Udanganyifu kidato cha nne waongezeka, Necta ikifuta matokeo ya watahiniwa 102
- Idadi ya waliofutiwa matokeo imeongezeka kutoka 75 wa mwaka 2020.
- Watahiniwa hao walifanya udanganyifu katika mitihani yao.
Dar es Salaam. Baraza la Mitihani la Tanzania (Necta) limefuta matokeo ya watahiniwa 102 waliobainika kufanya udanganyifu katika mitihani ya kidato cha nne uliofanyika mwishoni mwa mwaka jana huku udanganyifu ukiongezeka.
Akizungumza na vyombo vya habari leo jijini Dar es Salaam, Katibu Mkuu wa Necta, Dk Charles Msonde amesema wanafunzi hao ni kati ya wanafunzi 483,820 waliofanya mtihani wa kidato cha nne mwaka 2021.
“Kati ya watahiniwa waliobainika kufanya udanganyifu watahiniwa 83 ni wa Upimaji wa kitaifa wa darasa la nne, 27 ni wa upimaji wa kitaifa wa kidato cha pili, 102 ni wa mtihani wa kidato cha nne na watahiniwa wawili ni wa mtihani wa maarifa,” amesema Dk Msonde.
Ikilinganishwa na matokeo ya kidato cha nne ya mwaka 2020, mwaka huu wanafunzi wengi zaidi waliohusika kufanya udanganyifu kwenye mitihani ya kidato cha nne ikiwa ni ongezeko la wanafunzi 27.
Mwaka jana, ni wanafunzi 75 tu ndiyo walifanya udanganyifu katika mtihani huo.
Soma zaidi:
-
Shule 10 bora matokeo ya kidato cha nne 2021
-
Mwanafunzi bora kidato cha nne 2021 ataja siri za ushindi
-
Matokeo kidato cha nne 2021 hadharani
Baraza hilo limesema limefuta matokeo ya wanafunzi hao kwa mujibu wa kifungu cha 5 (2) (i) na (j) cha sheria ya Baraza la Mitihani sura ya 107 kikisomwa pamoja na Kifungu cha 30(2) (b) 2016 cha Kanuni za Mitihani.
Necta pia imezuia matokeo ya wanafunzi 555 ambao walipata matatizo ya kiafya na hivyo kushindwa kufanya mitihani yote au baadhi.
“Watahiniwa wahusika wamepewa fursa nyingine ya kufanya upimaji wa mtihani hii ya kitaifa mwaka huu wa 2022,” amesema Dk Msonde.
Latest