kuendelea kutoa adhabu.
Katika mtihani wa Kidato cha Nne (CSEE) wa mwaka 2025, Necta ilifuta matokeo ya watahiniwa 79, ambapo 77 walibainika kufanya udanganyifu na wawili kuandika lugha ya matusi katika karatasi zao za kujibia.
Aidha, katika mtihani wa kumaliza elimu ya msingi wa mwaka huo, watahiniwa 38 walifutiwa matokeo, wakiwemo 31 waliofanya udanganyifu na saba walioandika lugha ya matusi.
Hata hivyo, Profesa Mohamed amebainisha kuwa kufutiwa matokeo si mwisho wa safari ya elimu kwa watahiniwa hao, baraza linatoa nafasi ya kurudia mitihani kwa kuzingatia sheria na taratibu zilizowekwa na Baraza hilo.
“Kama mnavyojua, sera yetu ya elimu sasa inaelekeza elimu ya lazima ya miaka 10, na wanafunzi hawa wanatakiwa kufika mpaka kidato cha nne,” amesema Profesa Mohamed.